CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesitisha mikutano yake
ya Oparesheni Sangara na Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), iliyokuwa
ikiendelea mkoani Iringa.
Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Bw.
Hamad Yusuph, aliyasema hayo mjini hapa jana wakati akizungumza na
waandishi wa habari juu ya vurugu zilizosababaisha kifo cha mwandishi wa
Kituo cha Chanel Ten, marehemu Daudi Mwangosi.
Alisema uamuzi
huo umefikiwa na viongozi waliokuwa wakiratibu operesheni hiyo ili
waweze kurudi Dar es Salaam ambapo Jumapili wiki hii watakutana na
Kamati ya Halmashauri Kuu kujadili vurugu hizo ambazo zilitokea wilayani
Mufindi.
“Tumeamua kusitisha operesheni zetu kwa muda ili
tukakakutane na Kamati ya Halmashauri Kuu tuweze kujadili matukio
yaliyojiri likiwamo la kuuawa kwa mwandishi,” alisema Bw. Yusuph.
Katika
hatua nyingine, Bw. Yusuph amemtupia lawama Mkuu wa Jeshi la Polisi wa
Mkoa hapa, Charles Kamuhanda na kudai ndiye chanzo cha vurugu
zilizotokea Kijiji cha Nyololo.
Alisema baada ya viongozi wa
CHADEMA kuwasili na Kamanda wa operesheni hiyo, Bw. Single Kigairo,
katika eneo la Nyololo, polisi waliwazuia kufanya mikutano ya hadhara.
“Sisi
tulikubaliana na agizo lao lakini tulimuomba Kamanda wa Polisi Wilaya
ya Mufindi ili tufungue matawi ya chama na alikubali pamoja na kuwapa
maelekezo askari wake wasifanye lolote, baada ya makubaliano hayo
tulifanikiwa kufungua tawi la kwanza.
“Wakati tukiwa katika
harakati za ufunguzi wa tawi la pili, ghafla aliwasili Kamanda Kamuhanda
na kuamuru wafuasi watu wakae chini na kunyoosha mkono juu mikono juu
agizo ambalo tulilizingatia bila matatizo,” alisema.
Aliongeza
kuwa, jambo la kushangaza Kamanda Kamuhanda aliagiza wafuasi wa chama
hicho wakamatwe ndipo vurugu hizo zilipoanza kutokea na kusababisha
mauaji.
Akizungumzia mazingira yaliyosababisha kifo cha Mwangosi,
alisema polisi ndio waliomuua wakati akimtetea mwandishi wa Gazeti la
Nipashe, Bw. Godfrey Mushi, ambaye alikamatwa na polisi na kushambuliwa
wakati akikimbia moshi wa mabomu.
Alisema kabla ya kukumbwa na
umauti, marehemu Mwangosi alikuwa akirekodi matukio ya siku hiyo lakini
baada ya vurugu hizo kuanza, kila mmoja alianza kutafuta njia ya kuokoa
maisha yake
CHANZO MAJIRA
No comments:
Post a Comment