Na John Gagarini, Kibaha
CHAMA cha Waandishi wa Habari mkoa wa Pwani (CRPC) kimeitaka serikali kuitunza famailia ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten mkoani Iringa Bw Daud Mwangosi, anayedaiwa kuuwawa na askari.
Akizungumza mara baada ya maandamano yaliyofanywa na waandishi wa mkoa huo, jana mjini Kibaha mwenyekiti wa chama hicho Bw Masau Bwire alisema kuwa kwakuwa marehemu aliuwawa akiwa anatekeleza majukumu ya kuupasha umma kilichokuwa kikiendelea katika mkutano huo serikali inapaswa kuihudumia familia hiyo.
Bw Bwire alisema kuwa familia ya marehemu ilikuwa ikimtegemea hivyo ni vema serikali ikachukua jukumu hilo ili kuisaidia kwani kwa sasa hawatakuwa na uwezo wa kuendesha maisha yao hasa ikizingatiwa watoto wake wanahitaji kupata elimu, huduma nyingine za malezi na kibinaadamu.
“Tunataka serikali ibebe jukumu hilo kwa kuihudumia na kuitunza familia hiyo kwani kifo chake kilikuwa ni kibaya na alikufa akiwa chini ya askari ambao ni moja ya mihimila ya serikali inayotegemewa kutenda haki,” alisema Bw Bwire.
Alisema kuwa askari wote waliohusika wakamatwe na wasimamishwe kazi kupisha uchunguzi juu ya tukio hilo na wale watakaobainika kuhusika na mauaji hayo wafikishwe mahakamani ili kujibu tuhuma zitakazokuwa zinawakabili.
“Pia tunataka uongozi wa juu wa Jeshi la Polisi mkoani Iringa nao uwajibike endapo watabainika kushindwa kuzuia mauaji ya mwandishi huyo ambaye alikuwa akitekeleza majukumu yake na hata kama alivunja sheria alipaswa kukamatwa na kupelekwa kwenye vyombo vya sheria na si kuuwawa,” alisema Bw Bwire.
Aidha alisema kuwa wanataka kuwe na uchunguzi huru juu ya tukio hilo ili kuwawajibisha wale wote watakaobainika kutenda kosa hilo ambalo limeleta simanzi kubwa kwenye tasnia ya habari na wadau wake ambao wamehuzunishwa na tukio hilo.
Kwa upande wake Rais wa Umoja wa vyama vya waandishi wa habari Tanzania UTPC, Bw Keneth Simbaya alisema kuwa wanataka uchunguzi huo uwe na uwazi kwani tukio hilo lilikuwa wazi na watu waliona mwili huo ukiwa umeharibika vibaya.
Marehemu Mwangosi alifariki kwenye mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambao uliambatana na vurugu huko kwenye Kijiji cha Nyololo mkoani Iringa Septemba 2 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake