ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, October 27, 2012

Dk Slaa amlipua JK


Mwandishi Wetu, Tabora
KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amemlipua Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akidai kuwa hana ubavu wa kupambana na rushwa kwa kuwa chama chake kiliingia madarakani kwa rushwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.

Akihutubia katika mikutano ya hadhara katika Vijiji vya Kata za Kiloleli na Ipole, wilayani Sikonge, Mkoa wa Tabora, Dk Slaa alisema rushwa inazidi kukua siku hadi siku nchini.

Alidai kwa kuwa viongozi wa CCM waliingia madarakani kwa njia ya rushwa ndiyo maana hawawezi kulimaliza tatizo hilo.

Dk Slaa alisema Rais Kikwete anatania kuhusu tatizo la rushwa kwa kuzungumza tu majukwaani, huku akiwalinda washirika wake.



Alisema kama Rais Kikwete angekuwa mkweli angewakamata wamiliki wa Kampuni ya Kagoda ambao ni watuhumiwa wa wizi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (Epa) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Alidai kuwa ameshindwa kuwakamata kwa sababu fedha hizo ndizo zilitumika kumwingiza madarakani katika uchaguzi wa 2005.

Katibu mkuu huyo wa Chadema alisema vitendo vya rushwa vilivyojitokeza katika uchaguzi wa viongozi wa CCM ni kielelezo tosha kwamba, chama hicho hakina uwezo tena wa kupambana na rushwa.

"Tunawaambia CCM kuwa chama chao kimeoza kuanzia juu hadi chini, sasa mafisadi wameshika hatamu ndani ya chama hicho,” alisema.

Dk Slaa alisema, “Hivi Watanzania tunahitaji ushahidi wa namna gani ili kubaini uozo katika CCM na tuungane kukiondoa madarakani.”

Aliongeza, "Wakati chama hicho kinatopea kwenye lindi la rushwa na ufisadi, kiongozi wake mkuu ambaye Rais Kikwete naye anaishia kulalamika tu.”

Slaa alisema Rais Kikwete angekuwa na nia ya dhati
katika kupambana na rushwa, angeifanyia kazi orodha ya majina 11 ya watuhumiwa wakubwa wa ufisadi iliyotolewa katika Viwanja Mwembeyanga, jijini Dar es Salaam Septemba 2007.

Alisema kuendelea kulalamikia kuhusu rushwa bila kuchukua hatua yoyote, kunawashangaza wananchi ambao wanaona hata Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) bora ingevunjwa.

Hatuwezi kukubali taifa liangamie kwa sababu Rais anashindwa kuchukua hatua dhidi ya mafisadi na wala rushwa.

Rais Kikwete

Hivi karibuni Rais Kikwete wakati akifungua Mkutano Mkuu wa UVCCM mjini Dodoma aliwaasa vijana wa chama hicho kutojihusisha na rushwa hatua ambayo inaonekana sawa na kumpigia mbuzi gitaa.

Katika hotuba yake, Kikwete aliwaambia 'watajuta', ikiwa watachagua viongozi kwa misingi ya rushwa.

“Nawaambieni, mkifanya mchezo ipo siku mtakuja kujuta maana mkishamchagua kiongozi asiyefaa, mtalazimika kuwa naye huyohuyo hadi 2017, na kama Waswahili wanavyosema majuto ni mjukuu,” alisema Kikwete.

Kauli hiyo ya Kikwete ni kama aliyoitoa wakati akiahirisha Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Wanawake ya chama hicho (UWT)aliposema kuwa, CCM kinakwenda kubaya kutokana na chaguzi zake kugubikwa na vitendo vya rushwa.

Kikwete alisema siku zilizopita vitendo hivyo vilikuwa vikihusishwa zaidi na wanaume, lakini akaeleza kushangazwa kwake na makundi ya kina mama nao kuanza kujihusisha na rushwa.

Msekwa alonga

Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Pius Msekwa amezidi kuwasha moto ndani ya chama hicho, baada ya kuvitaka vyombo vya dola kuwachukulia hatua za kisheria wote waliotuhumiwa na rushwa katika uchaguzi wa ndani wa chama hicho.

Kauli ya Msekwa imekuja ikiwa ni siku tatu baada ya kuwapo kwa tuhuma za rushwa kutawala ndani ya uchaguzi wa Jumuiya ya  Umoja wa Vijana( UVCCM) na ule wa Jumuiya ya Wanawake (UWT) zilizomalizika mjini Dodoma.

Hata hivyo, kauli ya Msekwa inapingana na mawazo ya makada wengi wa chama hicho wanaopinga rushwa wakisema kuwa, uongozi wa chama unapaswa kuonyesha kwa vitendo dhamira ya kweli ya kukiokoa chama hicho ambacho hata Mwenyikiti wake, Rais Jakaya Kikwete alisema; “Rushwa inatupeleka kubaya.”

Matokeo ya uchaguzi wa UVCCM ndiyo yaliyozua tafrani kubwa kiasi cha baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu wa jumuiya hiyo, kumsindikiza kwa mabango Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein baada ya kufunga mkutano huo.

Mabango hayo yaliyokuwa na ujumbe wa kulalamikia mchakato wa uchaguzi kwamba ulitawaliwa na rushwa, yalitanguliwa na kauli za walalamikaji ambao tayari walikuwa wamewaambia waandishi wa habari kuwa wanamwomba Rais Kikwete atengue matokeo hayo, ikiwezekana katika muda wa saa 24.

Akizungumza jana asubuhi jijini Dar es Salaam, Msekwa alisema; "Kwanza nataka kusema, wote wenye malalamiko walitakiwa kuyapeleka kwenye ngazi husika, nimesikitishwa na hao ambao wamempa Rais saa 24 kufuta matokeo ya uchaguzi”.

"Hizi ni fujo tu, wapi kuna mamlaka inayomwamuru Rais au mwenyekiti kufanya hivyo, wanatakiwa kufuata taratibu na kanuni za uchaguzi... Hivi ni kifungu gani cha sheria kinachosema hivyo?," alihoji Msekwa.

Msekwa ambaye alikuwa akihojiwa na Kituo cha Radio One jana alisema kuwa kuna kanuni na taratibu mbalimbali za kuwasilisha malalamiko, ndipo hoja zinaweza kusikilizwa na kupata mafanikio.

Akizungumzia suala la rushwa ndani ya uchaguzi, alisema ni tatizo lililosambaa kwenye jamii na ni kasoro na upungufu uliokuwa sugu.

"Rushwa imesambaa kila mahali, polisi kuna rushwa, mahakamani rushwa, lazima tukemee, nimewahi kuzungumzia hili la rushwa kuwa ni kosa la jinai, lakini bado nasema kukemea haitoshi.

Waaswa kukataa mizigo mizito

Naye Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Tabora, Kansa Mbarouk akiwaambia wananchi wa kata hizo kwamba ugumu wa maisha unaowakabili unatoka na sera mbaya ya chama tawala.

Mbarook alisema CCM ya Mwalimu Julius Nyerere iliyokuwa ikishughulikia matatizo ya watu sasa haipo tena, badala yake wameichukua mafisadi.

Alisema chama hicho sasa kimebaki kuwa adui wa kuminya haki za raia.

"Miaka mingi sisi tumewabeba, tena wanatumia maneno yaleyale ya ‘Mzigo mzito mpatie Mnyamwezi akubebee’. Kwa hiyo Watanzania wa Tabora kwa muda mrefu tumekuwa tukiibeba CCM wakati wenzetu mikoa mingine wameshaikataa.
Aliongeza, Sasa ni wakati mwafaka kuanza kuutua huu mzigo, umetuchosha,” alisema huku akimpigia debe mgombea wa Chadema, David William katika kinyanganyiro cha udiwani kwenye uchaguzi mdogo utakaofanyika kesho katika eneo hilo

No comments: