ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, September 30, 2012

Hanang` hapatoshi: Sumaye ampiga `madongo` Nagu


Waziri Mkuu mstaafu, Fredrerick Sumaye
Tambo za kuwania ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), zimefikia ukomo, huku Waziri Mkuu mstaafu, Fredrerick Sumaye ‘akimpiga madongo’ Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwezeshaji), Mary Nagu.
Hatua hiyo imefikiwa jana wakati wawili hao na Leonsi Marmo, waliopitishwa kuwania nafasi hiyo, walipofanya kampeni zao jana.
NIPASHE Jumapili ilielezwa Sumaye, alipopata fursa ya kujieleza, alisema ikiwa atachaguliwa kushika nafasi hiyo, atairejesha hadhi ya CCM inayopotea wilayani humo.

Chanzo cha habari kilichoshiriki mkutano wa uchaguzi kwenye ukumbi wa ofisi za CCM wilayani humo, kilieleza kuwa, Sumaye alisema akiwa Mbunge wa Hanang’, CCM ilikuwa na nguvu dhidi ya upinzani tofauti na ilivyo sasa.
Sumaye alikaririwa akisema, wakati aking’atuka kuwania ubunge wa Hanang’, akimwachia Nagu, eneo hilo lilikuwa na diwani mmoja tu wa upinzani.
Lakini, Sumaye alielezea kushangazwa kwake na jinsi idadi ya madiwani ilivyopanda kutoka mmoja mwaka 2005 hadi 13 waliopo sasa.
“Hiki ni kielelezo kwamba CCM inapoteza nguvu na mvuto wake kwa umma, nimeliona hilo na kuliweka kuwa moja ya maeneo ya kuyafanyia kazi,” alikaririwa akisema.
Naye Nagu, alikaririwa akisema anafaa kushika wadhifa huo baada ya kuchukua uamuzi huo binafsi, na si kutumwa na mtu mwenye nia ya kuwania urais mwaka 2015 kama inavyoelezwa.
Nagu amekuwa akitajwa na kashfa ya kutumwa na kuungwa mkono na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa.
Hata hivyo, Nagu na Lowassa wamekuwa wakiyakanusha madai hayo, huku Lowassa akisema wote wawili (Nagu na Sumaye) ni rafiki zake.
Naye Leonsi Marmo anayepewa nafasi finyu ya kushinda, alisema anafaa kuchaguliwa kwa vile muda wote wa maisha yake anaishi Hanang’, tofauti na wagombea wenzake.
Hadi tunaingia mitamboni, taarifa kutoka Hanang’ zilieleza kuwa wajumbe wa kata 10 kati ya 25 zilizopo wilayani humo, zilikuwa zimeshapiga kura.
Hali hiyo ilisababisha uwezekano wa uchaguzi huo kufanyika hadi usiku wa manane.
HOFU YA VURUGU
Taarifa za awali zilieleza kuwepo njama za kutaka kuvuruga uchaguzi huo, zikimhusisha mmoja wa wagombea wa ujumbe wa Nec.
Hali hiyo ilitokana na madai kuwa mgombea huyo alisafirisha baadhi ya wanachama wanaohusika kupiga kura, miongoni mwa wao wakifika mjini hapa siku kadhaa kabla ya jana.
Hata hivyo, hapakuwa na taarifa zozote za mapigano, zaidi ya wapiga kura kuendesha kampeni za chini chini, hata baada ya wagombea wote kujieleza ukumbini.
“Kuna watu waliletwa na huyu (anataja jina la mgombea), tukaambiwa watasababisha vurugu lakini hapakuwa na vurugu zozote, hali imekuwa shwari,” alisema mmoja wa wapiga kura anayejitambulisha kwa jina moja la Lucas.
MATOKEO YA IRINGA MJINI
Kutoka mkoani Iringa, Abeid Kiponza ameshinda katika nafasi ya uenyekiti wa CCM wilaya ya Iringa Mjini
Kiponza alipata ushindi huo kwa kupata kura 298 kati ya 586 zilizopigwa ambapo 2 ziliharibika, akiwashinda Eliud Mvela (224) na Omary Mchomba (62)
Kwa upande wa ujumbe wa Nec, Mahmudu Madenge aliibuka mshindi kwa kupata kura 281 kati ya 538 zilizopigwa, huku 14 zikiharibika.
Madenge aliwashinda Vitus Mushi (243), Michael Mlowe (86) na Enock Ugulumu (62).
Kwa upande wa nafasi mbili za Jumuiya ya Wazazi kwenda Halmashauri Kuu washindi ni Shedraki Mkusa aliyepata kura 334 na Ali Mbata (269).
Jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT), washindi walikuwa ni Halima Hassan (266), Ashura Jengo (291), Nikolima Lulandala (325) na Fatuma Daudi (338).
Upande wa jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM), washindi ni Ally Simba (250), Salim Kaita (254), Mwaija Mwinyikayoke (270) na Clara Shirima (299)
Nafasi za tano za kuwania ujumbe wa Mkutano Mkuu wa taifa zilienda kwa
Agusta Mtemi (192), Abeid Kiponza (235), Amani Mwamwindi (311), Frederick Mwakelebela (321) na Salum Asas (346).

WAZEE DODOMA WAKANUSHA ‘KUHONGA’ WAJUMBE
Baraza la wazee wa CCM Mkoa wa Dodoma, limekanusha uvumi kuwa limewabeba baadhi ya wagombea wa nafasi mbalimbali mkoani hapo.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Kaimu Mwenyekiti wa baraza hilo, Balozi
Job Lusinde, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa.
Alisema kuwa baraza hilo haliko tayari kumbeba mgombea yeyote katika uchaguzi unaoendelea ndani ya CCM. Alisema kuwa wazee wa baraza hilo, wamefurahishwa na kitendo cha Nec, kuwateua vijana kuwania nafasi hizo.
“Ni vyema wagombea hao kufanya kampeni zao bila uhasama wala kuchafuana, huku wakizingatia amani na utulivu kwa nguvu ya hoja, bila kuhusisha baraza la wazee wa CCM Dodoma,”alisisitiza Lusinde.
Habari hii imeandikwa na Mwandishi Wetu, Hanang’, Mashaka Mgeta, Dar es Salaam na Augusta Njoji, Dodoma.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: