ANGALIA LIVE NEWS

Friday, October 19, 2012

Ponda afikishwa kortini pekupeku

Waandishi Wetu
KATIBU wa Jumuiya na Taasisi za  Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam akiwa chini ya ulinzi mkali, kujibu tuhuma tano zikiwamo wizi na uchochezi.

Tuhuma zingine ni kula njama, kuingia kwa nguvu kwenye eneo lisilo mali yake kwa nia ya kutenda kosa na kujimilikisha ardhi kwa nguvu na kusababisha uvunjifu wa amani.

Sheikh Ponda alifikishwa mahakamani hapo akiwa na watu wengine 49 akiwamo Bibi Zaina Yusufu (100), ambao waliunganishwa naye katika mashtaka manne isipokuwa shtaka la uchochezi ambalo linamkabili Ponda pekee.

Ponda ambaye anadaiwa kuwashawishi wafuasi wake kutenda makosa ya kihalifu alisomewa mashtaka, lakini alinyimwa dhamana baada ya Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka kuwasilisha mahakamani hati kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP)  inayozuia dhamana.

Hati hiyo ilitolewa chini ya kifungu cha 148 (4) cha sheria ya Mwenendo wa mashauri ya Jinai (CPA) na wakili Kweka aliomba iwekwe kwenye kumbukumbu za mahakama, hali iliyozua mabishano ya kisheria baina yake na wakili wa utetezi, Juma Nassoro .

Kufikishwa mahakamani
Ponda alifikishwa mahakamani hapo, jana saa 6:20 mchana  na gari lililosindikizwa na magari mengine mawili aina ya Land Rover Defender; kila moja likiwa na askari zaidi ya watano wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) ambao walikuwa na silaha.


Pia msafara huo, uliongozana na gari  la maji ya kuwasha pamoja na askari waliokuwa na mabomu ya kutoa machozi. Sheikh Ponda alipofikishwa  mahakamani alitenganishwa na washtakiwa wengine na alikuwa amevalia  kanzu huku miguuni akiwa hana viatu.

Alipelekwa moja kwa moja kwenye ukumbi wa Mahakama ya Wazi namba moja ambako aliwakuta washtakiwa wenzake 49. Washtakiwa hao wengine walifikishwa mahakamani hapo saa 5:15 asubuhi kwa karandinga.

Ilipofika saa 6:56 mchana, Hakimu Mkazi, Stuart Sanga aliingia mahakamani na kuanza kusikiliza  kesi hiyo. Hata hivyo alieleza kuwa shauri hilo lilipangwa kusikilizwa na Hakimu  Victoria Nongwa ambaye jana hakuwapo.

Baada ya kusema hivyo,  Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka alianza kuwasomea washtakiwa hao mashtaka yanayowakabili.

Mashtaka yao
Katika shtaka la kwanza, Wakili Kweka alidai kuwa Oktoba 12, mwaka huu  katika eneo la Chang'ombe Malkazi, washtakiwa hao kwa pamoja walikula njama ya kutenda kosa kinyume na kifungu cha 384 cha sheria ya kanuni ya adhabu.

Katika shtaka la pili alidai kuwa Oktoba 12, mwaka huu, katika eneo hilo la Chang'ombe Malkazi lililopo wilaya ya Temeke, kwa jinai na pasipo sababu za msingi  walivamia ardhi inayomilikiwa na kampuni ya Agritanza Ltd kwa nia ya kujimilikisha  isivyo halali.

Wakili huyo alidai kuwa kosa hilo ni kinyume na kifungu cha 85 na 35 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002. 

Katika shtaka la tatu, Kweka alidai kuwa kati ya Oktoba 21 na 16, mwaka huu  katika eneo hilohilo, washtakiwa hao kwa pamoja pasipo uhalali  wowote, walisababisha uvunjifu wa amani kwa kujimilikisha ardhi ambayo ni mali  inayomilikiwa kihalali na Kampuni ya Agritanza Ltd.

Wakili Kweka katika shtaka la nne, alidai kuwa washtakiwa hao kwa pamoja kati ya Oktoba 12 na 16, waliiba vifaa na malighafi mbalimbali za ujenzi, yakiwamo matofali 1500, tani 36 za kokoto na nondo  vyote vikiwa na thamani ya Sh59.65 milioni, mali ya kampuni ya Agritanza Ltd.

Walioshtakiwa wengine
Mbali na Ponda na Zainabu,  washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Kuruthumu Mfaume, Zainabu Mohamed, Juma Mpanga, Farida John, Adam Ramadhan, Athuman Salim, Seleman Jumbe, Salum Mzee,  Salum Ally na  Rahma Amza.

Pia wamo Halima Abbas, Maua Omary, Fatihia Habibu, Hussein Ally, Shaban Ramadhan, Hamis Mohamed, Rashid Ramadhan, Yusuphu Penza, Alawi Mussa, Ramadhan Rashid, Omary Ismail, Salma Abdulatifu, Halid Issa, Said Rashid, Pesual Bakari, Issa Msuya na  Ally Mohamed.

Wengine ni  Mohamed  Ramadhan, Abdallah Haule,  Juma Hassan,  Mwanaomary Makuka, Omary Bakari,  Rashid Ndimbo, Hamza Ramadhan, Ayoub Juma, Maulid Nandepa, Bakari Jamal, Swalehe Abdul,  Jumanne  Mussa, Salum Abdallah,  Hamis Mchomi, Bite Bilali, Amir Said, Juma Ally, Athuman Suleiman, Lukaiya Yusufu, Abubakari Juma  na Ally Shaban.

Baada ya kuwasomea mashtaka, Kweka aliiambia mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kisha alitoa hati ya DPP inayozuia dhamana kwa Sheikh Ponda na watuhumiwa wenzake 49.

Wakili wa utetezi, Nassoro  alipinga hati hiyo kwa madai kuwa sababu zilizotolewa na DPP za kuwanyima washtakiwa hao dhamana ni za kiujumla na kwamba mahakama haiendeshwi hivyo.

Wakili Nassoro alidai kuwa dhamana  ya mtu ni haki ya msingi ya mshtakiwa, hivyo haiwezi kuondolewa kwa maelezo ya kiujumla." 

"Makosa yote matano  yanayowakabili wateja wangu yanadhaminika na kama  DPP alikuwa anaona Ponda  aondolewe kupewa dhamana  ilibidi atoe sababu zinazoeleweka," alidai Nassoro.

Hivyo aliiomba Mahakama kutoa masharti ya dhamana kwa wateja kwake ambayo yanatekelezeka hususan kwa bibi kikongwe wa miaka 100.

Wakili Kweka alijibu hoja hizo kwa kusema kuwa kifungu cha 148 (4) kinajieleza chenyewe  na kuwa DPP anapokitumia, mahakama inafungwa mikono  na kwamba halazimiki kutoa sababu zozote.

"Ponda kwa sasa hapaswi kupewa dhamana kutokana na hati hiyo, atapewa dhamana hadi hapo DPP atakapoleta hati nyingine ya kutengua hati hii ya zuio la dhamana," alisisitiza Kweka.

Hata hivyo Hakimu Sanga alisema  yeye yupo mahakamani kwa niaba ya mwenzake tu na kwamba hawezi kuamua chochote hadi hapo hakimu anayepaswa kuisikiliza kesi hiyo, Victoria Nongwa atakaporejea. 

Aliiahirisha kesi hiyo hadi Novemba Mosi, mwaka huu itakapotajwa.

Baada ya kesi hiyo, Wakili Nassoro  aliwaambia Waislamu kuwa suala hilo ni kweli limeleta hisia, lakini wajue limefika mahakamani hivyo watulie, wawe na subira  na waamini kuwa mahakama itatenda haki.

Bakwata walaani 
BARAZA la Waislamu Tanzania (Bakwata), limelaani matukio yote ya vurugu yaliyofanywa kwa makusudi na watu wanaotumia mwavuli wa dini ya Kiislamu na kutaka sheria ichukue mkondo wake ili haki itendeke.

"Sisi tunalaani vurugu. Tunataka watu wafuate sheria na waziheshimu," alisema Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Bakwata, Shaban Simba.

Simba aliongeza kusema: "Hatufahamu alichofanya Sheikh Ponda hata akakamatwa lakini kama amekamatwa kwa sababu ya vurugu, sheria lazima ifuate mkondo dhidi yake na wanaofanya vurugu hizo kwa mgongo wake."

Mihadhara marufuku 
Katika hatua nyingine, Polisi wamepiga marufuku mihadhara ya aina yote nchini inayolenga kuleta uchochezi na kukashifu dini za wengine.

Akizungumza na Mwananchi jana, msemaji wa Polisi, Adivera Senso alisema polisi hawatamvumilia mtu au kikundi chochote chenye nia ya kuleta uvunjifu wa amani.

Senso alisema kuwa, kuna kikundi cha watu wachache kinachotumia mwavuli wa kidini kuvuruga amani ya nchi na kwamba jeshi hilo limejipanga kuhakikisha linakomesha vitendo hivyo.

"Napenda nikuhakikishie kwamba Jeshi la Polisi limejipanga vizuri kuanza kuwashughulikia watu wote wanaohatarisha amani ya nchi hasa wale wanaoendesha mihadhara ya kidini na kutumia mwavuli wa kidini. Wote watadhibitiwa," alisema Senso.

Alisema kuwa kama mtu anataka kufundisha dini kwa kutumia mihadhara anatakiwa kufundisha maadili ya dini yake kwa waumini wa dini yake na siyo kukashifu dini za wenzake kwani jambo hilo linalenga kuleta uchochezi na uvunjifu wa amani.

"Polisi hairuhusu mikutano yote inayotumia lugha za uchochezi  na wale wanaoendelea kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na kwamba hawaogopi vitisho vya mtu yeyote au kikundi chochote kinachojita cha kidini," alisema Senso.

Imeandikwa na Taus Ally, Gedius Rwiza na Festo Polea wa gazeti la Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

tumekutafutiyeni uhuru kutoka kwa mkoloni na historia yetu mmetupotoshea, tunalipa kodi zenu na makanisa na mapadri ndo wanafaidika, raisi anatumwa nchi za kiarabu kuomba omba kama omba omba halafu faida makanisa ndo yananufaika, elimu mnatubania kisa muonekana nyinyi ndo wenye kichwa, halafu mnasema tuna jazba je haya yanayotendeka siyo jazba, kule zanzibar si mlisema kwamba kama serikali hatoshughulikia basi nyinyi mtawashughlikia na kuwauwa maskini za mungu na sasa kumteka sheikh wao kama alivyo uliwa raisi wao.

mme mficha sheikh farid sasa anataka kumuuwa huyu ponda ole wenu nakuambiyeni

kama mnataka kuhesabu sensa sasa oneni wenyewe na mnajua waislamu ni wengi kuliko wakiristo ndo maana mnawafanyia kila njama kuwateketeza waovu nyinyi jueni hata mkiungama madhambi yenu katu daima abadan hayatofutika kesho mungu anakusubirini hakuna aliyechukua mzigo wenu kila mtu atabebe mzigo wake kwa yale ayatendayo cheo ni dhamani kuna siku mcha kiachia ngazi idha kufukuzwa kuachishwa kustaafu au kufaaa