ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, August 9, 2012

KWA NINI UTUMIE UDHAIFU WA MWENZA WAKO KUMTESA?

NDUGU zangu, kwanza nichukue fursa hii kumshukuru Mungu ambaye amenijaalia afya njema na kuniwezesha kuungana nanyi tena kupitia safu hii ambayo tunazungumzia mada mbalimbali zinazogusa maisha yetu ya kimapenzi.
Leo nataka kuzungumzia tabia ya baadhi ya watu kutumia udhaifu wa wenzao kuwatesa na kufikia hatua ya kuwakosesha amani. Kila binadamu ana udhaifu wake, hivyo ndivyo tulivyoumbwa! Akitokea wa kusema yeye amekamilika kila idara ni wazi atakuwa anamkufuru Mungu.
Unaweza kujiaminisha kuwa huna udhaifu wowote lakini kumbe watu wanaokuzunguka au mpenzi wao unayeishi naye amebaini udhaifu fulani kwako lakini anakuvumilia tu.
Hata hivyo, udhaifu ambao nitauzungumzia leo ni ule unaoyagusa maisha yetu ya kimapenzi ambao baadhi wanautumia kuwatesa wenza wao. Kwa nini nataka kulizungumzia hilo? Hebu msikilize kwanza huyu dada Husna wa Tanga ambaye nilizungumza naye wiki iliyopita kuhusu maisha yake ya kimapenzi:
“Mimi ni mgeni kwenye mapenzi na hii imetokana na maisha ambayo nimekuwa nikiishi na wazazi wangu. Nilikuwa nabanwa sana kiasi kwamba mambo ya mapenzi sikuwa nikipata nafasi ya kujifunza kwa namna moja au nyingine.
“Baba yangu alipofariki nikiwa na umri wa miaka 18 ndipo nilipoanza kujiingiza huko lakini sasa nikawa sijui chochote. Bahati mbaya sana nilitokea kumpenda mwanaume ambaye anaonekana ni mzoefu, basi kila tulipokuwa tunakutana faragha nikawa kama mzigo kwake, nilitarajia atanielekeza nifanyeje ili tufurahishane lakini cha ajabu hatukuchukua muda akaniacha.
“Kuanzia hapo nimekuwa ni mtu wa kuachwa kwa udhaifu huo wa kutojua majamboz. Nakiri mimi si lolote faragha lakini nahitaji kupewa nafasi ya kujifunza sasa kitendo cha kuteswa na wanaume kwa udhaifu wangu huo kinaniuma sana.”
Kwa kifupi dada huyu ni mgeni kwenye ulingo wa mapenzi na anakiri kuwa huo ndiyo udhaifu wake. Sasa inakuwaje mtu mwenye udhaifu kama huu kuteswa na wanaume kiasi cha kukoseshwa raha? Ina maana mtu ambaye hajui lolote kuhusu mapenzi hastahili kupendwa na kuelekezwa?
Achilia mbali hilo, kuna udhaifu wa kimaumbile ambao unatofautiana kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine. Kwa mfano, unaweza kuwa na mpenzi ambaye maumbile yake ni makubwa kiasi kwamba ukiwa naye faragha husikii ile furaha uliyotarajia.
Hilo lipo kwa wanaume na wanawake. Sasa, hebu jiulize, kuna mtu ambaye anamuomba Mungu ampe maumbile ya saizi flani? Kwa kifupi hakuna na ndiyo maana nasema ukiwa na mpenzi ambaye maumbile yake ya kiume ni madogo, hutakiwi kumfanyia visa eti kwa kuwa hakuridhishi.
Huo ni udhaifu wake kwa hiyo unatakiwa kukaa naye na kujadiliana kuona ni kwa jinsi gani mnaweza kuendelea kuwa pamoja kwa amani na furaha licha ya kuwepo kwa kasoro hiyo.
Kwa wanawake nako hivyo hivyo. Unaweza kuwa umeingia kwenye uhusiano na mwanamke ambaye maumbile yake ni makubwa. Jamani, udhaifu kama huo mbona unavumilika? Kama kweli uliyenaye unampenda kwa dhati basi kubaliana na udhaifu huo alionao.
Isifikie hatua eti kwa kuwa mpenzi wako huyo ‘akikimbia raundi moja tu hoi’ basi umuache au umsaliti. Kumbuka pia ukiwa naye ambaye bila ‘kukimbia raundi kumi’ hajaridhika itakuwa ni tatizo kwako. Kwa hiyo udhaifu wowote ambao utaubaini kwa mpenzi wako chukulia kama changamoto.
Ninachotaka kusisitiza leo ni kwamba kwenye mapenzi kuvumiliana ni jambo la msingi sana. Huwezi kumpata mpenzi ambaye amekamilika. Wewe unayesoma makala haya utakubaliana na mimi kwamba hata huyo uliye naye kuna baadhi ya vigezo ambavyo ulitaka awe navyo lakini hana ila unaendelea kuwa naye kwa kuwa umempenda.
Huo ndiyo upendo wa kweli. Utakuwa ni mnafiki na mzandiki endapo utajifanya unampenda huyo uliyenaye lakini kumbe kutokana na udhaifu wake unamsaliti. Hii ni mbaya sana na kama unafanya hivyo ujue unakosea.
Lakini pia katika hili hili la udhaifu, tujaribu kufichiana siri zetu. Si jambo jema kutangaza udhaifu alionao mpenzi wako kwa marafiki zake. Ni sawa waweza kuwa unafanya hivyo katika kutafuta ushauri lakini kumbuka kuna ambayo ukishayaona kwa mpenzi wako yanatakiwa kubaki siri na hustahili kuyaombea ushauri.
Si vizuri kuyaombea ushauri kwa kuwa kufanya hivyo ni kusambaza siri zinazoweza kumfanya ‘mtu’ wako akadharaulika. Wapenzi wa kweli ni wale wanaovumiliana kwa hali na mali hivyo uvumilivu wako iwe ni pamoja na kuukubali udhaifu alionao mwenzako.
Ni hayo tu kwa leo, tukutane tena wiki ijayo.

www.globalpublishers.info

1 comment:

Anonymous said...

Somo la leo limemefika mwake, kuna baadhi ya watu wanakuwa na aibu na wapenzi wao, sasa kama unaweza kumvulia nguo mpenzi wako aibu ya nini? Kuridhishana ndio mapenzi, kuongea ni vipi ufanyiwe ili ulifurahie tendo la ndoa ni haki yako. Kuna watu wanakuwa mabubu wanapenda wafanyiwe kitu fulani lakini hawasemi sasa mwenzio ataota? Matekeo yake utabadilisha wanawake/wanaume usipate hicho unachokitaka. Hakuna chuo mapenzi chuo ni nyie wenyewe kuongea mfanyiane nini. Mpenzi wako ni rafiki yako. Nimeshuhudia ndoa nyingi zinavunjika kwa ajili, ukiuliza.... mie mume wangu hanifanyii hivi/vile. Sasa je ulimwambia akufanyiee? Jibu hapana. Jaribu kuongea utafurahia tendo la ndoa na mpenzi wako...

Mdau wa maswala ya mapenzi