ANGALIA LIVE NEWS
Monday, July 2, 2012
Wabunge: Baraza la Mawaziri ni mzigo
Neville Meena na Habel Chidawali, Dodoma
KAMATI ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, imesema Baraza la Mawaziri lililoundwa na Rais Jakaya Kikwete ni kubwa linalohitaji kupunguzwa ili kupunguza gharama za uendeshaji wa Serikali.Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Paul Lwanji alisema jana Bungeni kuwa Baraza hilo linapaswa kupunguzwa kwa kuunganisha baadhi ya wizara na idara zinazoshabihiana bila kuathiri utendaji wa shughuli za Serikali.
Akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Rais kwa mwaka wa fedha uliopita na maoni kuhusu makadirio ya matumizi ya mwaka 2012/2013, Lwanji alisema idadi ya mawaziri, manaibu waziri, makatibu wakuu na manaibu wao ni mzigo mkubwa kwa walipa kodi.
Alisema umefika wakati kwa Serikali kukubaliana na ushauri wa wadau mbalimbali na kupunguza Baraza la Mawaziri pamoja na idara zisizo na umuhimu ili kuendana na pato la Taifa.
“Idadi ya mawaziri 30, manaibu waziri 25, makatibu wakuu 26, Naibu Katibu wakuu 26 ni mzigo mkubwa kwa nchi inayoendelea kama yetu. Kamati inashauri kwamba Serikali iangalie uwezekano kupunguzwa kwa kuunganisha baadhi ya Wizara na idara zinazoshabihiana bila kuathiri utendaji wa Serikali,” alisema Lwanji ambaye pia ni Mbunge wa Manyoni Mashariki.
Kamati hiyo ilipendekeza mabadiliko ya mfumo wa kuwateua watumishi wa ngazi za juu serikalini kutokana na wengi kuonekana kutokidhi vigezo vya uongozi.
Alisema umefika wakati wa kuwekwa utaratibu na uwezo wa mtu kumudu majukumu yake na uwezo wa kiakili (IQ), sifa na uzoefu.
Alisema katika utaratibu huo, kama mamlaka ikikosea na kumteua mtu kushika madaraka asiyostahili au ukomo wa kufikiri ukiwa umefika mwisho, ni wazi kuwa atashindwa kumudu nafasi yake na kuisababishia Serikali hasara.
Lwanji alisema Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imekuwa ikishindwa kuwachukuliwa hatua viongozi wanaoshindwa kutimiza wajibu wao.
Alitoa mfano wa madiwani 1,844 ambao mwaka jana hawakuchukuliwa hatua zozote licha ya kushindwa kutekeleza sheria ya sekretarieti, hivyo utekelezaji wa sheria hiyo kuachwa kwa madiwani 1,032 tu.
Aliliambia Bunge kuwa katika kipindi chote cha mwaka 2011, Sekretarieti hiyo ilishughulikia mashauri 23 tu ya viongozi wote walioshindwa kutekeleza Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Kamati hiyo iliitaka Serikali kutoa tamko kwa Watanzania ni lini itawafikisha mahakamani wahusika wote waliotajwa katika ripoti ya CAG kuwa walihusika kwa namna moja au nyingine katika kuihujumu nchi.
Kamati hiyo ilionyesha shaka katika madai ya wafanyakazi 8,134 ambayo thamani ya madai yao yalifikia jumla ya Sh8.3 bilioni ambayo yanaendelea kuhakikiwa na kuhoji fedha hizo zitatoka wapi kwani hazipo katika mafungu ya bajeti.
Mishahara juu
Katika hatua nyingine, Serikali imetangaza kupandisha viwango vya mishahara ya watumishi wa umma kuanzia Julai Mosi, mwaka huu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Manejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani alisema jana kuwa Serikali itarekebisha mishahara ya watumishi wake kwa kuzingatia uwezo wa bajeti na makubaliano yaliyofikiwa na Baraza la Majadiliano ya Pamoja Katika Utumishi wa Umma.
Hata hivyo Kombani hakuweka wazi kiwango cha nyongeza za mishahara hiyo na badala yake alitaja fedha zilizotengwa kwa ajili ya malipo ya mishahara na kulipa madeni ambazo ni Sh3.781 trilioni.
Alisema fedha hizo zitagharamia mishahara, upandishwaji vyeo na kulipia madai ya malimbikizo na mapunjo ya mishahara kwa watumishi wa Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Wakala na taasisi za Serikali na kwamba: “ Wenye madai mbalimbali watalipwa madai yao.”
Kombani alisema kiasi hicho cha fedha kimeongezeka kwa Sh510.807 bilioni ambacho ni sawa na asilimia 15.6 ya kiasi kilichokuwa kimepangwa kutumika mwaka wa fedha 2011/2012.
“Serikali itafanya utafiti kuhusu mishahara na maslahi ya wafanyakazi baina ya sekta binafsi na Serikali kwa lengo la kuwianisha na kuoanisha mishahara ya watumishi wa umma,” alisema.
Alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012/13, Serikali inatarajia kuajiri watumishi wapya 56,678 na kipaumbele kimewekwa katika sekta za elimu, afya, kilimo na baadhi ya vyombo vya dola.
Mbali na ajira hizo, Serikali itawapandisha vyeo watumishi 42,419 ikiwa ni hatua ya kufanya maboresho katika utendaji kazi wake.
Akizungumzia ujenzi wa kituo cha kuwaenzi waasisi wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, alisema katika kipindi hiki cha fedha, msingi wa jengo hilo utaanza.
Wapinzani wang’aka
Kwa upande wake, Msemaji wa Kambi ya Upinzani kuhusu Ofisi ya Rais na taasisi zilizo chini yake, Profesa Kulikoyela Kahigi alizungumzia tuhuma za rushwa zilizolitikisa Bunge.
“Zimetolewa tuhuma kadhaa na vyombo vya habari pamoja na waheshimiwa wenyewe kutuhumiana na wengine kukamatwa kwa tuhuma za rushwa. Ni dhahiri hata katika mchakato wa kuchagua wabunge la Afrika ya Mashariki kauli za vitendo vya rushwa zilitolewa na waheshimiwa wabunge,” alisema Profesa Kahigi na kuongeza:
“Kambi ya Upinzani inaitaka Takukuru kuhakikisha kuwa pamoja na kuwakamata watuhumiwa wengine, iendelee kuchukua hatua kulisafisha jina la Bunge katika kashfa hii nzito inayoliondolea heshima mbele ya jamii.”
Alisema kutokana na rushwa kuathiri maendeleo ya nchi, ni wakati mwafaka kwa Takukuru kuwa chombo huru kiutendaji ... “Tunapendekeza uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hii ufanywe na Kamati ya Taifa ya Uteuzi na athibitishwe na Bunge, pia taarifa za taasisi hii ziwe zinawasilishwa bungeni kila mwaka na kujadiliwa na Bunge kama ilivyo sasa katika kujadili taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.”
Mwananchi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment