Mahakama nchini Zimbabwe
imesitisha harusi ya Waziri Mkuu wa Zimbabwe Morgan Tsvangirai
iliyotarajiwa kufanyika hapo kesho kama ilivyokuwa imepangwa.
Mahakama imesema kuwa Tsvangirai tayari ana mke.
Mapema wiki hii mahakama kuu nchini
humo ilitupilia mbali madai ya Locadia Tembo aliyesema kuwa yeye ni mke
wa kitamaduni wa Bwana Tsvangirai na kusema kuwa ndoa za kitamaduni
hazitambuliki kisheria.
Lakini sasa Hakimu amekubaliana na Locadia na kuamuru harusi iliyopangwa kufanyika siku ya Jumamosi haitafanyika tena.
Hii ni licha ya baadhi ya viongozi wa nchi mbali mbali walioalikwa kwa harusi kuwasili nchini humo.
Mawakili wa Tsvangirai wanataka mahakama kutoa amri ya dharura na kuruhusu harusi hiyo kuendelea kama ilivyopangwa.
Kesi nyingine ambayo mahakama ilisikiza leo
dhidi ya Tsvangirai ni ya mwanamke mmoja kwa jina Nozipho Shilubane
aliyesema kuwa Waziri Mkuu huyo aliahidi kumuoa.
Baadhi ya wadadisi wanasema kuwa kesi hiyo ni
dalili ya njama za kisiasa kumpaka tope waziri mkuu kabla ya uchaguzi
mkuu utakaofanyika mwaka ujao. Tsvangirai atatoana jasho na rais Robert
Mugabe katika uchaguzi huo.
Lakini wengine wanasema kuwa Tsvangirai hana wa
kulaumu ila yeye mwenyewe kwani amejihusisha na wanawake wengi baada ya
mke wake kufariki katika ajali ya barabarani mwaka 2009 baada ya waziri
mkuu kuchukua wadhifa wake.
Mwandishi wa BBC Brian Hungwe mjini, Harare,
anasema kuwa harusi hiyo ilipangwa kufanyika katika mtaa mmoja wa
kifahari mjini Harare.
Rais Mugabe anatarajiwa kuandaa dhifa maalum kwa viongozi wa nchi za kiafrika walioalikwa kuhudhuria.
No comments:
Post a Comment