ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, August 7, 2012

Mbaroni kwa tuhuma za kuuza umeme wa Tanesco

Kamanda Suleiman Kova
(Kamanda wa Polisi Kanda
Maalum ya Dar es Salaam)



Hujumu katika Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) zinazidi kuibuliwa, baada ya jana kukamatwa kwa mwananchi mmoja mkazi wa jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kuiba umeme na kuwauzia wananchi wengine.

Mkazi huyo inadaiwa kuwa kwa muda mrefu amekuwa akiiibia Tanesco umeme kwa njia ya mtandao na kuuuza kwa bei ‘chee’ kwa wateja aliowasajili mwenyewe bila ya mapato yatokanayo na biashara yake kuingia ndani ya shirika hilo.

Mwananchi huyo aliyefahamika kwa jina la Ibrahimu Saidi, alikamatwa na maofisa wa Tanesco waliokuwa wameambatana na maofisa wa Polisi toka katika Kituo cha Oysterbay, akiwa ndani ya ofisi yake iliyoko kwenye nyumba namba 648, inayomilikiwa na Bakari Issah, huko Mwananyamala ‘A’ jijini Dar es Salaam



Vifaa vilivyokutwa ndani ya ofisi hiyo ambavyo amekuwa akivitumia katika biashara yake ya kuuza umeme wa ‘wizi’ toka Tanesco ni pamoja na kamba zinazotumiwa na mafundi wa kupanda kwenye nguzo, sili, mita, mavazi ya kazi yanayotumiwa na wafanyakazi wa Tanesco pamoja na mafaili ya kutunza kubukumbu za wateja yaliyokuwa na nembo za shirika hilo.

Akizungumza mara baada ya kukamatwa kwa Saidi, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma cha shirika hilo, Badru Masoud, alisema kuwa vifaa vyote vilivyokutwa katika ofisi ya mtuhumiwa ni mali ya Tanesco.

“Ndugu waandishi wa habari, vifaa vyote mnavyoviona hapa ambavyo vimekutwa katika ofisi hii ni mali ya shirika na haviruhusiwi kumilikiwa na mtu binafsi kama ilivyotokea kwa wenzetu hawa,” alisema.

Awali akizungumza na waandishi wa habari kabla ya zoezi la kwenda kumkamata mtuhumiwa huyo, Masoud alisema kuwa amewaita kwenda kushuhudia moja ya mafanikio ya shirika hilo katika vita vyake dhidi ya wale wote wanaolihujumu kwa kuliibia umeme kiasi cha kuathiri mapato yake.

“Na kwa kuwa tunaenda kumkamata mmoja wa watu ambao wamekuwa wakiliibia umeme kwa muda mrefu shirika kwa njia ya mtandao, imetubidi tuombe msaada wa Kamanda Suleiman Kova (Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam) atupatie vijana wake wazuri ili zoezi letu lisije ‘likafeli’ kutokana na kuvuja kwa taarifa na kumfikia mhusika,” alisema.

Alisema ni muhimu kwa wananchi wote wakaelewa kwamba Tanesco ya sasa si ya zamani na imejipanga kwa ukamilifu kuwatafuta wote wanaolihujumu shirika wao wenyewe au kwa kushirikiana na wafanyakazi toka ndani ya shirika lake, kwa njia zozote zile hasa za kuliibia umeme.

Aliwaasa wananchi ambao wamejiunganishia umeme bila ya kufuata taratibu au wanaopata umeme kwa bei isiyo ya shirika kuwasiliana na shirika mara moja ili kurekebisha kasoro zilizopo kwa kuwa limejidhatiti kuona kuwa halihujumiwi tena.    

IBRAHIMU SAID ANENA


Kwa upande, Said alikana kufanya biashara hiyo na kusema kwamba yeye ni mfanyakazi wa kampuni iitwayo Low Voltage Distribution Contractor inayomilikiwa na Mussa Haji, kampuni ambayo alisema inafanya kazi ya kandarasi ya umeme na imekuwa kwenye biashara hiyo kwa zaidi ya miaka kumi.

“Kwa hiyo si kweli kwamba tunawauzia umeme wananchi, bali tunafanya kazi ya kandarasi za umeme na kwamba kampuni yetu imesajiliwa kwenye Bodi ya Wakandarasi,” alisema.

Alipoulizwa kuhusiana na vifaa vilivyokutwa katika ofisi yao, alisema ni vya kwao ambavyo wanavitumia katika shughuli zao za kila siku ikiwa ni pamoja na kuweka takwimu za wateja wao.

Alipoulizwa kama ni vya kampuni yao kwa nini basi baadhi ya vifaa hivyo kama mafaili na unifomu vina nembo ya Tanesco, alikaa kimya.

MWENYE NYUMBA ANENA

Naye mmiliki wa nyumba ambayo ilikuwa na ofisi hiyo, Bakari Issah, alisema kwamba anamfahamu mwenye kampuni ambaye alimpangisha katika nyumba yake kuwa ni Mussa Mtavasi ambaye kampuni yake inafanya kazi ya kuweka umeme kwenye maeneo mbalimbali.

“Ninavyofahamu mimi ni kwamba, kampuni ya Mtavasi ina miaka mingi katika nyumba yangu. Alipanga mara ya kwanza, baadaye akahama na kisha akarudi tena. Ana zaidi ya miaka mitatu tokea aje kupanga safari hii ya mwisho,” alisema.

Alipoulizwa kama anajua kwamba mpangaji wake alikuwa akiuza umeme isivyo halali, alisema hafahamu kwa kuwa alikuwa na luku yake na kwamba baada ya mpangaji wake kuweka ofisi yake aliweka luku yake nje tofauti na ile inayotumika katika nyumba.

Alisema kwamba hata umeme ambao anautumia katika nyumba yake hununua katika ofisi za wauzaji wanaotambulika na Tanesco na si katika ofisi hiyo.

BALOZI WA ENEO HILO ATETA

Kwa upande wake, Balozi wa Shina la Mwinjuma Road ilipo ofisi hiyo, Saidi Mzungu, alisema kwamba kampuni inayotuhumiwa iko katika eneo hilo kwa zaidi ya miaka kumi hadi hivi sasa, ila hakujua kama inafanya kazi ya kuuza umeme.

Baadaye polisi walimchukua Said kwenda kituo cha Polisi Oysterbay.

Masoud alisema wataalamu wa tanesco watafanyia kazi kujua thamani ya umeme aliyoiba pamoja na gharama zake.
CHANZO: NIPASHE

No comments: