ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 18, 2012

Kwenye mapenzi kuna virusi, unapaswa kujua ‘kuskani na kudiliti’


KILA ninapotazama hatua ninazopiga kwa hakika ni Mungu tu! Anawezesha ujazo wa afya yangu na kwa hakika hata wewe umefika hapo ulipo kwa sababu anakupigania. Ipo sababu yake, jiulize ni wangapi waliotangulia. Tunakumbushana tu ndugu yangu.
Tupo kamili kwenye dimba la mapenzi. Tuendelee kuyapa nafasi ya kuyajadili, kuyachambua, kupeana muongozo kwa maana kila mmoja wetu anapaswa kupata alama A. Kama unafeli mapenzi ni furaha ipi utakayokuwa nayo? Hakikisha unafaulu.

Wakati unasaka ufaulu wako kwenye mapenzi, jipe nafasi ya kujiuliza kisha ujijibu mwenyewe, ni kwa nini mapenzi yanakuwa ya wasiwasi? Pengine wewe upo kwenye uhusiano wa mtindo huo au hata kama huhusiki, basi inawezekana ni shuhuda kwa mapenzi aina hiyo kwa mwenzako.
Kwa kifupi, mapenzi hayatakiwi kuwa ya wasiwasi. Inakuaje watu wawili wanaopendana halafu wawe na uhusiano usioeleweka? Hali ya kutokueleweka hutokea kwenye uhusiano wa watu wasiopendana. Yaani wamekutana ‘kimagumashi’, hawatafika.
Unapoingia kwenye uhusiano wa kimapenzi kabla ya kufanya jambo lolote lile, kitu cha kwanza ni kuhakiki kile kilichojazwa ndani ya moyo wako. Unapenda kweli? Je, upendo wako kwake unatosha kukufanya umuone yeye ni taa ya maisha yako?
Majibu ya maswali hayo, yanafaa kuja baada ya kujiuliza na kujijibu kama upendo wake kwako unatosheleza. Kama ana penzi lisiloeleweka, inatakiwa uachane naye haraka kabla hata hujajipima kama unampenda. Heri nusu shari kuliko shari kamili.
Ukishapenda na moyo ukagota kwa mtu ambaye hana hisia za kweli kwako, hiyo ni shari kamili. Hapa sina maana uishi kwa mitego, isipokuwa hali ya sasa inalazimisha kila mmoja wetu kuishi kwa mtindo wa kiuchunguzi. Usiende pupa, mapenzi yanahitaji muda.
Sina maana usifanye kazi zako uanze kumfuatilia hatua kwa hatua kujua nini anachokifanya. Simaanishi uajiri mabodigadi au uweke wapambe watakaokuwa wanamfuatilia mwenzio kila anapokwenda ili kujua mizunguko yake ya kila siku. La hasha!
Kwanza niseme kuwa kumfuatilia mwenzi wako ni ‘ushamba’, nawe hutakiwi kuwa mshamba wa mapenzi. Unahitaji kuwa na akili iliyotulia wakati unapotafuta majibu sahihi kuhusu mwenzi wa maisha yako. Hupaswi kutumia nguvu kujua kama anakufaa au hakufai.
Kanuni ni moja tu, jiachie kwa mwenzako kadiri inavyowezekana. Tena kama unaweza igiza kama umekufa kwake na hujiwezi. Ukimfanyia hivyo mtu asiyekupenda, atajenga kiburi. Atajiona amekupata kisawasawa. Badala ya kuishi kulingana na upendo wako kwake, ataona fahari ukiteseka kwa ajili yake.
Fanya hivyo nyakati za mwanzo halafu umuone. Majibu utakayoyapata yatakupa njia ya kupita. Je, kuna mapenzi hapo au kizunguzungu? Inawezekana mwenzako anajua mapenzi ila alisumbuliwa na ushamba. Kwa mtu mshamba, anapoona anapendwa, huinua mabega badala ya kurudisha mapenzi anayopewa.
Mshamba wa mapenzi anapoona anapendwa, kwa kiburi humgeuza punda mpenzi wake kwa kufanya anachokitaka. Mpenzi wake akikonda, yeye atacheka. Hivyo basi, wakati mwingine anaweza akawa anakupenda isipokuwa kinachomsumbua ni ushamba wake.
Utajuaje kama ni ushamba au hakupendi? Hakikisha kwamba baada ya kuwa umeshamuonesha kwa kiwango kikubwa kuwa umekufa kwake, naye akaanza kukufanyia visa vya hapa na pale, unachotakiwa kukifanya ni kubadilika ghafla. Yaani umfanye naye asikuelewe.
Mabadiliko yako, yatamsababishia maswali mengi mwenzi wako. Kwa mtu aliyekuwa anakucheza shere, akiona umebadilika, baada ya kujiuliza mambo mengi, jibu lake litamuelekeza ajipunguze. Hapo utakuwa umefanikiwa kukishinda kirusi hatari ambacho kingeusumbua moyo wako kwa muda mrefu.
La, asipojipunguza, ataanza kukufuatilia kwa ukaribu. Akili yake itamwambia una mtu mwingine anayekuzuzua wakati siyo kweli. Atashinda anasumbuka na simu yake akingoja umpigie lakini ataambulia sifuri. Akikupigia, pokea halafu muoneshe kwamba moyo wako una amani ya kutosha.
Mkionana, onesha uchangamfu wako. Usimfanye aone kuna upungufu ndani yako. Atakapoona una amani ya kutosha, ndivyo naye atakavyojitesa kwa maswali mengi. Baada ya hapo atanyanyua mikono kwamba hakuwezi. Sasa basi, wewe ndiye utakuwa umemuweza. Hapo tayari umemskani na umemdiliti.
Itaendelea wiki ijayo.

www.globalpublishers.info

No comments: