ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 23, 2012

Tanesco hoi, mgawo wa umeme mkali waja


  Maji yapungua Mtera
  Madeni hayabebeki
  Mkopo wa benki mgumu
Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
Ni miujiza tu itaponya nchi isiingie tena kwenye giza kwani kuna kila dalili kwamba mgawo mkali wa umeme ni kitu kisichoepukika kwa sasa.

Hali ya maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme ni mbaya, huku Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) likikabiliwa na ukata mkubwa ambao unalifanya kushindwa kuendesha vyanzo vya umeme wa mafuta na gesi, nyaraka mbalimbali ambazo NIPASHE imeziona na ambazo Bodi ya Shirika limepewa zinaonyesha.

Hali ya kina cha maji katika bwawa kuu la Mtera ni mbaya, huku hali ikiwa siyo ya kuridhisha katika mabwawa ya Kidatu New Panga Falls na Nyumba ya Mungu, hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kuathiri uzalishaji wa umeme kwa nguvu za maji katika gridi ya taifa.



Mbali na kupungua kwa vina vya maji katika mabwawa hayo, matatizo ya fedha ya Tanesco kwa sasa ni kama hayabebeki na kinachoendelea kati ya Shirika hilo na Wizara ya Nishati na Madini ni kama kuwindana huku matatizo sugu ambayo yameelemea shirika yakikaa bila kupatiwa ufumbuzi, hasa fedha ambazo ziliahidiwa bungeni wakati wa mkutano wa bajeti ya mwaka 2011/12 kwamba zingelipatikana. Hadi sasa ni kiza kinene.

Taarifa zinaonyesha kuwa kutokana na kuegemea zaidi kuzalisha umeme kwa nguvu za maji hasa tangu mwanzoni mwa mwaka huu kutokana na kukosekana kwa fedha za kununua mafuta ya kuwasha mitambo ya mafuta mazito, na baada ya msimu wa mvua za masika kufikia mwisho bila maji mengi kuingia katika bwawa la Mtera, hali katika kipindi cha Juli hadi Desemba inaweza kuwa mbaya zaidi kama fedha hazitapatikana kuwasha mitambo hiyo.

Taarifa za bodi zinasema kuwa kama matumizi ya maji ya Mtera ambalo ndilo pia hutegemewa na bwawa la Kidatu yataendelea kutumia kwa sasa na kwa kasi iliyoanza mwanzoni mwa mwaka huu, yatasababisha kina cha maji kufikia kina cha mita 688 juu ya usawa wa bahari, ifikapo Disemba mwaka huu. Kina hicho ni karibu kabisa na kina cha mita 687.5 ambacho ni lazima uzalishaji wa umeme usimame kitaalam.

Hakuna uwezekano wowote mkubwa wa hali ya maji katika bwawa la Mtera na mto mkuu wa Ruaha kubadilika hasa kutokana mvua za masika kufikia mwisho bila kuwa na maji mengi katika msimu wa mwaka huu.

Ingawa bodi ya Tanesco na Wizara wameelezwa kuwa ili kuokoa hali ya vyanzo vya umeme wa maji ni lazima kuelekeza nguvu zaidi kwenye vyanzo vya mafuta na gesi katika kipindi hiki cha kiangazi katika kuzalisha umeme, kinachoonekana kushika kasi sasa ni kutafutana uchawi kama ambavyo imetokea kwa kusimamishwa kazi kwa maofisa wanne waandamizi wa Tanesco, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Mhandisi William Mhando, Naibu Mkurugenzi, Huduma za Shirika, Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa Fedha, Lusekelo Kassanga na Meneja Mwandamizi Manunuzi, Harun Mattambo.

Kabla ya kufikiwa uamuzi wa kuwang’oa kwa muda vigogo wa Tanesco, bodi hiyo inayodaiwa kugawanyika kwa hatua zilizochukuliwa, ilielezwa kuwa tangu kukosekana kwa mafuta ya mitambo ya kukodi, uzalishaji wa umeme wa maji uliongezeka kutoka MW 154 Disemba mwaka jana hadi MW 270, lakini uhaba wa mafuta ulipoanza mwishoni mwa Februari mwaka huu ulifanya uzalishaji umeme uelemee zaidi mitambo ya nguvu za maji ili kukidhi mahitaji ya watumiaji bila kuwepo kwa mgawo.

Taarifa zaidi za uchunguzi zilizoifikia  NIPASHE zinaonyesha kuwa hali hiyo ilipunguza vina vya maji katika mabwawa ya Mtera na Kidatu zaidi ya ilivyotarajiwa.

Takwimu zinaonyesha kuwa hadi Julai mosi mwaka huu kina cha maji katika bwawa la Mtera kilikuwa ni mita  690.80, Kidatu 443.70, Kihansi 1145.10 New Pangani Falls 117.39 na Nyumba ya Mungu 684.21 juu ya usawa wa bahari, lakini kwa kuwa mvua zimekata na fedha za kununua mafuta ya kuendesha mitambo ya mafuta zikizi kuwa ndoto, vina hivyo vinakadiriwa kuwa vitapungua kwa kasi sana kwa sababu ndivyo vinazalisha umeme mwingi kwa sasa.

Wataalam wa Tanesco wamelithibitishia gazeti hili kuwa endapo bwawa la Mtera na Kidatu yatasimama kuzalisha umeme kutokana na kupungua kwa maji hakuna mradi wa umeme utakaoweza kuokoa tatizo hilo.

“Endapo vituo vya Mtera na Kidatu vitafungwa kutakuwa na tatizo la uhaba wa maji utaathiri kiwango cha umeme  kwenye gridi ya Kaskazini Magharibi (North West Grid) inayopeleka umeme kuanzia Dodoma, Singida, Shinyanga, Mwanza, Tabora, Musoma na maeneo ya jirani,” kilisema chanzo chetu kwa masharti ya kutokutajwa gazetini.

Meneja wa Tanesco anayesimamia uzalishaji umeme katika Bwawa la Mtera, Anthony Mbushi, alinukuliwa na vyombo vya habari Juni 21 mwaka huu akitaja sababu kubwa iliyosababisha kina cha maji kupungua katika bwawa hilo kuwa na matumizi mabaya ya maji yanayofanywa na wakulima wa kilimo cha umwagiliaji wa zao la mpunga katika tarafa ya Pawaga.

Wakulima wa vijiji vinavyolizunguka bwawa hilo pamoja na wafugaji ambao wanaharibu vyanzo vya maji vinavyotiririsha maji hayo kwenda bwawa la Mtera kwa kulisha mifugo yao, nao wanadaiwa kuongeza ukubwa wa tatizo.

UZALISHAJI UMEME

Tathmini ya Tanesco inasema kuwa mahitaji ya nishati ya umeme kuanzia Julai hadi Disemba mwaka huu yatafikia ni utafikia MW 833.

Katika kipindi hicho, mitambo ya nguvu za maji itachangia asilimia 23.62 za mahitaji ya umeme na asilimia 49.79 itatokana na mitambo ya gesi asili na asilimia 25.59 itatokana na mitambo ya mafuta.
Katika kipindi hicho mitambo ya nguvu za maji itazalisha kwa wastani wa MW 151 ambapo kituo cha Mtera kitazalisha MW 22, Kidatu MW 54, Kihansi MW 60, Nyumba ya Mungu MW 3, Hale MW 3, New Pangani Falls MW 9 na Uwemba MW 0.2.

MADENI  MAKUBWA


Hali ya uzalishaji umeme ikiwa hivyo, habari za ndani ya Tanesco zinasema kuwa shirika hilo lihitaji kiasi cha Sh. bilioni 462 kutoka serikalini ili kukabiliana na mahitaji ya uzalishaji nishati kati ya Juni na Desemba mwaka huu.

Kupatikana kwa fedha hizo ni sawa na kusema kuwa ni jambo la kufa au kupona kwani vinginevyo taifa litaingia kwenye mgawo mkali wa umeme.

Bodi ya Tanesco imekwisha kuelezwa hali hiyo na hata Wizara ya Nishati na Madini ambayo inatarajiwa kuwasilisha makadirio ya matumizi yake bungeni wiki hii, nayo imepewa nakala ya ripoti ya hali ya fedha ya shirika na mwenendo wa maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme.

Wakati ripoti hiyo inaonyesha kuwa Tanesco itazalisha kiasi cha Sh. bilioni 566.771 kwa kipindi cha miezi sita ijayo, gharama pekee za kununua umeme kutoka kwa makampuni yanaozalisha nishati hiyo inakisiwa kuwa Sh. bilioni 587.156, kikiwa ni kiasi kikubwa kwa asilimia nne ya mapato yote ya Tanesco.

Tanesco hununua umeme kutoka IPTL, Songas, Symbon (Dar, Dodoma na Arusha) na Aggreko.

Taarifa hiyo kwa bodi pia ilisema kuwa Tanesco wanatarajia kupata mapato mengine ya Sh. bilioni 181.43 ikijumuisha ruzuku ya Sh. bilioni 80 ambazo serikali imekuwa ikitoa kufidia pengo la kutokupatikana nyongeza kubwa ya bei ya umeme kama ambavyo ilikuwa imeombwa kutika Mamlaka ya Usimamizi wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura). Mwaka jana Tanesco waliomba ongezeko la asilimia 150 ya bei ya umeme kwa wateja lakini EWURA ilipitisha asilimia 40.

Wakati serikali ikihemewa na Tanesco kwa kiwango hicho, suala la nyongeza ya bei ya umeme kwa watumiaji wake linazidi kuwa jambo lisiloepukika katika kipindi hiki kuelekea Desemba mwaka huu, ni lazima fedha hizo zipatikane haraka, vinginevyo mgawo ni suala ambalo limekwisha kuanza kimya kimya kwa sasa.

Bodi ya Tanesco pia imearifiwa juu ya ugumu unaoikabili Shirika katika kupatikana kwa mkopo kutoka muungano wa mabenki (consortium) wa Sh. bilioni 408.

“Mahitaji ya fedha ni zaidi ya Sh. bilioni 408 za mkopo wa mabenki. Kimsingi mkopo huo utaiwezesha Tanesco kupata Sh. bilioni 346.8 tu kwa sababu serikali itaudhamini kwa asilimia 85…” inasema sehemu ya taarifa ya Tanesco kwa bodi.

Hata hivyo, mkopo huo ingawa unatazamwa kama mkombozi kwa Tanesco, taarifa yake kwa bodi imeleeza machungu mengine kuwa kazi yake siyo kusaidia katika uzalishaji wa nishati tu, bali pia kulipa deni la Sh. bilioni 276.81, hivyo kiasi kitakachobaki ndicho kitaelekezwa kuzalisha umeme wa dharura.

Wakati mkopo wa mabenki hayo ukikabiliwa na changamoto ya kupitishwa na serikali, taarifa zaidi zinasema kuwa wapo wakopeshaji ambao wameonyesha nia ya kuikopesha serikali mkopo wa Dola za Marekani milioni 300 katika kipindi cha wiki nane mpaka 10 baada ya makubaliano kufikiwa ili kuikomboa Tanesco.

CHANZO: NIPASHE

3 comments:

Anonymous said...

Hii nchi yetu imekwenda na maji,Hatuna viongozi ambao wanafikiria,Hili tatizo la umeme limekuwa likigarimu nchi hela nyingi sana lakini cha ajabu hakuna ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la umeme.Viongozi wanatakiwa kutafuta suluhisho la kudumu nasio haya ya muda mfupi ambayo kwa mwananchi wakawaida kama mimi naona yanongeza ufisadi serikalini.

Anonymous said...

Tthis is stupid inawezekana vipi mgao ukawa mkali wa masaa 24 kwani. Hawakujua hilo toka mwanzo kama kuna matatizo ya umeme wakachukua hatua za haraka? Halafu kwa nini iwe inapokuwa ramdhani umeme ndio tatizo mbona xmas hakuna matatizo ya umeme wala sikukuu yaenyewe ya xmas umeme haukwatwi? Ni ubaguzi wa kidini tu hakuna lolote shenzi hawa wahusika wajiuzuru au shirika liuzwe kwa mtu binfsi sababu uendeshaji mbovu hela wanakula wakubwa tu wanazidi kuvimbiana matumbo kama wajawzito wasiojulikana watajifungua lini huku mzigo ukielemea wananchi imagine mgao masaa 24 vitu vinavyoharibika nani alipe? Then hawatangazi kama mgao umeanza wanakata umeme kienyeji kama mataahira flani mbona majumbani kwao umeme unawaka? Wajiuzuru tumechoka na hawa mbwa wanaojiita tanesco pamoja na wizara ya nishati wote ni mbwa na fisi maji wakubwa stupid idiots

Anonymous said...

sorry kwanini nchi iuzwe halafu kila mwananchi apewe chake.