CCM NZEGA YATISHIA KUMVUA UANACHAMA,ASEMA YUKO TAYARI KUJIUZULU UBUNGE
Fidelis Butahe Dar na Mustapha Kapalata, Nzega
SAKATA la makada wa CCM, Hussein Bashe na Dk Hamis Kigwangala kutoleana bastola, limechukua sura mpya baada ya Jeshi la Polisi kuingilia kati na kumnyang’anya bastola Kigwangala huku likianza kuwahoji wapambe wa mahasimu hao.
Habari zilizopatikana jana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, (RPC) Antony Lutta zilieleza kuwa jeshi hilo linaishikilia silaha ya Dk Kigwangala hadi hapo uchunguzi utakapokamilika.
Kauli hiyo ya polisi imekuja siku moja baada ya uongozi wa chama hicho Wilaya ya Nzega, kutaka suala hilo liondolewe polisi ili walishughulikie kimyakimya ndani ya chama.
Mwananchi Jumapili lilipomtafuta Dk Kigwangala ambaye pia ni Mbunge wa Nzega na kumuuliza kuhusu suala hilo alisema: “Bastola yangu mbona ninayo, hilo halina ukweli, bastola ninayo hapa.”
Wakati hayo yakiendelea, uongozi wa CCM wilayani humo umempa onyo kali Dk Kigwangala ukieleza kwamba endapo ataendeleza msimamo wake wa kukataa kuhojiwa na chama, atachukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kunyang’anywa kadi ya uanachama.
Kujiuzulu ubunge
Hata hivyo, mbunge huyo alisema kuwa hana imani na uongozi wa CCM wilayani Nzega na kwamba iwapo CCM mkoa na taifa hautaingilia kati mgogoro huo, yuko tayari kujiuzulu ubunge.
Bashe na Dk Kigwangala ambao ni mahasimu wa siku nyingi katika medani za siasa wilayani Nzega walidaiwa kutoleana bastola Alhamisi iliyopita walipogongana katika ofisi za CCM wilayani humo, wakati wakirejesha fomu za kuwania Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) kupitia wilaya hiyo.
Hata hivyo, pamoja na taarifa hizo kuthibitishwa na viongozi wa CCM wilayani humo na RPC Lutta, kila mmoja alikanusha madai hayo akimtuhumu mwingine kuwa ndiyo chanzo cha ugomvi huo.
Wakati Bashe alisema Dk Kigwangala ndiye aliyetoa bastola kumtishia wakiwa ndani ya Ofisi ya CCM Wilaya, Dk Kigwangala alieleza kuwa walinzi wa Bashe ndio waliomtishia yeye bastola na kwamba tayari amelifikisha suala hilo polisi na wanalifanyia kazi.
Kauli ya Kamanda Lutta
Jana Lutta alisema ingawa imemnyang’anya bastola Dk Kigwangala, mbunge huyo anamiliki silaha hiyo kihalali.
“Taarifa zao tutazitoa baadaye kwa sababu hivi sasa tunakusanya ushahidi na tunawahoji wapambe wao, ambao inasemekana wakati tukio linatokea walikuwepo eneo hilo,” alisema Lutta na kuongeza:
“Silaha yake ipo katika Kituo cha Polisi Nzega, uchunguzi tulioufanya unaonyesha kuwa ni yake, anaimiliki kihalali. Ni kweli ndugu yangu silaha yake tunaishikilia.”
Alisema kuwa kazi ya polisi ni kuchunguza tukio zima na ikikamilisha uchunguzi wake, itaupeleka katika mamkala husika.
CCM watoa tamko zito
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nzega, Francis Shija alisema tangu kutokea kwa tukio hilo, Dk Kigwangala alikataa kutoa maelezo katika kikao cha dharura cha Kamati ya Siasa Wilaya kilichofanyika juzi na kile cha Kamati ya Maadili kilichofanyika jana.
Alisema vikao bado vinaendelea ili kubaini ukweli wa tukio hilo na kuongeza kuwa uongozi wa chama utahakikisha haki inatendeka kwa watuhumiwa hao, ili kila mmoja apewe adhabu yake pamoja na onyo kali, kama wanastahili.
“Vikao vitaendelea ili kubaini ukweli na mtu atakayekaidi kutoa ushirikiano hatua zitachukuliwa dhidi yake ili iwe fundisho kwa wengine,” alisema Shija na kuongeza:
“Kama Kigwangala ataendelea kukaidi kila tutakapomwita ili aeleze kilichotokea tutamnyang’anya kadi ya uanachama, ila sidhani kama itafika huko, tutajitahidi tuyamalize kistaarabu.”
Alipoulizwa kuwa taarifa zilizopo kuwa uongozi wa CCM wilaya hiyo unampendelea Bashe alisema: “Siyo kweli, hatuegemei upande wowote katika suala hili. Kamati ya Maadili haijaegemea kwa Bashe tutahakikisha haki inatendeka na chama hiki hakina makundi kila mtu anavuna alichopanda.”
Kauli ya Kigwangala
Kwa upande wake Kigwangala alisema kuwa kikao cha Kamati ya Siasa kilivunjika jana kwa sababu hakuwa na imani na wajumbe waliokuwa wakiendesha kikao hicho.
Aliwataja wajumbe wa kikao hicho ambao hana imani nao kuwa ni pamoja na Shija na Katibu wa chama hicho Wilaya ya Nzega, Kajoro Vyohoroka.
Alisema hata kikao cha maadili ambacho kilifanyika baada ya kuvunjika kwa kikao cha Kamati ya Siasa, nacho kina watu ambao hana imani nao.
‘’Siwezi kutoa hoja zangu za msingi kwa kamati hii ya maadili, kwani hakuna kilichobadilika kwa sababu wanaokisimamia ni Shija na Vyohoroka na wote wapo upande wa Bashe. Siwezi kukubali kuhojiwa hadi jambo hili litakapopelekwa katika ngazi nyingine ndani ya chama,” alisema Kigwangala.
Alisema siasa za CCM Wilaya ya Nzega ni ‘siasa uchwara’ kwa kile alichoeleza kuwa ni kuwapo kwa makundi yasiyo na msingi wala faida kwa CCM na kusisitiza kuwa kama jambo hilo halitafanyiwa kazi yupo tayari kujiuzulu ili kumwacha Bashe aendeleze siasa uchwara.
“Endapo tatizo hili halitaingiliwa kati na CCM ngazi ya mkoa na taifa, nipo tayari kujiuzulu ubunge na kukabidhi,” alisema Kigwangala.
”Mimi silaha ninayo siku nyingi tu na hata mara moja sijawahi kumtishia mtu maisha, kama unataka kuiona ipo siku nitakuonyesha,” alisema Kigwangala akimwambia mwandishi wa habari hizi.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment