ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 2, 2012

Ripoti mauaji ya Mwangosi kuwekwa hadharani Oktoba 9


Ripoti ya uchunguzi wa mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari mwakilishi wa kituo cha televisheni ya Channel Ten, mkoani Iringa, marehemu Daudi Mwangosi, uliofanywa na timu ya waandishi wa habari watatu kutoka Baraza la Habari (MCT) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), itawekwa hadharani Oktoba 9, mwaka huu.

Azma hiyo ilitangazwa jana Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga, baada ya timu hiyo kukamilisha uchunguzi wake hivi karibuni.

Mukajanga alitangaza azma hiyo alipotakiwa na NIPASHE kueleza lini ripoti hiyo itatangazwa.

Akijibu swali hilo kwa njia ya maandishi, Mukajanga alisema kwa kifupi: “Jumanne Oktoba 9, 2012 Inshallah.”

Awali, NIPASHE ilizungumza na Katibu Mtendaji wa TEF, Neville Meena, ambaye alisema uchunguzi wa timu hiyo umeshakamilika na kwamba, ripoti yake imekabidhiwa kwa Bodi ya MCT. 



Timu ya waandishi hao iliyoundwa Septemba 4, mwaka huu, iliongozwa na Meneja wa Utafiti na Machapisho wa MCT, John Mirenyi, wajumbe wakiwa ni Mhariri wa masuala ya siasa wa gazeti la Mwananchi, Hawra Shamte na Mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini, Kitivo cha Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma, Simon Berege.

Timu hiyo ilipewa siku nane na ilianza kazi yake Septemba 6, mwaka huu, kubaini ukweli wa tukio hilo na kuweka kumbukumbu sahihi ya tukio hilo.

Wakati huo huo, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso, alikataa kuzungumzia timu ya jeshi hilo iliyoongozwa na Mkuu wake, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema, umekwisha au nini kinaendelea, akisema hawaruhusiwi kufanya hivyo kwa kuwa liko mahakamani kisheria.

“…Waziri wa Mambo ya Ndani alishalisemea,” alisema Senso.

Mwangosi, ambaye alikuwa pia Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani humo (IPC), aliuawa kwa kupigwa na bomu lililosambaratisha mwili wake wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuwazuia kufungua tawi la chama hicho, katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi, mkoani humo, Septemba 3, mwaka huu.

Tayari askari polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), mwenye namba G2573, Pasificus Cleophace Simon (23), amefikishwa mahakamani akituhumiwa kwa mauaji ya Mwangosi.
CHANZO: NIPASHE

No comments: