Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania, Sophia Simba akishangilia ndani ya Ukumbi wa Chuo cha Mipango kwenye mkutano mkuu wa 8 wa umoja huo taifa uliofanyika jana, mjini Dodoma. Picha na Edwin Mjwahuzi
AZOZANA NA SHYROSE, NUSURA WAZIPIGE UKUMBINI KABLA YA UCHAGUZI
Na Habel Chidawali, Mwananchi Dodoma
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba ameendeleza ubabe wake dhidi ya hasimu wake kisiasa, Anne Kilango baada ya kumbwaga kwa idadi kubwa ya kura katika uchaguzi wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT).
Hii ni mara ya pili kwa Simba kumshinda Kilango katika kuwania nafasi ya uenyekiti wa UWT, mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2008, ambapo Simba aliibuka mshindi.
Katika uchaguzi huo uliofanyika mjini Dodoma ukisimamiwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, Sophia Simba alipata kura 716 huku Kilango akipata kura 310 na mgombea wa tatu wa nafasi hiyo Maryrose Majinge aliambulia kura 7.
Simba, Bhanj wazozana
Hata hivyo, uchaguzi huo ulinusurika kuingia dosari baada ya mbunge wa Afrika Mashariki Shyrose Bhanj, kuchafua hali ya hewa ambapo yeye na mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Simba nusura wapigane.
Katika tukio hilo, Shyrose na Simba huenda wangepigana kutokana na kila mmoja kutaka kuonyesha ubabe kwa mwenzake.
Hali hiyo ilitokea baada ya Bhanj kuelekeza tuhuma za moja kwa moja kwa Simba kuwa katika kipindi chake cha uongozi, hakusimama katika majukwaa kuisaidia CCM hata siku moja.
Kauli hiyo ilionekana kumkwaza Simba, aliyekuwa jukwaani akijieleza na baada ya kushuka alikwenda moja kwa moja mahali alipokuwa ameketi Bhanj na kumnyooshea kidole akisema: “Huniwezi wewe!”
Kauli hiyo ilimkasirisha Bhanj na kufanya ahamaki. Aligeuka na kuuliza: “What! Uko na mimi?”
Ilikuwa kama sinema, kwani awali, Bhanj alitoka katika kiti alichoketi na kwenda kukaa mbele, alipokuwa ameketi Sophia Simba, ili aweze kupata nafasi ya kuuliza maswali.
Awali Bhanj alimuuliza mgombea Anne Kilango Malecela akitaka kujua kilichomsukuma kugombea uenyekiti wa UWT.
Hata hivyo, swali hilo lilikataliwa na aliyeongoza mkutano huo akiwa msimamizi wa uchaguzi huo, Profesa Anna Tibaijuka akisema halikuwa na mashiko.
Hata hivyo, Bhanj aliomba nafasi tena, kabla ya kuipata ya kumuuliza Simba, Tibaijuka aliwaelekeza kuwa, aulize swali na siyo kutoa hotuba.
“Mheshimiwa mjumbe, naomba uulize swali siyo kutoa hotuba, tafadhali naomba apewe nafasi ya kuuliza swali maana naamini pia mgombea wetu ni mahiri atalijibu tu,” alisema Tibaijuka, kauli iliyotafsiriwa na baadhi ya wajumbe kuwa ni ya kumbeba Simba.
Akijibu swali hilo Simba alisema: “Huyu mjumbe, hajui kabisa kampeni za chini, hizo kelele za wajumbe zinaonyesha kuwa nilikuwa nafanya kazi kikamilifu, ndiyo maana hata yeye amekuwa ni Mbunge wa Afrika Mashariki kupitia sisi wanawake.”
Majibu ya Simba yalilipua kelele kutoka kwa wajumbe ambao moja kwa moja walianza kumshangilia licha kuwa awali ilikatazwa kufanya hivyo.
Baada ya kumaliza kujieleza na kuomba kura, ndipo Simba alishuka kuelekea mahali alipoketi na Bhanj alisimama akitaka kumpisha, lakini ghafla Simba akamnyooshea kidole na kumweleza kuwa hatamuweza.
Ndipo wakaanza kujibizana na kusababisha mkutano huo kusimama kwa muda, huku wapambe waliodaiwa kuwa wa Sophia Simba wakionekana kukerwa zaidi na kutaka kumpiga Bhanj, aliyesaidiwa na watu wa usalama kuondolewa eneo hilo.
Hata hivyo, Profesa Tibaijuka alizuia watu wa usalama wasimtoe nje Bhanj kwa sababu ni mjumbe halali wa mkutano huo
Mwananchi
No comments:
Post a Comment