SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Marekani na Umoja wa Ulaya, zimekubaliana kuchunguza kuwepo kwa meli za mafuta za Iran zinazofanya biashara kwa kutumia Bendera wa Tanzania. Meli hizo zikikutwa zikiwa na bendera hiyo, zinaweza kuifanya Tanzania kukumbana na vikwazo vya kiuchumi, vinavyotokana hatua ya Marekani na Umoja wa Ulaya, kuiwekea Iran vikwazo, kufuatia madai kuwa nchi hiyo ina mkakati wa kutengeneza silaha za nyuklia.
Hata hivyo Iran imesema mpango huo ni kwa matumizi ya nishati ya umeme. Hatua ya mataifa hayo kutaka kufanyika kwa uchunguzi, inafuatia taarifa za hivi karibuni juu ya kuwepo kwa meli hizo 10 za mafuta zinazoaminiwa kuwa zinamilikiwa na Kampuni ya NITC ya nchini Irani, zikifanya biashara kwa kutumia bendera ya Tanzania.
Hata hivyo Serikai ya Mapinduzi ya Zanzibar, imetoa ufafanuzi kuhusu taarifa hizo na kwamba meli hizo si za Iran. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alisema wameamua kushirikiana ili kujua ukweli wa suala hilo.
“Tayari SMZ imezungumzia suala la meli hizo. Imesema zilizosajiliwa ni 399, kumi na moja ni za mafuta, lakini walipofuatilia ziliposajiliwa (Dubai) walielezwa kuwa si za Iran,” alisema Membe. Alisema taarifa za kuwepo kwa meli hizo si za kupuuzwa ndio maana wameamua kwa pamoja kufanya uchunguzi, ili kujua ukweli. “Tunafanya utafiti na ukweli utajulikana ambao unaweza kukanusha au kuthibitisha jambo hili,” alisema Membe. Alisema sababu za kuchunguza jambo hilo ni baada ya wakala aliyezisajili meli hizo kukanusha kuwa si za Iran.
Hali kadhalika hatua ya Balozi wa Iran nchini naye kukataa kuwepo kwa jambo hilo. Membe alisema kama meli hizo zitagundulika kuwa ni za Iran, zitafutwa na hazitaruhusiiwa kutumia bendera ya Tanzania. “Tunayafanya haya sio kwa sababu yameibuliwa na Mjumbe wa Baraza la Congress, Howard Berman bali ni kubanwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo sisi ni wanachama,” alisema Membe.
Hata hivyo Membe alitaka suala hilo lisitumike kuwagawa wananchi na kuvunja Muungano.
“Tutaujua ukweli na kila kitu kitakwisha, tudumishe Muungano wetu na tusikubali jambo hili litetemeshe Muungano huu,”alisema. Wiki moja iliyopita, Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano wa Zanzibar, Hamad Masoud Hamad alikiri kuwapo kwa meli hizo Zanzibar na kwamba zilisajiliwa kisheria Zanzibar chini ya Sheria ya usafiri wa Bahari Zanzibar ya mwaka 2006.
Hata hivyo alikana kuwa zinamilikiwa au kuwa na uhusiano wowote na Iran. Akiwasilisha majibu ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika Baraza la Wawakilishi, kuhusu sakata hilo, Hamad alisema baada ya taarifa hizo, SMZ ilifanya mawasiliano na Kampuni ya Philitex ya Dubai iliyopewa zabuni ya kufanya usajili wa wazi wa meli za kimataifa, kutaka kujua wamiliki wa meli zilizotajwa.
Alisema kampuni hiyo ilitoa majibu kuwa wamiliki wa kampuni hizo walikana kuwa na uhusiano na Serikali ya Iran. Taarifa za kuwepo kwa meli 10 za mafuta zinazoaminiwa kumilikiwa na Kampuni ya Iran ya NITC, zikifanya biashara kwa kutumia bendera ya Tanzania, ziliibuliwa na gazeti dada la The Citizen. Taarifa zilizotolewa Ijumaa iliyopita na Shirika la Habari la Uingereza (Reuters), zilisema sakata hilo, huenda likaiweka pabaya Tanzania kwa kukosa misaada kutoka Marekani ikiwa ni pamoja na kuwekewa vikwazo na nchi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Reuters, onyo hilo lilitolewa na Mjumbe wa Baraza la Congress, Howard Berman ambaye alisema tayari Marekani imeshamwandikia Rais Jakaya Kikwete, kuhusu suala hilo. Berman ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje alisema kitendo hicho kwa kiasi kikubwa kinaweza kuzorotesha uhusiano wa Tanzania na Marekani. Alisema barua iliyotumwa kwa Rais Kikwete pia imesema kuwa kama meli hizo za mafuta zitaendelea kufanya kazi zikiwa na bendera za Tanzania, Utawala wa Rais Obama utalazimika kuiwekea vikwazo Tanzania.
