ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 17, 2012

KULAZIMISHA MAPENZI NI KUJIDHALILISHA

KAMA ada tumekutana tena machache, ili dunia ikamilike aliletwa mwanamke kuipamba na kuwa liwazo la mwenzake, japo kuna wanawake hawajui hilo na kuwa chanzo cha mateso ya wenza wao.
Leo nimekuja na mada moja kutokana na kupata malalamiko kutoka kwa msomaji wangu mmoja kuwa, kuna binti alimpigia simu na kusema anampenda na anataka awe mpenzi wake, lakini bwana yule alimjibu kistaarabu kuwa hawezi kuwa mpenzi wake kwa vile yupo ndani ya uhusiano wa ndoa.
Lakini yule msichana amekuwa akimsumbua sana kila siku kwa meseji za kuendelea kumtaka, ingawa amekuwa akimueleza kuwa hawezi kuongeza mpenzi mwingine zaidi ya mkewe.
Binti yule amekuwa akimtumia zaidi ya meseji 100 za mapenzi kila siku kuonyesha hisia zake za kimapenzi huku akimbembeleza jamaa amkubali ili awe mpenzi wake kwa vile hakuna mtu mwingine chini ya jua aliyemuona anamfaa kama yeye.
Kila anapomueleza kuwa haiwezekani, yeye hasikii na anazidi kumtumia ujumbe wa mapenzi hata akiwa nyumbani, kitu ambacho anakiona kama kitamharibia nyumba yake.
Baada ya kunieleza yale na kuomba ushauri, nilifanya hivyo lakini niliona kuna umuhimu wa kuwaeleza watu wote wenye tabia ya kulazimisha mapenzi, wasifanye hivyo.
Sizungumzii wanawake tu, bali hata wanaume wengi wamekuwa na tabia hiyo, hata kama mwanamke ni mke wa mtu, kwa vile kapata namba yake humsumbua bila kuangalia yupo sehemu gani, pia yupo tayari hata kumvunjia ndoa yake.
Tabia hizo zimekuwa kero kwa watu wengi. Siku zote mapenzi ni ridhaa ya watu wawili waliokubaliana kwa hiyari yao bila kulazimishana na si lazima unayempenda akukubalie.
Hakuna watu wanaopendana kwa pamoja, kuna mtu ataanza na kupeleka maombi kwa mwenzake ambaye naye atayaangalia yale maombi, kwa kujiuliza kama mtu aliyemtaka anakubalika moyoni mwake.
Tumewaona wengi wakiomba kupewa muda ili kuzungumza na mioyo yao kama ipo tayari kupokea au kukataa maombi.
Kama ipo tayari kukupokea, jibu huwa ndiyo, lakini kama haipo tayari jibu lake huwa siyo. Hapa ndipo penye tatizo, wengi wanapotamkiwa hawatakiwi huwa hawakubali na huanza kulazimisha mapenzi na kusababisha karaha kwa mwingine.
Hata kama mtu unampenda kuliko kitu chochote, ombi lako linapokataliwa, unatakiwa kukubaliana na kilichotokea. Watu wa aina hii huwa hawajiamini, wana jicho fupi na wavivu kuisumbua akili yao kwa kuona kitu kimoja na kukichukulia ndiyo kila kitu katika maisha yao.
Ikitokea bahati mbaya hukukubaliwa, kubaliana na hali halisi ili kumpa uhuru uliyemtaka kufanya uamuzi wake bila kulazimishwa.
Penzi la kweli huwa halilazimishwi na si kila unachokipenda utakipata, kama umekosa endelea kutafuta kwa vile dunia hii kila kukicha wanazaliwa wazuri kuliko waliopita. Acha uvivu wa fikra wa kutoisumbua akili yako, badala yake unang’ang’ania kitu ambacho hakikutaki.
Kulazimisha mapenzi ni sawa na kuchanganya maji na mafuta, siku zote havikai pamoja. Hebu thamini utu wako, wewe si mtu wa nyongeza ambaye huna thamani tena.
Thamani yako ni kubwa, acha kujidhalilisha kwa kulazimisha mapenzi. Mbegu ya penzi humea kwenye udongo wenye rutuba ya mapenzi, kulazimisha mapenzi ni sawa na kupanda mbegu yako kwenye mawe, pia kutafuta mateso ya kujitakia.
Hebu jiheshimu, jithamini, acha ulimbukeni, mtu kakuambia ana mpenzi basi hebu jenga heshima.
Hakuna mtu anayeweza kumkubali mwendawazimu kama wewe, kwa vile mwenye akili timamu hawezi kulazimisha mapenzi, akielezwa huelewa.
Jiheshimu utaheshimiwa, ukijidharaulisha hakuna mtu atakayekuheshimu.
Tukutane wiki ijayo.

No comments: