Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano wa Zanzibar, Hamad Masoud Hamad amejiuzulu wadhifa wake leo jioni imeelezwa. Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee ilisema tayari Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk. Ali Mohammed Shein amekubali ombi la Waziri Hamad Masoud kujiuzulu.
“Tarehe 20 Julai,2012 Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Mheshimiwa Hamad Masoud Hamad alimuandikia barua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk Ali Mohammed Shein ya kumuomba ajiuzulu kufuatia ajali ya kuzama kwa meli ya Mv. Skagit iliyotokea Julai 18,2012” Ilisema taarifa ya Dk. Mzee. Kufuatia kujiuzulu kwa waziri huyo, Rais Dk Shein amemteua Mwakilishi wa Jimbo la Ziwani(CUF) Rashid Seif Suleiman kuwa Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano.
“Kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano,Rais amemteua Rashid Seif Suleiman kuwa Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano” Taarifa ya Ikulu ilisema.
Uteuzi wa Waziri mpya wa Miundombinu na Mawasiliano umeanza Julai 23 mwaka huu na habari zilizo ufikia mtando huu ni kwamba nafasi yake imerithiwa na Mhe. Rashid Seif Suleiman (Ziwani, CUF).
Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk. Ali Mohammed Shein ameunda Tume ya kuchunguza ajali ya kuzama kwa meli ya Mv. Skagit.
Mwenyekiti wa Tume hiyo ni Jaji Abdulhakim Ameir Issa, wajumbe ni Meja Jenerali S.S. Omar, COMDR. Hassan Mussa Mzee, Kapteni Abdulla Yussuf Jumbe, Kaptein Abdulla Juma Abdulla, Salum Taoufiq, Kaptein Hatibu Katandula, Bi. Mkali Fauster Ngowo, Ali Omar Chengo na Shaaban Ramadhan Abdalla Katibu wa Tume.

1 comment:
Siyo kwamba kajiuzuru, kafukuzwa kazi kwa kulazimiswa kujiuzuru. Alipewa nafasi ya kujiuzuru kwa hiari, alikataa kwa kisingizio kuwa asingeweza kuzuia upepo na hivyo hana makosa. Sasa iweje leo agundua makosa yake na kuamua kujiuzuru? Huu ni mfano mzuri maana atakayepewa nafasi hiyo atakuwa halali usungizi. Huu ndiyo uwajibikaji ambao usiishie tu kwe meli, bali hata milipuko ya mabomu ili wananchi wawe na imani na serikali yao, siyo kusubiri mpaka CHADEMA waandamane.
Post a Comment