Katika maelezo yake Waziri Hamad alitoa orodha ya meli za kimataifa zilizosajiliwa ndani ya wiki mbili zilizopita huo Zanzibar.
Meli hizo ni Daisy, Justice, Magnolia, Lantana, Leadership, Companion, Camellia, Clove, Courage, Freedom na Valor ambazo zote zinamilikuwa na kampuni kutoka Malta na Cyprus.
Chadema yaichimba Serikali kuhusu Taarifa za Iran kutumia Bendera ya Tanzania
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeibebesha lawama Serikali kikidai ina kigugumizi kuhusu madai ya meli ya mafuta ya Iran kutumia bendera ya Tanzania ili kukwepa vikwazo vya kiuchumi vya kimataifa.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Hamad Mussa Yussuf alisema kupitia taarifa kwa gazeti hili kwamba haoni sababu ya Serikali kujikanyaga katika jambo hilo.
“Tunashangaa kwa takribani muda wa juma moja sasa zimekuwapo taarifa katika vyombo vya habari kuhusu kampuni moja ya meli inayodaiwa kutoka Iran, inayojulikana kwa jina la NITC (National Iranian Tanker Company), inatumia Bendera ya Tanzania, isivyo kihalali,” alisema Yussuf.
Alielezea kwamba kitendo hicho ni kinyume kabisa na sheria za nchi na zile za kimataifa na kwamba ni jambo nyeti ambalo halipaswi kufanywa kama la mchezo lakini anashangaa Serikali inajikanyaga kutoa taarifa sahihi.
“Pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kukanusha taarifa hizo, Chadema kinaitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa taarifa kwa umma juu ya hatua ilizochukua kuchunguza madai hayo,” alisema.
Chadema imetoa shutuma hizo wakati Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe akisema kitendo hicho ni kosa kisheria, lakini akasema taarifa hiyo ni ngeni ila vyombo husika vitalichunguza.
Yussuf alisema kuwa ili Tanzania ijisafishe Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilipaswa kushirikiana na Serikali ya Muungano kufanya uchunguzi wa haraka na kubaini msingi wa tuhuma hizo na kuchukua hatua.
Yussuf aliilaumu maofisa wa Serikali ya Zanzibar akisema siyo mara yao ya kwanza kufanya vitendo vya kizembe na kutoa mfano wa kashfa ya kuzama kwa meli ya Spice Islender.
Hofu ya Chadema alisema ni kwamba ina hofia “Tanzania itaonekana inaibeba na kuisaidia Iran kukwepa vikwazo ambavyo nchi hiyo inatishiwa na mataifa ya Magharibi, hasa Marekani na Umoja wa Ulaya.”
Yussuf alisema mataifa hayo makubwa hutumia mabavu na vitisho kuzichagulia baadhi ya nchi nyingine duniani, nini cha kufanya na rasilimali zake mathalani mzozo unaoendelea na Iran kuhusu urutubishaji wa madini ya urani.
“Si nia ya Chadema kuingia katika mgogoro wa Iran na Mataifa ya Magharibi hapa kupitia mjadala wa madai hayo yaliyoandikwa kwenye vyombo vya habari; lakini inatoa tamko kufuatia ukimya na kigugumizi cha Serikali,” alisema.
Chanzo cha sakata hili kinadaiwa kinatokana na Mbunge mmoja wa Marekani ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Nje, Howard Berman kuandika barua kwa Rais Jakaya Kikwete akimuarifu juu ya suala hilo la Meli za NIT kutuhumiwa kupeperusha Bendera za Tanzania.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment