ANGALIA LIVE NEWS

Monday, September 17, 2012

Pinda kutoa maamuzi magumu dhidi ya Halmashauri Misungwi




Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, huenda akalazimika kuivunja Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza baada ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Bernard Polycalp, anayetuhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha za maendeleo kugoma kujiuzulu kwa hiari.

Akiwahutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika juzi kwenye uwanja wa Mwanakenenge mjini Misungwi baada ya kufanya ziara ya kukagua shughuli za maendeleo, Pinda alisema atalazimika kufanya maamuzi magumu ikibidi kuivunja halmashauri hiyo kama njia ya kumuondoa Mwenyekiti huyo ambaye amekataa katakata kujiuzulu licha ya chama chake (CCM) kumtaka afanye hivyo kwa hiari.

Pinda alisema mbali na CCM mkoa wa Mwanza kumshauri ajiuzulu, hata yeye (Pinda) amejaribu kumshauri mara mbili lakini bado aligoma kuachia ngazi.



“Juzi Mwenyekiti wenu wa Halmashauri (Polycarp), alikuja pale Ikulu ndogo (jijini Mwanza), tukazungumza naye kuhusu tuhuma zinazomkabili, nikamshauri alijiuzulu lakini akakataa akidai eti anayesababisha achukiwe na wananchi ni Mbunge," alisema.

Aidha, alisema wakiwa katika kikao cha ndani kilichohusisha madiwani wote wa halmashauri hiyo, alimshauri kwa mara nyingine ajiuzulu lakini aligoma.

"Mwenyekiti wenu amekataa ushauri wangu wa kumtaka ajiuzulu. Hajui kuwa mimi ndiye bosi na mwenye kauli ya mwisho. Nadhani hakuna njia nyingine isipokuwa kuivunja halmashauri. Hatma ya jambo hili itajulikana siku chache zijazo baada ya kurejea Dar es Salaam,” alisema Pinda.

Hatua ya Waziri Mkuu kuweka hadharani sakata hilo ilikuja baada ya kumuita Polycalp, aliyekuwapo kwenye mkutano huo wa hadhara awasalimie wananchi baada ya kuwa amesahaulika wakati wa utambulisho uliofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo.

“Kabla sijazungumza lolote, kuna mtu muhimu sana hapa amesahaulika kutambulishwa. Namuomba Mwenyekiti wa Halmashauri ya Misungwi aje jukwaani japo awasalimie wananchi," alisema Pinda baada ya kukaribishwa kuwahutubia wananchi.

Hata hivyo, wakati Polycalp akisimama kuelekea jukwaani, wananchi walianza kumzomea huku wakipaza sauti kumtaka Waziri Mkuu amuondoe madarakani kwa madai kuwa ni fisadi ametafuna fedha zao za maendeleo.

Licha ya kujitahidi kuwatuliza na kuwasalimia kwa kuchanganya lugha ya Kiswahili na kisha Kisukuma, Polycalp aliendelea kukabiliwa na shinikizo la kelele za wananchi ambao waliendelea kumzomea na kumuita fisadi na mchwa anayetafuna fedha za maendeleo.

“Hatukutaki, ondoka, fisadi wewe umekula fedha zetu,” walisikika wananchi wakipaza sauti, hali iliyomfanya Pinda amtake Polycalp ateremke jukwaani na kurudi kuketi.

Baada ya zomea zomea hiyo ya wananchi ndipo Waziri Mkuu alipoamua kuweka hadharani hali halisi kuhusu sakata hilo la ubadhirifu unaomkabili Polycalp na jinsi alivyokaidi ushauri wa kumtaka ajiuzulu ili kulinda heshima yake na chama chake.

Tofauti na utaratibu alioutumia wa kuwahutubia wananchi moja kwa moja wakati alipokuwa kwenye ziara katika wilaya nyingine, ilimlazimu Pinda atoe fursa kwa wananchi kuzungumza au kuuliza maswali kabla ya kuwahutubia.

Idadi kubwa ya wananchi walinyoosha mikono kutaka kuzungumza lakini Pinda alitoa nafasi kwa watu sita ambao wengi hoja zao zililenga kutaka kujua hatma ya halmashauri yao baada ya kubainika kuwepo kwa ubadhirifu uliosababisha aliyekuwa Mkurungenzi Mtendaji Xavery Tiluselekwa, ashushwe cheo na kufunguliwa mashitaka.

Akitoa ufafanuzi juu ya hoja hizo za wananchi, Pinda huku akionekana mwenye ghadhabu, alisema mwaka 2009/2010 halmashauri hiyo ilipata hati yenye shaka na mwaka wa fedha 2010/2011 chini ya uenyekiti wa Polycalp, ilipata hati chafu, hali iliyoonyesha kuwepo kwa ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma.

Alisema mbali ya ripoti hiyo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, ripoti ya Tume ya ukaguzi maalum, pia ilionyesha kuwepo kwa upotevu mkubwa wa fedha za maendeleo wilayani humo.

"Ripoti ya CAG na ile ya Tume maalum zinatueleza ukweli wa tatizo lilipo hapa Misungwi. Mwenyekiti wenu huyu amekuwa akifanya biashara na halmashauri yake kupitia kampuni yake ya ujenzi. Kimaadili, kiuongozi na kisiasa, ni jambo lisilokubalika hata kidogo,” alisema.

Pinda aliitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Mwanza kuharakisha uchunguzi wake ili watakaobainika kuhusika katika ubadhirifu wa fedha za wananchi wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.
CHANZO: NIPASHE

No comments: