BASHE AMTUHUMU KIGWANGALLAH KUMTISHA KWA SILAHA,NAYE AENDA POLISI KUWATUHUMU WAFUASI WA BASHE KUMTISHA
Waandishi Wetu
VITA ya mahasimu wa siku nyingi katika siasa wilayani Nzega, Hussein Bashe na Dk Hamis Kigwangallah imechukua sura mpya, baada ya makada hao wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufikia hatua ya kutishiana kwa bastola hadharani.Hata hivyo, pamoja na taarifa hizo kuthibitishwa na viongozi wa CCM wilayani humo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Bashe na Kigwangallah kwa nyakati tofauti kila mmoja amekanusha madai hayo akimtuhumu mwenzake kuwa ndiye aliyekuwa na silaha.
Wakati Bashe akisema Dk Kigwangallah ambaye pia ni mbunge wa Nzega ndiye aliyetoa bastola kumstishia wakiwa ndani ya ofisi ya ya CCM Wilaya, Dk Kigwangallah anaeleza kuwa walinzi wa Bashe ndio waliomtishia yeye bastola na kwamba tayari amelifikisha suala hilo polisi ambao wanalifanyia kazi.
Habari zilizolifikia gazeti hili zilieleza kuwa, Dk Kigwangallah na Bashe walizua tafrani hiyo juzi wakati wakirejesha fomu za kuwania nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) kupitia Wilaya ya Nzega.
Upinzani baina ya wanasiasa hao vijana, ulianza 2010 baada ya Kigwangallah kupitishwa na CCM kugombea ubunge katika jimbo hilo licha ya kushika nafasi ya tatu katika kura za maoni, ndani ya chama hicho.
Bashe ambaye aliibuka kidedea katika mchakato huo wa kura za maoni alitoswa na chama hicho kwa maelezo kuwa hakuwa raia wa Tanzania, huku aliyeshika nafasi ya pili, Lucas Selelii ambaye alikuwa kinara wa kupambana na mafisadi wa chama hicho naye akitoswa. Baadaye Waziri wa Mambo ya Ndani wa wakati huo, Lawrence Masha alisema Bashe alikuwa raia halali wa Tanzania.
Vita hiyo ilionekana kuendelea juzi baada ya kudaiwa kutishiana bastola huku kila mmoja akitoa maelezo ya kumrushia lawama mwenzake.
Ilivyokuwa
Katibu wa CCM Wilaya ya Nzega, Kajoro Vyehoroka alisema Bashe alifika ofisini hapo kurejesha fomu saa 09:50 alasiri, muda mfupi baada ya Dk Kigwangallah ambaye alifika saa 09:48.
“Kigwangala alifika na kuingia ofisi ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Fransis Shija, ambako alikaa na kujaza fomu yake. Bashe naye alifika akaingia ofisini kwangu, akakaa na kuandika," alisema.
Katibu huyo aliendelea kueleza kuwa ilipofika saa 9:55, Dk Kigwangallah alikwenda kwa katibu muhutasi kurejesha fomu yake na kukaa hapo.
"Bashe alipofika hapo naye alisimama akingoja Kigwangallah amalize, lakini Kigwangallah alimueleza kuwa muda wa kurejesha fomu umemalizika, hivyo kumzuia kurudisha fomu, hali iliyozua mvutano na vurugu" alieleza katibu huyo.
Katibu wa Vijana wa CCM Wilayani Nzega, Salome Nyombi, alisema baada ya vurugu hizo kuzuiliwa ndani ya ofisi ya katibu, Bashe alitolewa nje ambako alianza kuwasimulia rafiki zake kilichotokea ndani.
Alisema baadaye Kigwangallah naye alifa eneo hilo na kuanza kurusha maneno, hali iliyozua mtafaruku mwingine katika eneo hilo.
"Alipozuiliwa kufanya vurugu, aliendelea kutukana na kisha kutoa bastola akiwatishia watu waliokuwa wakizungumza na Bashe kwa madai kuwa ni vibaraka wake," alisema na kuongeza:
“Hali ilikuwa mbaya kiasi cha baadhi yetu kulazimika kukimbia, na wengine tulilala kwenye viti, lakini kijana mmoja anayeitwa Sango, alimzuia (Kigwangallah) kwa kujaribu kumpiga kwa kiti, ndipo watu walipomtoa Bashe na kumpeleka eneo lingine.”
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wilayani Nzega, Mary Igogo, alisema amesikitishwa na vurugu hizo na kusema iwapo wasingemzuia Bashe, kungezuka ugomvi mkubwa.
Katibu CCM mkoa
Katibu CCM Mkoa wa Tabora, Iddi Ame akizungumuza kwa simu, alisema ndani ya CCM ni ajabu kwa wanachama kutishina kwa silaha.
Ame alisema kuwa kitendo hicho ni aibu kubwa kwa CCM huku akiuagiza uongozi wa Wilaya ya Nzega kutoa maamuzi mapema juu ya vurugu za makada hao.
“CCM hatuna historia ya kutishana kwa bastola na kamwe jambo hilo haliwezi kuwa siasa kwa kuwa linaleta sura mbaya ndani ya chama chetu, nawaagiza uongozi wa wilaya watoe tamko au maamuzi ya jambo hili mapema,”Ame.
Shuhuda
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye jina lake halikufahamika mara moja, alisema vurugu zilikuwa kubwa zaidi nje ya ofisi za CCM baada ya mahasimu hao kutolewa ndani ya ofisi hizo baada ya kuanza kulumbana.
Taarifa kutoka Jeshi la Polisi zilieleza kuwa Kigwangallah alifika katika kituo cha polisi na kufungua malalamiko ya kutishiwa maisha na Sango Issaya, Hussein Bashe pamoja na Majaliwa Bilali.
Taarifa hizo zilifafanua kwamba kwa nyakati tofauti mahasimu hao walitoa maelezo yao polisi na wapo nje kwa dhamana mpaka pale upelelezi wa tuhuma walizopeana utakapokamilika.
"Tumepokea taarifa za hawa watu na tunaendelea na upelelezi wetu mpaka hapo tutakapojiridhisha na ushahidi ndipo tutawapeleka mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili,”alisema ofisa mmoja wa polisi wa ngazi za juu wilaya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Antony Rutta, aliliambia gazeti hili kuwa taarifa za tukio hilo alizipata, lakini anaendelea kuzifuatilia kujua chanzo chake.
“Ni kweli nimepata taarifa za Bashe na Kigwangallah wamedaiwa kutishiana bastola…mimi nilisikia hayo nikiwa njiani kutoka huko Nzega kurudi Tabora….nitafuatilia,”alisema.
Kauli za Bashe, Kigwangallah
Bashe alikiri kutokea vurugu hizo, lakini akakanusha kumtishia bastola Dk Kigwangallah akidai kuwa mwenzake huyo ndiye aliyemtishia yeye kwa bastola akitaka fomu yake isipokelewe kwa kile alichoeleza kuwa imechelewa kurejeshwa.
“Huyu ndugu yangu ana visa na chuki dhidi yangu, ni kweli alinichomolea bastola, lakini wanachama walituamulia," alisema
Hata hivyo, Bashe alieleza kuwa pamoja na hila hizo, Dk Kigwangallah hamuwezi kisiasa kwani katika chaguzi zote zilizowahi kufanyika zikiwahusisha wao, amekuwa akimshinda kwa kishindo.
"Kigwangallah pia aliwahi kuvamia mkutano wangu, lakini niliwaambia watu wangu wamwache. Anachotafuta ni confrontation (msuguano) na mimi ili kutokee tatizo nienguliwe kwenye uchaguzi baada ya kuona haniwezi," alisema.
Bashe alisema kwamba amegundua Kigwangallah anatumia mbinu ili majina yao yakatwe yote kwa kuwa ameshaona hawezi kumshinda. “Jamani Kigwangallah hawezi kunishinda, amenitishia na bastola nikakaa kimya, sikupenda kabisa kumjibu maana najua anachotafuta,” alisema
Kwa upande wake, Dk Kigwangallah alisema aliomba Bashe azuiwe kurejesha fomu yake kwa kuwa aliirudisha nje ya muda, lakini alishangaa kuona anafanyiwa vurugu na wafuasi wake.
Alisema alitishiwa maisha na watu watatu ambao aliwataja akiwamo Bashe na kueleza kuwa tayari malalamiko hayo ameyafikisha polisi.
"Walinzi wa Bashe ndio walionitishia bastola na baada ya tukio hilo nikaenda kuripoti polisi na tayari polisi wamechukua hatua ikiwamo kuwafikisha mahakamani Bashe na wapambe wake hao," alisema Dk Kigwangallah na kuongeza;
“Huyu ndugu yangu (Bashe) ni mzushi anataka kuyakuza mambo tu. Katika hilo Katibu amembeba kwani muda wa kurejesha fomu ulikuwa umeisha".
Alisema Bashe amekuwa akijaribu kumfanyia faulo ya kumtishia huku akitembea na jopo la waandishi wa habari ili wamchafue.
’’Nimeamua kuja kutoa taarifa kwani nimetishiwa maisha yangu na kijana huyu pamoja na Bashe lazima nitoe taarifa hizi, maana nimeonewa,’’alisema Kigwangallah.
Alipoulizwa kana anamiliki bastola, Kigwangallah alisema kuwa kwa muda mrefu amekuwa akimiliki silaha hiyo.
“Kama ningeamua kuua ningeweza kufanya hivyo ila naelewa maana ya kuwa na silaha ya moto, ndio maana nimekuja hapa kutoa taarifa kwa sababu lolote linaweza kutokea” alisema mbunge huyo wakati akiwa Kituo cha Polisi Nzega.
Zungu amkacha Mkono
Katika hatua nyingine mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu ameshindwa kurudisha fomu ya kuwania nafasi ya uenyekiti wa Wazazi Taifa.
Siku ya mwisho ya kurejesha fomu ilikuwa juzi, lakini mbunge huyo ambaye pia ni mwenyekiti wa Bunge alishindwa kuirejesha kama walivyofanya wagombea wengine 16 akiwemo Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment