Chanzo simu ya mkononi
Ajali hiyo ilitokea jana majira ya saa 2:30 asubuhi katika eneo la Matundasi umbali wa kilometa 21 nje ya mji wa Chunya, wakati wajumbe hao wa CCM zaidi ya 100 wakitokea katika kata za Lupa, Upendo na Mamba kwenda kwenye mkutano wa uchaguzi.
NIPASHE ambalo lilifika kwenye eneo la tukio na baadaye kwenye Hospitali ya Wilaya ya Chunya, lilishuhudia magari ya kubeba wagonjwa zaidi ya matatu yakisomba majeruhi kuwatoa eneo la ajali na kuwapeleka hospitalini, huku wengi wao wakiwa na majeraha mabaya katika sehemu mbalimbali za miili yao.
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya wilaya ya Chunya, Dk. Henry Mwansasu, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kudai kuwa amepokea mwili wa mtu mmoja pamoja na majeruhi 85.
Amemtaja mtu aliyepoteza maisha kwenye ajali hiyo kuwa ni Issaya Nchimbi (45), ambaye ni Katibu wa Uchumi na Fedha wa tawi la CCM la Madimbwini katika kata ya Mamba wilayani Chunya.
Alisema kati ya majeruhi hao, 11 hali zao ni mbaya na wamelazwa hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu na uchunguzi zaidi, huku majeruhi wengine 63 ambao walipata mshtuko na majeraha madogo madogo wakipatiwa matibabu na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Akizungumza na gazeti hili katika Hospitali ya wilaya ya Chunya, mmoja wa majeruhi hao, Bw. Frank Bone (40), mkazi wa Lupa Tingatinga, alisema mbali na ajali hiyo kusababishwa na dereva ambaye alitaka kupokea simu huku gari likiwa kwenye mwendo mkali, pia gari hilo lilikuwa limajaza abiria kupita kiasi, hivyo muda mwingi wa safari yao lilionekana kumshinda dereva.
Alisema kuwa waliianza safari yao kutoka kijiji cha Mamba majira ya saa 9:00 usiku na kuwapitia wajumbe wengine wa kata za Lupa na Upendo, ingawa gari lilijaa baadhi walining’inia kwenye mabomba ya vyuma.
Mwingine aliyejeruhiwa paji la uso, Jamson Mwaluka, mkazi wa kata ya Lupa, alisema kabla ya ajali dereva wa gari hilo, aliyetajwa kwa jina moja la Mchungaji, alipigiwa simu na ndicho chanzo cha ajali hiyo.
“Dereva alipigiwa simu iliyokuwa mfukoni, wakati anahangaika kuitoa gafla alijikuta yuko kwenye kona na alipojaribu kuliweka sawa ndipo gari lilipoteza muelekeo na kupinduka,” alisema Mwaluka.
Kwa mujibu wa majeruhi hao, gari hiyo ilibeba zaidi ya watu 100 ambao wote walikuwa ni wajumbe wa Mkutano Mkuu wa uchaguzi wa CCM wilaya ya Chunya, kutoka kata tatu za Mamba, Lupa, Tinga na Upendo katika jimbo la Lupa.
Hata hivyo, licha ya ajali kutokea, mkutano wa uchaguzi uliendelea kama ulivyopangwa, huku baadhi ya majeruhi walioruhusiwa kutoka hospitalini nao wakijumuika kushiriki kwenye uchaguzi na wengine ambao wamelazwa wakiandaliwa utaratibu wa kupiga kura wakiwa wodini.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment