Simba Sc
Azam Fc
MABINGWA wa ligi kuu Bara Simba Sc leo wanashuka katika
uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuwakabili Azam Fc katika mchezo wa
kuwania Ngao ya Jamii.
Mchezo wa leo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa
kutokana na kila timu kuhitaji kushinda kombe hilo ambapo pande kila timu
imejinasibu kunyakua kombe hilo.
Akizungumzia mchezo huo, Ofisa habari wa Simba Ezekiel
Kamwaga alisema kwamba kikosi chake kipo tayari kwa mchezo huo ambao wanataka
kulipiza kisasi cha kufungwa na Azam mabao 3-1 katika mchezo wa nusu fainali ya
kombe la Kagame.
Alisema kikosi chake kipo tayari kwa mchezo huo ambapo
mafunzo ya kocha wao mkuu Milovan Cirkovic, sambamba na michezo kadhaa ya
kujipima nguvu ambayo kwa kiasi kikubwa imewapa mwanga wa kubaini mapungufu na
hivyo kuyafanyia kazi.
“Sisi ndiyo mabingwa watetezi wa ligi na pia ndiyo
tunashikilia kombe la Jamii hivyo itakuwa jambo la ajabu sana kama tutalipoteza
kirahisi kombe moja”, alisema
Kamwaga aliongeza kwamba wachezaji wote wapo katika hali
nzuri huku pia mshambuliaji wao wa kimataifa Emmanuel Okwi ambaye juzi
alijiunga na wenzake anatarajiwa kuwa mmoja ya wachezaji watakaoshuka dimbani
leo.
Kwa uapande wa Azam kupitia kwa ofisa habari wake Jaffer
Iddi Maganga, alisema kikosi cha timu hiyo kipo tayari kwa mchezo huo na kwamba
wembe waliotumia kuinyoa Simba kwenye Kagame utatumika pia na leo.
Aliongeza kwamba wachezaji wote wa fiti kwa mchezo huo
hivyo kocha atapanga mchezaji yoyote atakayeona anastahili kucheza mchezo huo.
Kwa mara ya kwanza, mechi ya ngao ya Jamii ilichezwa
mwaka 2001 ambapo Yanga iliitwaa baada ya kuifunga Simba mabao 2-1, huku mwaka
jana Simba ilitwaa ngao hiyo baada ya kuifunga Yanga mabao 2-0, wakati mwaka 2010 Yanga ilitwaa ubingwa baada ya
kushinda penalty 3-1 dhidi ya Simba na mwaka 2009 Mtibwa ilitwaa ubingwa baada
ya kuifunga Yanga mabao 2-1.
Katika hatua nyingine, Shirikisho la soka Tanzania (TFF)
limekataa ombi la vilabu vya Azam na Simba kutaka mechi hiyo ichezwe usiku
badala ya saa 10 jioni kama ilivyopagwa.
Asilimia tano ya mapato yatakayopatikana kwenye hiyo
yatakwenda kwenye Hospitali ya Temeke mkoani Dar es Salaam ambapo viingilio
katika mchezo huo vimepangwa kuwa sh 5,000 kwa viti vya rangi ya bluu na
kijani, sh. 10,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 kwa viti vya VIP C na
B wakati VIP A itakuwa sh. 20,000.
No comments:
Post a Comment