ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 4, 2012

Kikwete kumzika Kardinali Rugambwa

Raginald Miruko, Bukoba
RAIS Jakaya Kikwete keshokutwa anatarajiwa kuongoza maelfu ya waumini wa Kanisa Katoliki katika kuhamisha masalia ya mwili wa Mwadhama Laurean Rugambwa kutoka Kanisa la Kashozi na kuzikwa rasmi katika Kanisa Kuu mjini Bukoba.

Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Mhashamu Methodius Kilaini amelieleza Mwananchi kuwa, mbali na kiongozi huyo wa nchi, wamealikwa viongozi wengine wa kitaifa na kidini kutoka ndani ya nje ya nchi.

“Watu watakuwa wengi, tumemwalika Rais Kikwete, Kardinali Pengo, mawaziri, maaskofu wote wa Tanzania na wengine kutoka kwa majirani zetu Uganda na Burundi,” alisema Askofu Kilaini katika mahojiano maalumu.

Siku moja baada ya mazishi hayo, itafanyika shughuli ya  kubariki upya Kanisa Kuu la jimbo hilo baada ya kukamilika ukaratabati wake wa miaka 17, ulioanza mwaka 1995.


Matukio hayo mawili yatakwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Marehemu Rugambwa Julai 12, 1912. 

Kuhamisha mwili Rugambwa ambaye alikuwa Kardinali wa kwanza Mwafrika aliyefariki dunia Desemba 8, 1997 na mwili wake kuhifadhiwa katika Kanisa la kwanza la Katoliki mkoani Kagera, Kashozi, kunatokana na kauli yake ya  kuzikwa katika Kanisa Kuu la Bukoba alilochagua yeye.

Askofu Kilaini, alisema shughuli ya kuhamisha mwili huo kutoka katika Kanisa la Kashozi itafanywa na watalaamu wa afya walioandaliwa na kuwekwa katika jeneza jipya kwa ajili ya mazishi rasmi.

Paroko wa Parokia ya Kashozi, Padri Anthony Rugundiza alisema jana kuwa wageni wanaopeleka jeneza kutoka Dar es Salaam wanatarajiwa kuwasili Bukoba leo na baada ya hapo maandalizi ya mwili huyo yataanza.

Kaburi la muda la Kardinali Rugambwa limekuwa likitumiwa kama sehemu ya utalii na waumini kufanya maombi na mafungo, na tangu azikwe miaka 15 iliyopita hadi jana maelfu ya watu walikuwa wamekwishalitembelea.

“Si rahisi kujua idadi ya waliotembelea, lakini ni wengi kwa maelfu. Wengine wamekuwa wakifanya maombi yao na wengine wameandika hata barua zenye ujumbe wa mambo wanayotaka Rugambwa  awaombee kwa Mungu,”
alisema Padri Rugundiza.

Padri Rugundiza alisema wamekwishafungua kaburi hilo kufanya usafi na lile jeneza la awali bado lina hali nzuri, lakini wameamua kutolitumia kwa mazishi rasmi.

Mwananchi

No comments: