Gari la Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) aina ya Isuzu
Pick-Up, likiwa eneo la ajali katika kijiji cha Kirinjiko wilayani Same
mkoani Kilimanjaro jana, baada ya kugongana na lori la mizigo ambapo
watu watatu walifariki dunia papo hapo akiwamo dereva wa gari hilo,
Robert Huho (picha ndogo). Picha na Daniel Mjema
WATU watatu wamefariki dunia papo hapo akiwamo dereva wa gari la
magazeti la kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), kugongana
na lori la mizigo aina ya Scania.
Ajali hiyo mbaya ilitokea jana
saa 11:00 alfajiri katika eneo la Kirinjiko nje kidogo ya mji wa Same,
baada ya gari la MCL Isuzu namba T336 BFU kugongana na Scania namba T415
AAM.
Taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari jana na kamanda
wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Robert Boaz ilisema gari hilo la MCL
lilikuwa likiendeshwa na dereva Wambura Ramadhan.
Gari hilo la
MCL lilikuwa likitokea Jijini Dar Es Salaam kwenda Arusha kupitia Moshi
wakati Lori hilo la Scania likiwa na Tela namba 411 AAM nalo lilikuwa
likitokea Jijini Dar Es Salaam.
Kamanda Boaz aliwataja
waliofariki kuwa ni dereva wa MCL Robert Huho, Ibrahim Mrutu (65) na
Abdalah Rajab (49) wote wakiwa ni madereva wa kampuni ya Simba Truck ya
Arusha.
Kwa mujibu wa kamanda Boaz, watu wote watatu waliofariki
dunia pamoja na majeruhi walikuwa katika gari dogo wakiwa wamepakia
nyuma pamoja na shehena ya magazeti.
Waliojeruhiwa katika ajali
hiyo ambao walifikishwa Hospitali ya Wilaya ya Same na kuhamishiwa KCMC
ni Agustino Nguma, Hamza Omary na Mtero Mussa au Simon Lusekelo.
Majeruhi
wengine wawili walitibiwa na kuruhusiwa ambapo Mtero aliyekutwa
hospitali ya Same kabla ya kuhamishiwa KCMC alisema alikuwa hafahamu kwa
nini yuko hospitali.
“Ninachokumbuka ni kwamba nilipanda gari la
Mwananchi pale Dar es Salaam saa 6:00 usiku kwenda Arusha lakini
nashangaa kwanini niko hospitali…kumetokea nini?” alihoji.
Hata
hivyo taarifa zaidi zilizopatikana eneo la tukio zilisema gari la MCL
lililigonga kwa nyuma lori hilo likiwa limesimama barabarani bila kuwapo
alama zozote kama limeharibika.
Dereva wa lori hilo ambaye
alikataa kujitambusha kwa gazeti hili alikanusha akisema gari lake
lilikuwa likitembea lakini mashuhuda waliokutwa eneo la ajali wasisitiza
lilikuwa limesimama.
Sheria za usalama barabarani zinataka gari
linaloharibika na kusimama barabarani lazima liweke alama maalumu
zinazong’aa (reflectors) lakini lori hilo halikuwa nazo.
Wakati
Kamanda Boaz akisema gari hilo la MCL lilikuwa likiendeshwa na dereva
Wambura, dereva huyo alikanusha madai hayo akisema gari hilo lilikuwa
likiendeshwa na marehemu.
“Nimewaambia Polisi japokuwa
mimi ni dereva wa Mwananchi lakini wakati wa ajali sikuwa naendesha mimi
lakini bado wanashinikiza kuwa mimi ndiye nilikuwa naendesha,” alisema.
Kwa
kawaida magari ya safari ndefu ya MCL huwa na madereva wawili wa
kusaidiana na siku hiyo, mtumishi mwingine wa MCL, Rahib Bakari alikuwa
ameomba lifti akielekea Mwanga.
Wambura alisema aliendesha gari
hilo kutokea jijini Dar es Salaam hadi katikati ya Mombo na Hedaru
ambapo alibadilishana na marehemu ili amalizie umbali uliokuwa umebakia.
Sababu
nyingine inayowafanya polisi waamini kuwa Wambura ndiye aliyekuwa
akiendesha gari hilo ni kitendo cha kutoka salama wakati eneo la kiti
cha abiria ndilo limeharibika zaidi.
“Pale mbele nilikuwa nimekaa
mimi, Mangi (Rahib) na marehemu ndio alikuwa akiendesha na baada ya
kile kishindo tu aliruka kwenye gari kwa kiwewe na kuumia zaidi,”
alisema Wambura.
Polisi wamemweka mahabusu dereva huyo wa MCL kwa
madai ya kuendelea na uchunguzi zaidi huku wakishikilia msimamo kuwa
Wambura ndiye alikuwa akiendesha gari hilo.
No comments:
Post a Comment