Calvin Kiwia
BEKI, Mbuyu Twite kuzomewa na kuitwa mwizi na mashabiki wa Simba na Kocha Saintfiet kutishia kuondoa timu uwanjani, ni miongoni mwa matukio yaliyotawala mchezo wa kirafiki kati ya Yanga na Coastal Union kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana.
Katika mchezo huo uliokwisha kwa Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, Twite alijikuta kwenye wakati mgumu kutokana na kuzomewa na kubezwa na maneno machafu kutoka kwa mashabiki wa Simba.
Hata hivyo, Twite aliyeonyesha kiwango kizuri na kushangiliwa na mashabiki wa Yanga na hata kocha wake kumpongeza, muda wote alicheza kwa kujiamini na kubeza kelele za mashabiki wa Simba kwa kubusu jezi ya Yanga kila kelele dhidi yake ziliposikika.
Twite aliziingiza kwenye mzozo na malumbano klabu za Simba na Yanga baada ya awali kusaini kwa Wekundu hao wa Msimbazi na kisha kuachana nao na kutua Jangwani.
Aidha, mechi hiyo nusura iingie dosari baada ya kocha wa Yanga Saintfiet kuamua kuitoa uwanjani timu yake kwa kile alicholalamika baada ya wapinzani wao Coastal Union kuchelewa kufika uwanjani wakati wao ndiyo walioomba mchezo huo.
Hata hivyo, jitihada za kumshawishi kocha kurudisha timu uwanjani zilizofanywa na Katibu Mkuu Celestine Mwesigwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Abdallah Bin Kleb zilifanikiwa na mchezo kuanza.
Katika mchezo huo, Coastal Union walikuwa wa kwanza kulifikia lango la Yanga dakika ya pili ya mchezo kwa shuti la Soud Mohamed kutulizwa mikononi mwa kipa Ally Mustapha.
Yanga ilijibu shambulizi hilo dakika tatu baadaye kwa shuti kali la beki Stephano Mwasika kushindwa kulenga lango na kwenda nje katika dakika ya 18.
Coastal walitawala sehemu ya katikati kwa kujaza viungo wanne, Jerry Santo, Seleman Selembe, Razack Khalfan na Soud Mohamed na hivyo kuwalazimu Yanga kupitisha mashambulizi kupitia pembeni.
Razack Khalfan alibadili matokeo ya mchezo kwa kufunga bao la kuongoza kwa Union baada ya shuti lake la umbali wa mita 27 kwenda moja kwa moja kwenye kamba za Yanga.
Kipindi cha pili, Kocha Saintfiet aliwapumzisha Oscar, Abdul, Mwasikwa na Kavumbagu na nafasi zao kuchukuliwa na Shamte Ally, Frank Domayo, Tegete na David Luhende.
Sehemu kubwa ya kipindi cha pili, Yanga walipiga kambi ya mashambulizi langoni mwa Coastal na kukosa mabao kupitia kwa Msuva, Kavumbagu katika dakika za 46 na 55, huku shuti la Joshua likigonga mwamba dakika ya 69.
Mchezo mbaya wa kiungo Santo ambaye awali alishaonywa kwa kadi ya njano na mwamuzi, Hashim Abdallah ulimponza katika dakika ya 60 baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu kufuatia kumchezea vibaya Twite.
Kutoka kwa Santo kulionekana wazi na Yanga hawakusita kutumia faida hiyo kwa kufanya mashambulizi na kupata bao la kusawazisha Coastal wakijifunga wenyewe.
Bao hilo lilitokana na makosa ya beki Philipo Mutesela aliyejaribu kuicheza bila mafanikio krosi ya Shamte na kuishia kuupeleka mpira kwenye nyavu zake katika dakika ya 85.
Bahanunzi aliwaondoa mashabiki wa Yanga uwanjani wakiwa vifua mbele baada ya kufunga bao la ushindi dakika ya 88 kwa shuti kali akimalizia pasi ya kupenyeza aliyopewa na Domayo.
Saintfiet aliwapongeza wachezaji wake kwa ushindi huo na kusema, hawakucheza vizuri kipindi cha kwanza lakini waliimaliza nusu yote ya pili kwa kuonyesha kiwango kizuri, huku akimwagia sifa Twite kwa kucheza vizuri.
Kwa upande wake Kocha wa Coastal, Juma Mgunda alikubali matokeo na kusema anachokifanya kwa sasa ni kujenga timu.
Yanga: Ally Mustapha, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite, Saimon Msuva, Haruna Niyonzima, Didier Kavumbagu, Said Bahanunzi, Stephano Mwasika.
No comments:
Post a Comment