ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, July 24, 2012

‘Wananchi ndio wataamua ya Kigamboni’

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka


Wakati serikali ikiwa imekwishatenga  Sh. trilioni 11.6 kwa ajili ya ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni jijini Dar es salaam, Diwani wa Kata ya Vijiweni, Suleiman Mathew, amesema utekelezaji wa mradi huo utategemea maamuzi yatakayotolewa na  wananchi.

Diwani huyo alitoa ufafanuzi huo juzi (Jumapili) wakati wa akingumza na wananchi wa kata hiyo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya shimo la mchanga kwamfaayeka.

Mathew alisema wananchi wa kata hiyo wasiwe na wasiwasi kwani utekelezaji wa ujenzi utategemea wananchi na kuna kamati ilishaundwa na inaendelea kufanya kazi.

“Jamani sasa mimi kwenda bungeni na kurudi lisiwe tatizo hapana, Dodoma nitaendelea kwenda kadri inavyowezekana na Mtanzania yeyote ana uhuru wa kwenda kuhudhuria vikao vya Bunge, matatizo madogo yaliyopita kati yangu mimi na mbunge tutayamaliza,” alisema Mathew.

Alisema hakuna sababu kwa suala la ujenzi wa mji mpya wa kigamboni kuwa ajenda ya kisiasa na kwamba wanaotaka kujipatia umaarufu kupitia suala hilo wangoje 2015.



Mathew alisema yeye na madiwani wenzake wataendelea kushirikiana na Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndugulile na kwamba hata juzi amewaaga wakati anakwenda Ulaya kikazi.

Katika mkutano huo diwani huyo alikabidhi vifaa mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya Sh. Milioni tatu, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi alizotoa mwaka 2010.

Vifaa alivyokabidhi ni pamoja na kompyuta nne, tenki la maji la lita 4000, turubai na nyenzo za kilimo.

Akiwasilisha bajeti ya 2012/2013, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka, alisema wizara yake imetenga Sh. trioni 11.6 ambazo zitakuwa zinatolewa kwa awamu.

Wakati wa kikao hicho cha bunge, Mbunge wa Kigamboni (CCM), Dk. Ndugulile, alisema mradi wa ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni ni batili kwani umekiuka sheria na kwamba, kinachofanywa na serikali ni kung’ang’ania udalali kwa kutaka kuchukua ardhi ya wananchi maskini na kuiuza kwa bei kubwa kwa matajiri, kinyume cha ahadi yake ya maisha bora kwa kila Mtanzania.
CHANZO: NIPASHE

No comments: