ANGALIA LIVE NEWS

Friday, September 7, 2012

Tatizo si ndoa, ila ndoa na nani?


NI imani yangu mtakuwa salama kabisa na mnaendelea vyema na majukumu yenu ya kila siku. Kama ndivyo, sifa, heshima na utukufu Kwake aliye juu.
Marafiki zangu, leo nataka tujadili mada muhimu sana katika maisha yetu ya uhusiano. Sikia...ndoa haiji mara mbili. Ni kifungo cha moja kwa moja. Kwa maana hiyo hakuna kujaribu kwenye ndoa.
Ukifanya makosa leo mara moja tu, unakuwa umeyagharimu maisha yako yote. Najua vijana wengi (hasa wasichana) wanapata wakati mgumu sana unapofikia wakati ambao wanadhani umri wao unawapasa kuingia kwenye ndoa bila mafanikio.

Zipo dhana nyingine ambazo si sahihi. Msichana akiwa na zaidi ya miaka 25, anajiona ana nuksi na amekosa bahati ya kupata mume wake wa ndoa. Eti ndoa ni bahati! Si kweli. Si suala la bahati...huja kwa wakati unaostahili!
Utakuja kumsikia mwingine anasema: “Ni bora niolewe na yeyote atakayekuja mbele yangu, maana nahisi nina nuksi. Hakuna anayetaka kunioa, kama ni kupenda nitajifunzia huko huko.”
Huu si mtazamo sahihi marafiki zangu. Suala la ndoa si la kubahatisha. Ujue kwamba ukiingia kwenye ndoa kwa lengo la kuondoa nuksi, kweli itakuwa hivyo...maana utaolewa ili uonekane halafu siku mbili tatu, UNAACHIKA!

MASWALI YA MSINGI YA KUJIULIZA
Ndugu zangu, kabla ya kuamua kuingia kwenye uhusiano (hasa ndoa) na mwenzi uliyempenda, yapo mambo ya msingi sana ambayo ni vyema kama ungeyapa kipaumbele kichwani mwako.
Huna sababu ya kuingia kwenye ndoa kama majibu ya maswali yako uliyojiuliza si mazuri. Yana viashirio vibaya. Lazima kwanza majibu yako yawe mazuri yenye kukupa matumaini mapya katika maisha yako ya ndoa.
Ni maswali gani hayo ya kujiuliza? Twende tukaone marafiki zangu.

ULIOTA KUWA NA NANI?
Jambo la kwanza kabisa kujiuliza kichwani mwako ni kwamba, kabla ya kukutana na huyo ambaye unatarajia kuingia naye kwenye ndoa, awali uliota kuwa na nani? Lazima kichwani mwako ulikuwa na mtu uliyekuwa unawaza kuwa naye.
Zipo sifa za kawaida ambazo mtu anaweza kuvutiwa nazo kabla ya kukutana na mtu ambaye anadhani anaweza kuwa wake kwenye ndoa. Itakuwa vichekesho mwanaume kukubali kuingia kwenye ndoa na mwanamke mwembamba sana, wakati kichwani mwake alikuwa akivutiwa zaidi na wanawake wenye maumbo makubwa!
Ndugu zangu, ingawa wengi wanakwepa ukweli huu lakini ni kweli kabisa kuwa, kila mmoja huwa na chaguo lake kichwani kabla ya kukutana na mhusika wake. Uliwaza nini kabla? Kuwa na mwanaume mweusi au mweupe?
Acha kubahatisha, hakikisha unayekuwa naye ni yule ambaye ulitamani kabla ya kukutana naye. Ukilazimisha kuwa na mtu ambaye unajua wazi kwamba moyo wako haujaridhika ni tatizo kubwa sana hapo baadaye.
Lazima awe na vigezo vile muhimu ambavyo kweli unavihitaji kutoka kwa mwenzi wa maisha yako. Kumbuka kwamba, ukishaingia kwenye ndoa si rahisi kutoka. Utakuwa naye siku zote za maisha yako.
Je, itakuwaje utakapoanza kuhisi upungufu wake au kutamani wengine nje ya ndoa yako, wakati tayari umeshaingia ndani? Tafakari hili kwa makini.

CHAGUO LA NDANI
Siri ya pendo la dhati lipo ndani ya moyo wa mhusika. Lazima moyo wako ukiri kwamba aliye mbele yako unavutiwa naye kwa kila kitu. Hutakiwi kuwa na ukakasi wowote moyoni mwako. Maana kuna wengine utamsikia akisema: “Ni mzuri lakini siyo sana...sijapenda kabisa matege yake, lakini si vibaya maana ana macho mazuri, sema hana shepu kali sana...nitaoa hivyo hivyo, marafiki zangu wote wameshaoa nimebaki mimi.”
Huu ni mtazamo hasi rafiki zangu. Kabla ya kuamua kuingia kwenye ndoa, lazima moyo wako uridhie na ukupe kibali rasmi kwamba, sasa NENDA KWAKE, MAANA HUYO NDIYE NILIYERIDHIKA NAYE! Hapo sasa unaweza kupiga hatua moja mbele na kuamua bila kuwa na shaka yoyote kwamba huyo ndiye.

ANA KASORO GANI?
Hakuna aliyekamilika chini ya jua, lakini kuna wengine kasoro zao zinavuka mipaka. Ni kweli ni vyema kujifunza kusamehe lakini kuna maeneo mengine ni magumu zaidi kuweza kusameheka kwa urahisi.
Mfano umemfumania mpenzi wako zaidi ya mara tatu, hutakiwi kuendelea kung’ang’ania kwamba unampenda na unataka kuingia naye kwenye ndoa. Uchumba tu umemfumania mara tatu, mkioana si ndiyo ataingia na mpenzi wake hadi chumbani kabisa?
Hakuna sababu ya kukimbilia ndoa marafiki zangu, lakini jambo la msingi ni kujua unakwenda kwenye ndoa na nani. Bado kuna mambo mengi zaidi ya kujifunza ndugu zangu, lakini ufinyu wa nafasi unanifanya nikomee hapa kwa leo. Wiki ijayo si ya kukosa.

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.

No comments: