ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 27, 2012

Sensa ni moto, wawili mbaroni

  Maeneo mengi hali ni shwari
  Vifaa ni tatizo, nyumba zafungwa
Sensa ya watu na makazi ilianza jana nchini nzima kwa mafanikio makubwa licha ya changamoto kadhaa kujitokeza, ikiwamo baadhi ya watu, hususan waumini wa dini ya Kiislamu kususia kushiriki kwa madai ya kutokuwapo kwa kipengele cha dini katika madodoso ya sensa.

Hatua ya waumini hao kususia sensa imeripotiwa kwenda mbali zaidi, baada ya baadhi yao kutiwa mbaroni na polisi kwa madai ya kuhamasisha watu wasishiriki na wengine kuwazuia makarani wa sensa kufanya kazi yao kwa kuwanyang’anya vifaa vya kazi.



Matukio hayo yalitokea kwa nyakati tofauti katika maeneo ya Wilaya za Ilala, Kinondoni na Temeke, jijini Dar es Salaam.

Zoezi hilo lilianza juzi usiku jijini Dar es Salaam kwa makarani kuchukua takwimu za watu kwenye maeneo wanayokaa watu wasio na makazi maalum, ikiwamo nyumba za kulala wageni, uwanja wa ndege, vituo vya mabasi na treni.

NIPASHE, ambayo ilizungukia maeneo ya Tabata, Buguruni, Vingunguti, Manzese, Ubungo, Kimara, Goba, Mbezi Beach, Keko, Temeke na Tandika, katika maeneo hayo, kuanzia saa 1.30 asubuhi hadi saa 9 alasiri, ilishuhudia makarani wakiendelea na kazi hiyo, huku changamoto hizo zikijitokeza.

Katika Wilaya ya Temeke watu 20, walikamatwa na polisi, watatu kati yao wakituhumiwa kukutwa na mabango yanayohamasisha watu kususia sensa na 17 kukataa kutoa taarifa kwa makarani wa sensa.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Temeke, David Misime, aliliambia NIPASHE jana kuwa waliokataa kutoa taarifa kwa makarani wa sensa, wanne walikamatwa eneo la Mbagala Kibangulile, Kata ya Mianzini, mmoja Kigamboni na tisa Kilakala.

Alisema watu watatu waliokutwa wakibandika mabango hayo, walikamatwa eneo la Mbagala Kiburugwa.

Kamanda Misime alisema watuhumiwa wote wanahojiwa na polisi na kwamba, ushahidi unakusanywa na ukikamilika watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Katika Wilaya ya Kinondoni Mkazi wa Magomeni, Salum Ndunguri (40) alikamatwa kwa tuhuma za kumnyang’anya karani wa sensa vifaa vya kazi .

 Naye Khalfan Juma (27), Mkazi wa Kimara Mwisho,  alikamatwa kwa tuhuma za kuhamasisha watu kususia zoezi hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Charles Kenyela, alithibitisha kukamatwa kwa watu hao kwa tuhuma hizo na hadi tunakwenda mitamboni walikuwa wakishikiliwa katika vituo tofauti vya polisi.

Alisema Nduguri alikamatwa eneo la Magomeni baada ya karani wa sensa, Angela Silayo, kufika nyumbani kwake kwa lengo la kuchukua takwimu za sensa na kumnyang’anya makabrasha ya kazi.

 Kwa upande wa Khalfan, alisema alikamatwa baada ya kukutwa maeneo ya Kimara akiwa amebeba bango linalohamasisha watu wasishiriki sensa.

Bango hilo lina maandishi yanayosomeka: “Waislamu hatuhesabiwi sensa kwa sababu ya Mwenyezi Mungu.”

 Hadi tunakwenda mitamboni, Khalfan alikuwa akishikiliwa katika kituo cha polisi Wilaya ya Kipolisi Kimara kilichoko Mbezi Kwa Yusufu.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, alisema hadi jana jioni hali ya usalama ilikuwa nzuri na kwamba, hakukuwa na mtu aliyekamatwa kwa kuhusika na vurugu katika zoezi la sensa.

Eneo la Goba, baadhi ya nyumba zilishuhudiwa zikiwa zimebandikwa mabango yanayosomeka: “Sisi Waislamu, nyumba hii hatuhesabiwi.” 

Mbali na hayo, baadhi ya waumini wanadaiwa kuwafukuza majumbani mwao makarani wa sensa na wengine kufunga nyumba zao na kisha kuondoka wakikwepa kuhesabiwa.

Tukio la kufukuzwa kwa makarani, lilishuhudiwa na NIPASHE katika maeneo ya Ubungo Kibangu, jijini Dar es Salaam.

Makarani hao wakiwa wamejiandaa kwa ajili ya sensa, walifika katika moja ya nyumba hizo na kuwakuta watoto.

Baada ya kujitambulisha, watoto hao waliwaeleza makarani hao kuwa hawawezi kuamua lolote mpaka kwanza wawasiliane na baba yao, jina lihahifadhiwa ili aruhusu ama kuhesabiwa au la.

Watoto hao waliwasiliana na baba yao, ambaye kupitia simu ya mkononi aliomba kuongea na makarani waliofika nyumbani kwake.

Watoto waliwapa makarani simu na mkuu huyo wa kaya alijitambulisha kuwa yeye ndiye mwenye nyumba na kuwaeleza kuwa yeye na familia yake hawako tayari kuhesabiwa, hivyo akawataka waondoke.

“Kwa kuwa hawakutaka kutupa ushirikiano tulilazimika kuondoka,” alisema mmoja wa makarani hao, Joyce Malangalila.

Aidha, nyumba zilizofungwa kwa madai ya wenyeji kukwepa kuhesabiwa, zilishuhudiwa maeneo ya Buguruni, Vingunguti, Tandika na Kimara.

Mbali na nyumba kufungwa, pia baadhi ya Waislamu katika maeneo ya Tabata Darajani, walishuhudiwa wakiwagomea makarani wa sensa kuhesabiwa.

Kutokana na hali hiyo, Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Tabata Darajani, Cleophas Chiwangu, aliyekuwa akiwaongoza makarani hao, aliwasiliana kwa simu na polisi wa kituo cha Buguruni kuwataka wafike ili kuwatia mbaroni waumini hao kwa kukwamisha zoezi hilo.

Polisi walifika eneo hilo, lakini wakasema kwa kuwa sensa itachukua wiki nzima, watu hao wanatakiwa kuelimishwa ili waelewe umuhimu wake, badala ya kutumia nguvu.

Wakati hayo yakijiri, baadhi ya misikiti ya Mwananyamala, Kinondoni, Magomeni, Tandika, Mbagala, Temeke na Ubungo, ilishuhudiwa ikihamasisha waumini kutoshiriki sensa kwa kusambaza vipeperushi.

Baadhi ya vipeperushi viliwataka waumini kususia sensa na katika kutekeleza hilo, viliwataka kwenda misikitini kukaa Itiqafu (kutawa msikitini) kufanya maombi mbalimbali katika muda wa sensa.

VIFAA BADO TATIZO

Wakati hayo yakijiri Dar es Salaam, katika baadhi ya mikoa, vifaa hususani sare za makarani na madodoso vilichelewa kufika hivyo kuchelewesha zoezi hilo.

Mkoani Kilimanjaro zoezi hilo lilianza vizuri licha ya kuwepo kwa kasoro ndogo ndogo kama ukosefu wa vifaa vya kuwatambulisha makarani na wasimamizi wanaofanyakazi hiyo.

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, alithibitisha kuwepo kwa mapungufu hayo, ikiwemo makarani na wasimamizi kukosa sare za fulana, kofia na majeketi maalum (Reflectors), ambazo ni moja ya vifaa muhimu katika kuwatambulisha.

Alisema hadi wakati zoezi hilo linaanza kwa mkoa mzima, hakuna aliyepata vifaa hivyo ingawa vingine vimepatikana na kwamba matumani ni kuvipata wakati zoezi likiendelea.

“Tulichofanya kama serikali ya mkoa nikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Sensa ya mkoa, kila karani kwenye eneo lake anapaswa kushirikiana na viongozi wa mitaa na vijiji, ambao tumewapa mafunzo ili iwe rahisi kufika kwenye meneo husika bila usumbufu,” alisema.

Akizungumzia kikundi cha watu kilichokuwa kimepanga kugomea sensa, alisema katika eneo la Kifaru wilayani Mwanga, kwenye msikiti wa Answar Sunna, yupo kiongozi ambaye aliwataka watu kugomea zoezi hilo, lakini baada ya serikali kuingilia kati alikubali kushirikiana na makarani pamoja na wasimamizi kupita kwenye nyumba alizokuwa amewaambia wasihesabiwe.

Alisema katika wilaya za Mwanga, Hai, Moshi na Same makarani walianza zoezi hilo kwa maeneo korofi ambayo kikundi hicho kiliwataka wasihesabiwe ikiwemo kwenye taasisi za Kiislamu kama shule na vyuo, ambako baada ya kikao cha muda mrefu walikubali zoezi hilo kuendelea.

Naye, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, alisema kwa ujumla hali ya ulinzi na usalama kwenye zoezi hilo ni mzuri na kwamba watu wanaendelea kuhesabiwa na hakuna aliyekataa.

Baadhi ya wasimamizi na makarani, walisema kukosekana kwa vifaa hivyo kuna athari kubwa kwao kwani maswali yamekuwa mengi na hivyo kutumia muda mrefu kuwaelewesha wananchi ili wahesabiwe.

Hali kama hiyo imejitokeza katika mikoa ya Geita, Dodoma na Kigoma.
Imeandikwa na Muhibu Said, Dar; Salome Kitomary, Moshi
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: