ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 16, 2012

Kwenye mapenzi kuna virusi, unapaswa kujua ‘kuskani na kudeliti’-5


WIKI iliyopita wakati nahitimisha kirusi cha tatu ambacho ni “Wivu”, nilieleza kwamba inapotokea mizunguko yako ya kikazi, inakutaka ukaribiane na watu mbalimbali bila kujali jinsia zao. Mwenzi wako haelewi kuhusu hilo, matokeo yake anakuwa kikwazo kikubwa kwenye utendaji wako. Ukipigiwa simu ya kazi, yeye anawaza ni mapenzi. Huyo bila shaka anakuharibia.
Kwa faida ya maisha yako unatakiwa kumwepuka mapema mpenzi anayekuonea wivu mpaka anakwamisha shughuli zako. Mpenzi bora ni yule anayekupa wepesi wa kutimiza majukumu yako ya kila siku. Haiwezekani akawa anakudidimiza.

KIRUSI NO. 4, UAMUZI WA JAZBA
Hapa naona ni busara kwanza kufafanua kuwa wakati mwingine Mungu anataka tukutane na watu ambao siyo sahihi kwanza ili tukikutana wa watu sahihi, tujue jinsi ya kuwatunza, kuwathamini na kujivuna kuwa nao.

Unaweza kuwa na mwenzi bora lakini usigundue, ukamfanyia vitimbi. Wengine hutambua kwamba mume au mke wake alikuwa bora mpaka pale watakapoachana. Hivyo basi, ukishayaona kwa mtu ambaye siyo sahihi, siku ukimpata anayekidhi matakwa ya moyo wako, lazima utajivunia zawadi uliyopewa na Mungu.
Mara nyingi hutokea unakutana na mtu ambaye anamaanisha mno kwako lakini kutokana na historia yako ya kuumizwa huko nyuma, ukawa humuamini, kwa hiyo ukamuacha na yeye aende. Hupaswi kuwa na uamuzi wa jazba kwenye mapenzi. Tafakari, fanya uchunguzi halafu uitafakari kwa kina ripoti ya uchunguzi wako kabla ya kuamua.
Uamuzi wa jazba, kukimbilia kuacha ni aina nyingine ya kirusi. Hapo sasa kirusi kinaweza kuwa wewe mwenyewe. Unatakiwa kujiangalia kwa makini mno. Pima kiwango chako cha hasira na tukio lenyewe halafu jikosoe. Jitahidi kupiga moyo konde mara nyingi iwezekanavyo.
Penda sana kujirudi, uamuzi wa kuacha uje baada ya kujiridhisha kwamba hakika mwenzi wako uliyenaye hawezi kukidhi viwango vya moyo wako. Uwe umejitahidi kumkosoa na kumsahihisha mara kadhaa. Ukiwa na tabia ya kuacha na kukimbilia kuanzisha uhusiano mpya, maana yake wewe ni kirusi.
Ni kweli kuwa mlango wa furaha unapofungwa, mwingine hufunguliwa lakini mara nyingi huwa hatujui thamani ya kitu tunachopata au tulichonacho mpaka pale tunapokipoteza. Sasa usifike huko, fanya upembuzi na uchambuzi wa kina. Heri kumsahihisha leo kwa udhaifu wake mdogo ili baadaye akupe furaha kamili na ya kudumu, kuliko kumuacha kisha ujute kwa miaka mingi wakati akiwa ameshakupa kisogo.
Naendelea kukubali kuwa kumpa mtu mapenzi yako yote haimaanishi naye atakupa au kukurejeshea kwa kiwango kilekile ambacho wewe umekitoa. Zingatia kwamba umeamua kupenda, usipende kwa matarajio ya kwamba naye atakupenda na kukujali kwa kiwango unachokiwaza.
Timiza wajibu wako, ukiona hakupi unachotaka tambua kwamba unayo nafasi ya kumuelewesha kile ambacho anatakiwa kukifanya ili ufurahie mapenzi yake. Fanya kazi nzuri kila siku, tambua ya kwamba wanaofanikiwa katika maisha ya kimapenzi ambao leo wanajisema wanakula bata ni wale walioamini katika kufundisha.
Itaendelea wiki ijayo.

www.globalpublishers.info

No comments: