Friday, August 10, 2012

Wapinzani wamlipua Mkurugenzi wa Mifugo


Waziri,Dk David Mathayo David
Daniel Mjema, Dodoma
KAMBI ya Upinzani Bungeni, jana ilimlipua Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Mifugo, Dk E. J. Sekidio kwa kutoa vibali vya kuagiza tani 127 za nyama ya kuku kutoka nje ya nchi, hasa kutoka Brazil.

Kwa mujibu wa kambi hiyo, uagizaji huo wa kuku ni kinyume cha sheria za nchi na matamko mbalimbali yanayotolewa mara kwa mara bungeni na Serikali.

Suala hilo liliibuliwa bungeni jana na Msemaji wa kambi hiyo, Sylvester Kasulumbai, wakati akiwasilisha maoni ya kambi hiyo kuhusu bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi iliyowasilishwa na waziri wake, Dk David Mathayo David.

Kasulumbai alisema Aprili 5 mwaka huu mkurugenzi huyo alitoa kibali namba 000551 kwa kampuni ya Frostan Ltd ya jijini Dar es Salaam  kuagiza tani 27.1 za nyama ya kuku kutoka Brazil.

Alisema Julai 20 mwaka huu, mkurugenzi huyo pia alitoa kibali kingine chenye namba 00000409 kwa Kampuni ya Malik Faraji, kuagiza tani 100 za nyama ya kuku kutoka Zanzibar.

Kwa mujibu wa msemaji huyo, tani hizo 100 za nyama za kuku zilizoagizwa kutoka Zanzibar zilikuwa ni kwa ajili ya migodi ya madini ya Barrick.

“Taarifa zinaonyesha kuwa Tanzania ina kuku takribani milioni 58 wanaofugwa, lakini pamoja na kuku wote hao bado wizara imeendelea kutoa vibali vya kuagiza kuku kutoka Brazil,”alisema.

Kambi hiyo iliitaka Serikali kutoa maelezo kama ni sahihi kuendelea kutoa vibali vya kuagiza kuku kutoka nje ya nchi wakati nchi ina wafugaji
wa kuku.

“Tunataka kujua nyama za kuku kiasi cha tani 100 zilizoagizwa kutoka Zanzibar ni kutoka nchi gani na kama ni kutoka Zanzibar, kwanini wanahitaji kibali kusafirisha nyama kuja bara,”alisema.

Kambi hiyo pia imekilipua kiwanda cha sukari cha Kagera Sugar kwa kutumia ekari 45,000 ilizopewa na Serikali. kulikodisha kwa wafugaji wa Rwanda na Uganda.

Kasulumbai alifafanua kuwa vitalu vya Ranchi ya Kitengule viligawiwa kwa wafugaji wawekezaji wadogo wadogo ambapo kila mmoja alipata kati ya hekta 2,000 na 3,000.

“Lakini cha ajabu kiwanda cha Kagera Sugar kilipewa hekta 45,000 wakati kiwanda hicho hakina mifugo kwa kisingizio tu cha kutaka kulima miwa ndani ya eneo hilo la ufugaji,” alisema.

Kasulumbai alisema kiwanda hicho hivi sasa kinatumia eneo hilo kukodisha wafugaji wa Rwanda na Uganda, ilihali wafugaji wa Tanzania wakikosa eneo la kulishia mifugo yao.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake