MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa amesema yuko tayari kufuta chama chochote ambacho kitakuwa na mwelekeo wa kuvuruga na kuvunja amani ya nchi kwa kukiuka sheria na taratibu.
Amesema sheria inampa mamlaka ya kuvifuta vyama vya siasa vinavyokiuka sheria na kwamba akiona kuna umuhimu huo, hatasita kufanya hivyo.
Akizungumza ofisini kwake Dar es Salaam jana, Tendwa alisema yuko tayari kufuta chama ambacho kinakwenda kinyume cha sheria kwa kuwa sheria na mamlaka ya kufanya hivyo anayo.
Msajili huyo alisema vyama vyote vya siasa vinatakiwa kuhakikisha vinafuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo ili kulinda amani, badala ya kuchochea chuki zisizo na msingi.
“Kwa hivi sasa kuna ujambazi wa kisiasa na inasikitisha sana haya mauaji ambayo yametokea kwa kipindi cha hivi karibuni na huko nyuma kwa sababu yamekuwa yakisababishwa na siasa, kinachotakiwa ni vyama kuheshimu sheria zilizopo,” alisema Tendwa.
Alisema tangu mfumo wa demokrasia ya vyama vingi uanzishwe, kwa mwaka jana mpaka hivi sasa kumekuwa na matukio mengi ya ghasia, yakiwamo ya mauaji ya raia na kuwa hata wakati wa uanzishwaji wa mfumo huo ulioanza miaka 20, haikuwa hivyo.
“Nina mwaka wa 12 tangu niwe hapa, lakini kuanzia mwaka jana matukio yamekuwa ni mengi sana ambayo yote yanasababishwa na hizi siasa, na kwa sasa tunasema hatutaki kuona tena mauaji yakiendelea, imetosha. Tutafuta chama chochote kiwe na wabunge au hakina wabunge,” alifafanua Msajili huyo.
Aidha, alielezea pia mauaji yaliyotokea Arusha, Singida, Morogoro na Iringa yakikihusisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwa ni mfano mbaya.
Alisema kama watu wataendelea kufa katika mikutano ya kisiasa, wananchi watakuwa na hofu ya kuhudhuria mikutano ya kisiasa katika siku zijazo.
Alivionya vyama vya siasa kuhusu kampeni zisizo na kikomo katika kusaka uhuru wa kidemokrasia, akisema kwamba wanapaswa kusubiri wakati mwafaka, na kwamba hayuko tayari kuona watu zaidi wanakufa kutokana na kutotii sheria kunakofanywa na viongozi wa kisiasa.
Hata hivyo alikataa kuzungumzia tukio la hivi karibuni la kuuawa kwa mwandishi wa habari wa Channel Ten mkoani Iringa, Daudi Mwangosi, akisema suala hilo bado liko katika uchunguzi.
“Tunapaswa kusubiri ripoti ya Tume iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, kuchunguza kifo hicho,” alisema Tendwa.
Alitoa mwito kwa vyama vyote vya siasa kufahamu kwamba vyama vyao vinaongozwa na sheria na kuendesha siasa zao kwa busara na kujizuia kuingia nchi katika machafuko.
CHANZO HABARI LEO
2 comments:
Nahisi kwamba itakuwa si busara na hivyo ni kutoitakia amani nchi yetu ya Tanzania kwa kufanya hivyo maana kama watanzania wanakerwa na udhalimu,wizi wa mali za umma, kutotendewa haki pale wanapodai haki yao, wakipata sehemu ya kuonyesha kutoridhika kwao kupitia chama chochote,ambacho hakitakuwa CCM ofcourse maana hao ndio washukiwa wa kwanza,watakuwa vyama vya upinzani.Msajili akisema anafuta chama hicho ni kama kumuona nyoka anaingia uvunguni mwa kitanda ukajifariji kwamba as long aonekani is ok kulalia kitanda. Tunapaswa kuelewa kwamba Tanzania ya myaka hiyo siyo sawa na ya myaka hii kwakumaanisha kizazi.Kizazi hiki hakikotayari kusubiri kama kile cha zamani.Maana cha zamani kilisubiri matokeo yake yanaonekana.hata kama ni watoto wako wakiwa hawasikii,utaishia kuwapiga tuu na siyo kuwauwa.Hau kuwariject kwamba siyo wanao.Ikumbukwe kipindi Mrema amekuja juu, baba wa taifa alisema,kukataza washabiki wasimshangilie au wasiandamane kumbeba ni kumuongezea umaarufu.Hizi ndizo busara tunazohitaji zitumike kwa wakuu wa vyombo vya dolla kwamba wakiona chadema,cuf,nccr,au hata ccm, polisi wasaidie tu kulinda mali za wananchi,usalama barbarani n.k si kuwapiga mabomu.unatumia siraha kwa watu wasiyo na siraha una wazimu?Kwa hiyo busara itumike siyo kufuta vyama maana vyama vinaweza kuwepo na kuleta vurugu vizuri pindi mtakuwa mmevifuta na havionekani na hamjui wanakutania wapi.
Wazo Lako in Zuri sana. Lakin kwanza unatakiwa ukifute CCM ndio chama kinachosababisha vurugu na fujo
Post a Comment