
Watu tisa wametiwa mbaroni katika Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara kwa tuhuma za kupatikana na nyara za serikali pamoja na bunduki mbili.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kukutwa na nyumbu watano na kanga watatu wenye thamani ya Sh. 3,209,480.
Aidha, wanadaiwa pia kukutwa na silaha na magari mawili huku mmoja wao akituhumiwa kukutwa akiwa na jozi tatu za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Afisa Wanyamapori wa Wilaya ya Mbulu, Allan Shanny, alisema watuhumiwa hao walikamatwa juzi majira ya saa12:00 asubuhi katika pori la hifadhi la Bonde la Yaeda Chini wilayani Mbulu.
Shanny alisema kukamatwa kwa watuhumiwa hao kulitokana na raia wema kutoa taarifa kwa Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD), George Kyando, ambaye alichukua hatua mara moja
.Alisema Kamanda Kyando aliwatuma askari ambao walikwenda kuwakamata watuhumiwa hao.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Juma Rashid (56), mkazi wa Singida, Kukuni Wadee (30), mwenyeji wa Geita anayedaiwa pia kukutwa akiwa na jozi tatu za JWTZ, Greyson Msengi (61), mkazi wa Singida na Raphael Matola (53), mkazi wa Shinyanga na Shabani Omari (30), mkazi wa kijiji cha Dominiki mkoani Singida
Aliwataja wengine kuwa ni Bakari Mbwana (30), Omari Abraham (57), Zosmos Patrick (33) na Adamu Issa (27), wote wakazi wa mkoani Singida, ambao alisema hao walidai kuwa hawahusiki bali waliitwa kama mafundi wa magari.
Kwa mujibu wa Shanny, watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na bunduki mbili moja aina ya shotgun na risasi zake tano na nyingine aina ya Mark IV. Silaha nyingine alizodai walikutwa nazo watuhumiwa ni mapanga sita visu vinne.
Aidha, alisema watuhumiwa pia walikutwa wakiwa na tochi kubwa tatu, sufuria tano na madebe mawili ya unga wa mahindi na magari mawili aina ya Land Rover TID lenye namba za usajili T 652 APK, lilikiendeshwa na Raphael Matola (53) na lingine lenye namba za usajili T161 ARR likiendeshwa na Zosmos Patrick (33).
Shanny alisema Sheria ya Wanyamapori ya mwaka 2009, inakataza shughuli za uwindaji haramu isipokuwa kwa kibali maalum (leseni) tu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment