JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limewataka wananchi kuepuka vurugu zinazohatarisha usalama, na kulinda amani iliyopo nchini
JWTZ imetoa kauli hiyo siku moja baada ya waumini wa dini ya Kiislamu jijini Dar es Salaam kuandamana sababu ya malalamiko kadhaa kama kukamatwa kwa Sheikh Issa Ponda na wafuasi wake 49 wiki iliyopita kwa tuhuma mbalimbali, kutoweka kwa kiongozi wa UAMSHO Sheikh Amir Farid Hadi, na malalamiko mengine.
Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe, amesema hatua ya wanajeshi kujitokeza katika kuzima vurugu zilizotokea jijini juzi, ilikua na lengo la kuwaonyesha wananchi kwamba JWTZ ipo kikazi zaidi, na anayetaka vurugu atashughulikiwa kisheria.
“Juzi tulionyesha ‘talent show force’ ili watujue kama tupo kazini, hata kama wametuona tupo kimya, hatuna mzaha katika kulinda na kusimamia ulinzi na usalama wa taifa hili, kwa hiyo tulikuwa kwenye sehemu ya utekelezaji wa majukumu yetu, na kwamba atakayekwenda kinyume tutamshughulikia,” alisema Mgawe.
Alisema zoezi hilo litaendelea kwa maandamano yoyote yatakayoonyesha dalili za kuhatarisha usalama wa nchi. Aliongeza kwamba wanajeshi watashiriki kikamilifu ili kuhakikisha kuwa wananchi wanafuata sheria na taratibu zilizopangwa, bila ya kuathiri usalama wa nchi.
Alisema kwa sasa wanasubiri kibali cha polisi cha kuhusu kuhitaji msaada ili waweze kuungana nao katika kushughulikia maandamano yenye lengo la kuhatarisha amani na utulivu.
“Tunawataka wananchi kufuata sheria na taratibu zilizopo na kuepuka kuhatarisha amani ya nchi, kama wanataka tuingie kazini tutafanya hivyo, ila tunachowaasa ni kufuata taratibu zilizopo,” alisisitiza.
Katika vurugu za juzi, watu 53 walitiwa mbaroni kwa tuhuma za kushiriki kwenye maandamano.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, watu hao watafikishwa mahakamani Oktoba 22 mwaka huu. Source: Mdimuz blog
No comments:
Post a Comment