ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 3, 2012

Mkutano na Waandishi NIDA Zanzibar

MKURUGENZI wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa NIDA.Vuai M. Suleiman (kati), akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vilioko Zanzibar kuhusiana na kuaza kwa Uandikishaji Vitambulisho vya Taifa kwa Wananchi wa Zanzibar wiki ijayo, mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Walemavu Welesi Zanzibar.kulia mwenyekiti wa mkutano huo Salma Said na kushoto Ofisa wa Vitambulisho NIDA Abdalla Mmanga. 
Juu na chini ni WAANDISHI wa habari wakiwa katika mkutano huo wa NIDA kuhusiana na uandikishaji wa Vitambulisho vya Taifa Zanzibar
Salma Said, Zanzibar

MAMLAKA ya vitambulisho vya taifa Tanzania (NIDA) inaaza rasmi kusajili na kutoa vitambulisho hivyo kwa wazanzibari Octoba 15 mwaka huu.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa vitambulisho hivyo, Vuai Mussa Suleiman wakati akizungumza na waandishi wa habari katika katika ukumbi wa watu wenye ulamavu welesi Kikwajuni ikiwa ni sehemu ya kujitayarisha na kazi hiyo.

Akizungumzia faida za vitambulisho hivyo, Mkurugenzi alisema vina faida kubwa kwa wananchi na hivyo kuwasisitiza wanadishi wa habari kusaidia serikali zote mbili ili kutoa elimu kwa umma ili kazi hiyo ifanikiwe.

Alisema kazi hiyo imeanza kwa watumishi wa umma kusajiliwa na baadae na baadae kwenda kusajili katika kila wilaya ambapo kila wilaya imepangiwa siku 10 kwa ajili ya usajili wa vitambulisho hivyo.

Akizungumzia utaratibu wa utoaji wa vitambulisho hivyo, Mkurugenzi alisema vitatolewa kwa makundi matatu, wananchi ambao ni raia, wageni na wakimbizi.


Aidha katika wazanzibari wanaoishi nje ya nchi Vuai alisema watakaporejea nyumbani wataweza kusajiliwa na kupewa vitambulisho vya Mtanzania huku akikanusha vitambulisho hivyo kutotumika kisiasa.

“Vitambulisho havitatumika kisiasa kabisa kwa hivyo kwa wale watanzania waliopo nje ya nchi watakaporudi nyumbani watasajiliwa na kupewa vitambulisho vyao na hilo wala watu wasiwe na wasiwasi” alisisitiza Mkurugenzi huyo.

Aidha alisema zipo faida nyinyi za kuwa na kitambulisho cha taifa kama vile kitambulisho cha mzanzibari mkaazi na hivyo vitambulisho hivyo vitatumika katika huduma mbali mbali za kijamii na za maendeleo.

Akizitaja hasara za kutokuwa na vitambulisho vya mtanzania, Mkurugenzi alisema wananchi kuendelea kuwa katika umasikini kwa kushindwa kupata mikopo katika banki na taasisi za fedha, ambapo benki zimekuwa zikitoa riba kubwa kutokana na kuwa baadhi ya wananchi kutorejesha mikopo kwa kukosekana kutambuliwa.

Alisema pia bodi ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu imekuwa inapata matatizo na malalamiko mengi kwa kushindwa kumtambua mwanafunzi yupo anastahiki mkopo na kwa kiasi gani ambapo urudishwaji wa mikopo umekuwa ni mgumu.

Mkurugenzi huyo alisema kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu na has unaofanywa na raia kutoka nchi jirani na wafungwa waliomaliza adhabu zao au kuachiwa huru kwa msamaha wa rais ni miongoni mwa hasara za kutokuwa na kitambulisho.

Kuongezeka kwa mrundiko wa wafungwa katika magereza mbali mbali nchini kutokana na kutokuwepo na uthibiti wa wafungwa wa kifungo cha nje ni miongoni mwa hasara hizo.

Alisema serikali inabeba mzigo mkubwa wa gharama wakati wa zoezi la kupiga kura kwa kuwa na kitambulishocha taifa ambapo hupunguza gharama kubwa za kuhuisha daftari la kudumu la kupigia kura kila inapohitajika.

Aliwaambia waandishi wa habari kwamba mpango huo wa kuwa na vitambulisho utasaidia serikali katika mipango yake ya maendeleo na utarahisisha na kuwawezesha vijana wengi kupata hati za kusafiria (passport) tofauti na hali ilivyo sasa.

Mkurugenzi huyo alisema vitambulisho hivyo vina hadhi sawa na vile vya mzanzibari mkaazi na kukanusha kuwa vina lengo la kuishushia hadi Zanzibar kama nchi ambapo baadhi ya watu wameanza kuwa na khofu juu ya kuchukua vitambulisho vya Matanzania wakihofia kufutwa vile vya Mzanzibari Mkaazi (ZANID).

“Ni imani yangu kubwa wananchi, viongozi wa dini, masheha na wanasiasa kwa ujumla, tutatoa ushirikiano kwa maafisa wetu wasajili ambao watakuwa katika kila shehia kufanya usajili, na kila mmoja wetu aone ana jukumu kubwa la kulipa kipaumbele suala hili ni kwa maendeleo na kwa mustakabali wa taifa letu” amesema Vuai.

Baadhi ya viongozi wa dini wa kiislamu ndio wanaowashawishi wafuasi wao kugomea vitambulisho hivyo, ambapo alieleza kuwa ofisi yake imefanya juhudi ya kukutana na viongozi wa kiislamu ili kuondosha shaka juu ya vitambulisho hivyo.

Akizungumzia mtazamo wa jumuiya ya uamsho na mihadhara ya kiislamu Zanzibar (JUMIKI) Katibu wa jumuiya hiyo Sheikh Abdallah Said Ali alisema kitambulisho cha Mtanzania kinakuja kufuta kitambulisho cha Zanzibar kwa kuwa ndio kitakachoshughulikia masuala yote ya kijamii.

“Mimi naona kama ni mipango maalumu ya serikali ya Jamhuri kutaka kuifuta sehemu ya Zanzibar kuwepo katika jamhuri ya muungano wa Tanzania na ndio maana tunasema hakuna sababu ya kuchukua kitambulisho hicho kwa kuwa sisi tuna vitambulisho vyetu” alisema Sheikh Abdallah.

Alisema masharti ya upatikanaji wa vitambulisho vya taifa ni mepesi ambapo vitagaiwa hata kwa watu ambao hawatakuwa na vyeti vya kuzaliwa, lakini kupitia kamati za vijiji vyao watajadiliwa na hatimae kupewa vitambulisho hivyo huku akiwatoa khofu wazanzibari kwa kuwaambia havitatumika kisiasa.

Watanzania wote wenye umri miaka 18 na kuendelea watapatiwa vitambulisho hivyo ambavyo vitahitajika katika matumizi mbali mbali ikiwemo huduma za kijamii na kuimarisha usalama.

Tanzania hivi sasa inatekeleza mpango wake wa kutoa vitambulisho kwa raia zake, baada ya mchakato uliochukua miaka mingi hadi kukamilika na kuanza rasmi mwaka jana ambapo zaidi ya billioni 200 zitatumika katika mradi huo mkubwa.

No comments: