Mgeja ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, amesema tuhuma zilizotolewa na Dk. Slaa dhidi ya Sitta na wabunge hao, zinathibitisha jinsi kiongozi huyo na wenzake walivyo wasaliti ndani ya chama chao na serikali, na kwamba kitendo cha kuigeuza ofisi ya spika kuwa kijiwe cha kupanga uhaini na usaliti ndani ya CCM hakivumiliki hata kidogo.
Mgeja alitoa kauli hiyo jana jijini Mwanza, alipozungumza na waandishi wa habari kwa lengo la kumpongeza Dk. Slaa kwa kufichua uozo wa Waziri Sitta na wenzake hao. Alisema Dk. Slaa ameisaidia CCM kutambua viongozi wake wanaokisaliti.
"Nianze kwa kumpongeza Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Slaa kwa kufichua madhambi ya Samuel Sitta. Huyu mtu (Sitta), ni hatari sana katika maendeleo ya chama chetu.
"Dk. Slaa ametueleza jinsi Sitta alivyotumia ofisi ya spika kama kijiwe cha kutaka kukisaliti chama chetu na kuanzisha CCJ. Huyu mtu ni hatari sana... tunaomba CCM imtose yeye na wabunge hao 55 maana uroho wao wa madaraka unaweza kuigharimu CCM.
"Kwa kashfa hii nzito dhidi yao, namshauri wapime, watafakari na hatimaye wachukuwe hatua. Pia nawashauri kwanza watubu na kuomba radhi chama na wana CCM wote, au wajiengue kwa hiari yao bila shuruti, ili walinde heshima yao. Wasingoje kuhukumiwa na wanachama," alisema.
Mjumbe huyo wa NEC na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga aliyejipambanua kupiga vita ufisadi na vitendo viovu ndani na nje ya CCM, alisema historia ya Waziri Sitta inajionesha wazi kwamba ni 'mkorofi na msaliti mkubwa', kwani mwaka 1966 akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alishiriki maandamano hadi Ikulu kupinga sheria ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Alisema katika harakati zao hizo za kupinga sheria hiyo iliyotaka kila mwanafunzi wa Chuo Kikuu lazima ajiunge na Jeshi la Kujenga Taifa, Baba wa Taifa wakati huo akiwa Rais wa nchi na mkuu wa chuo hicho, alilazimika kumchapa viboko Sitta kutokana na usaliti wake huo kwa serikali.
Mgeja alisema mbali na kufanya maandamano hayo, Sitta na wenzake ambao wengine ni marehemu kwa sasa walikuwa na mabango yenye ujumbe mkali kwa serikali, ukiwemo uliosema 'Onyo kali na la mwisho kwa serikali', na kwamba alikuwa akiipinga pia Serikali ya Baba wa Taifa huku akiusifu uongozi wa kikoloni.
"Huyu Sitta ambaye leo hii anawadanganya watu, kipindi hicho akisoma Chuo Kikuu alikuwa akiipinga serikali na kudai afadhali serikali ya kikoloni. Tusipoamini leo usaliti wake huu tunasubiri hadi aje shetani atuambie usaliti wa Sitta ndipo tuamini?
"Za mwizi ni 40, ndiyo maana tumeambiwa toka mwaka 2005 hadi 2010 huyu Sitta amekuwa akikisaliti chama chetu kupitia Bunge alilokuwa akiliongoza. Tunataka chama kimtose na kisiwaonee haya wasaliti hawa wakubwa. Wasipoondoka kwa hiari yao wataondolewa kwa nguvu ya wanachama wa CCM,” alisema.
Alimtuhumu pia Waziri Sitta kwa kauli zake za kulalamikia serikali bila kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayolikumba taifa, na alimtaka ataje jinsi alivyoisaidia serikali kupunguza tatizo la ajira kwa vijana, mfumuko wa bei, ufisadi na mambo mengine ndani ya chama na serikali.
Kwa mujibu wa Mgeja anayedaiwa kuanza kuundiwa mbinu chafu za kutaka kuangushwa katika kinyang'anyiro cha uenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga na kundi la kigogo mmoja anayetajwa kutaka kugombea urais mwaka 2010, tuhuma hizo dhidi ya Waziri Sitta zimekisaidia maradufu chama, kwani siyo Dk. Slaa pekee aliyewahi kumshutumu kiongozi huyo kwa usaliti ndani ya chama.
Alisema yupo tayari kusulubiwa, kutolewa kafara au kufukuzwa na chama kwa kusema ukweli daima, kwani anayasema hayo kwa kufuata kiapo cha katiba ya CCM.
No comments:
Post a Comment