ANGALIA LIVE NEWS

Monday, September 17, 2012

Wajumbe Wa Baraza La WaWakilishi Waitembelea Tume Ya Katiba


Tume ya Mabadiliko ya Katiba imesisitiza umuhimu wa wadau mbalimbali wakiwemo wanasiasa, asasi za kiraia na kidini kuwaacha wananchi kutoa maoni yao binafsi kuhusu Katiba Mpya.
Akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar leo (Jumatatu, Septemba 17, 2012), Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Joseph Warioba alisema katika mikutano ya ukusanyaji wa maoni inayoendelea, na kukusisitiza kuwa makundi na taasisi mbalimbali vitapata nafasi ya kukutana na Tume na kutoa maoni yao.

Aidha Jaji Warioba alisema kuwa changamoto kubwa ambayo Tume hiyo inakabiliana nayo ni wananchi kupewa mawazo ya kuzungumza na watu wengine, jambo ambalo haliwasaidii wananchi .

“Makundi ya watu, Taasisi za kirai na hata vyama vya siasa vimekuwa mstari wa mbele kuwalisha wananchi mambo ya kuzungumza “ alisisitiza Jaji Warioba.

Mwenyekiti huyo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba aliwataka wawakilishi hao kuisaidia Tume kuwaelimisha wananchi kuwa tayari kutoa maoni yao ya moyoni na kukataa kabisa kupokea mawazo ya watu wengine ili katiba itakayopatikana iwe inawakilisha mawazo yao.



Jaji Warioba alikuwa akijibu swali la Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Ali Abdalla Ali ambaye alitaka kujua changamoto ambazo Tume inakutana nazo katika utekelezaji wa majukumu yake.

Jaji Warioba amesisitiza kuwa viongozi wa makundi mbalimbali na vyama vya siasa wana wajibu wa kuwaelimisha wananchi kutoa maoni yao binafsi badala ya kuwaelekeza aina ya maoni wanayopaswa kuyatoa.

Akizungumzia kuhusu muda uliopangwa katika kutekeleza kazi hiyo, Jaji Warioba alieleza kuwa pamoja na changamoto hiyo lakini Tume imejipanga kumaliza kazi yake ndani ya muda iliopewa kisheria.

“Tume imejipanga kuhakikisha ifikapo April 26 2014 katiba mpya inakuwa tayari. Kimsingi mazingira ya hali ya kisiasa nchini yanalazimisha kuwepo na katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ili kuweka maelewano ya kitaifa” alifafanua.

Wajumbe hao wa Baraza la Wawakilishi wapo katika ziara ya taasisi mbalimbali za Muungano zilizopo Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Ali Abdallah Ali amesema Wajumbe wa Kamati watatumia uzoefu na elimu waliyoipata katika ziara yao ili kuisaidia Tume kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Wajumbe hao walipata nafasi ya kutembelea vitengo vya Utafiti na Taarifa Rasmi (Hansard) ambapo waliweza kuona jinsi maoni yanavyopokelewa na na kufanyiwa kazi .

Ismail Ngayonga,

Information officer,
Constitutional Review Commission (Tanzania),
PO Box 1681,
Dar es Salaam,
Tel: +255 (0) 22 2133425,
Fax: +255 (0) 22 2133442,
Mobile: +255 (0) 717 084252
Email: ngayongaismail@yahoo.com,
Website: www.katiba.go.tz

No comments: