ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 17, 2012

Wafanyabiashara amlalamikia Waziri Kagasheki

Mwandishi Wetu, Karatu
MFANYABIASHARA Ally Said mkazi wa Karatu mkoani Arusha, amemuomba Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Hamis Kagasheki kumsaidia kurejeshewa gari lake ambalo hufanya biashara ya taxi mjini Karatu, baada ya kukamatwa kwa tuhuma za kubeba watu wanatuhumiwa kufanya ujangili.

Katika barua ya Said kwenda kwa Waziri kagasheki, mfanyabiashara huyo alisema gari lake hilo, ambalo linashikiliwa na askari wa Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro tangu Agosti, dereva wake Joseph Lulu alikamatwa baada ya kuitwa kuwachukua abiria wanne katika eneo la Oldian nje kidogo ya mji wa Karatu.

"Sasa mimi sitaki kuingilia kesi hii, ila ninaomba kurejeshewa gari wakati uchunguzi wa tuhuma unaendelea kwani gari hili ndilo nategemea kwa maisha yangu na familia yangu. Kwa miezi miwili nimehangaika bila mafanikio," alisema Said.

Awali, Lulu alisema  Agosti 4 mwaka huu, akiwa katika kazi yake ya udereva wa taxi  alipigiwa simu na watu waliokuwa katika eneo la Odiani nje kidogo ya Karatu, ili awafuate.

Alisema baada ya kufika aliwakuta watu hao, Oleteyetu Laizer, Saitabau Lomayan, Bilali Athuman na Assanal Mushi ambao aliwabeba na kuanza kuwarejesha Karatu mjini.

Lulu alisema akiwa njiani ndipo alikamatwa na polisi ambao waliomba kupekua gari na walifanya hivyo na hawakukuta kitu na ndipo waliwapeleka polisi.

"Baada ya kufikishwa  polisi  watu wengine watatu walikamatwa na tuliunganishwa nao tukidaiwa ni majangili," alisema Lulu.

Alisema  watu hao walitambuliwa kuwa ni Michael Manday, George Malkiadi na Elikana Moses na  wote baadaye walifunguliwa kesi  namba 24 mwaka huu, ya kukamatwa  kwa pamoja kwa kosa la kuuwa Tembo wanne, wenye thamani ya Sh23.5 milioni.

"Mimi sihusiki na tukio hili, ndio sababu tunaomba uchunguzi ufanyike ili haki ipatikane mapema," alisema Lulu.

No comments: