Lakini taratibu udini na ukabila umeanza kuingia kwa kasi katika nchi yetu, kitu ambacho naona ni hatari sana kwa vizazi vyetu na vijavyo. Matukio ya wiki iliyopita huko Mbagala jijini Dar es Salaam ni sawa na yaliyotokea Zanzibar. Makanisa yamechomwa moto. Siku hizi kiongozi anadiriki kusimama jukwaani na kudai chama fulani ni cha dini au mtu fulani achaguliwe kwa kuwa ni kutoka ‘kanda yetu.’ Hili ni jambo la hatari.
Binafsi nakumbuka sana hotuba ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyoitoa Hoteli ya Kilimanjaro mbele ya Klabu ya Waandishi wa Habari Tanzania Machi 13, 1995, ambapo alitaja nyufa tano zinazolitikisa taifa letu hadi kufikia katika msingi ule imara wa utaifa uliojengwa kwa muda mrefu. Nyufa zipo kwenye muungano, kuendesha mambo bila kujali sheria, rushwa na udini na ukabila.
Kwa muda mrefu sasa, nchini mwetu kumesikika malalamiko au manung’uniko ya wafuasi wa dini moja kudai kukandamizwa au kunyimwa fursa sawa za elimu katika nchi yetu, ni wazi walalamikaji wanaona kuna udini.
Huko nyumba yalitolewa madai ya haki za Waislam kama yalivyotolewa na kauli ya Baraza Kuu la Jumuia na Taasisi za Kiislam Tanzania mwaka 1993. Mwaka 1998 kulitolewa waraka kwa serikali kulaumu Kanisa Katoliki na Serikali ya CCM katika hili. Kuna malalamiko yanayojirudiarudia licha ya kutolewa majibu na mamlaka husika.
Mwalimu alipokuwa akila kiapo cha kuwa Rais wa Jamhuri ya Tanganyika alizungumzia tofauti ya elimu kati ya Wakristu na Waislam, hiyo ilikuwa Desemba 10, 1962 katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam na alisema, nanukuu:
“…uhasama baina ya waumini wa Kiislam na Kikristo ambao unaweza kuenezwa na fikra potofu , kama tunavyojua, ni matokeo ya serikali ya kikoloni kutojihusisha hata kidogo na elimu kwa Waafrika na kwa maana hiyo wengi wa wale walioipata kwa kiwango chochote, walifanya hivyo kupitia shule za misheni na kwa hiyo ni Wakristo, hivyo wengi wao ni Wahaya, Wanyakyusa na Wachaga…”
Kwangu mimi haya yalikuwa mawazo sahihi ya Mwalimu na hakuna aliyebisha, lakini watu wasioitakia mema nchi hii wakachukulia maneno hayo kwa kugeuza kibao na kudai Waislam hawajapewa elimu kwa makusudi.
Mwaka 1970 serikali ya Nyerere iliamua kutaifisha shule zote za misheni na za binafsi katika nchi yetu kama hatua muhimu ya kupunguza tofauti katika elimu kwa Waislam na Wakristo maana kuanzia hapo hapakuwepo tena shule za misheni. Matokeo ya utaifishwaji ule, yameharakisha sana upatikanaji wa elimu kwa Waislam wengi hapa nchini.
Alhaji Ally Hassan Mwinyi, Rais wa Awamu ya Pili aliliona tatizo la elimu kwa Waislam na wakati anafungua Ofisi za Shirika la World Muslim League mwaka 1998 jijini Dar es Salaam, alisema “… Ndugu Waislam, punguzeni malalamiko dhidi ya serikali na muanze kufanya kazi… tujenge vyuo vya elimu ya kizungu ili tuwaandae watoto wetu kushika nafasi za uongozi…” naamini huu ulikuwa mwongozo bora na safi kwa Waislam.
Mwaka huu, 2012 baadhi ya Waislam wamelalamikia matokeo ya mtihani wa Kidato cha Sita kwa shule za Waislam hata kuwafanya wengine wasiwe na imani na uongozi wa Baraza la Mitihani (NECTA) lakini Sadiki Godigodi ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Tanzania Islamic Peace Foundation alitoa maelezo ya kueleweka sana katika gazeti la Majira la Jumatatu, Juni 25, mwaka huu.
Alisema wasahishaji wakati wa kufanya kazi hiyo huwa wanaona namba za watahiniwa wala siyo majina yao, hivyo hawajui karatasi hii ya Mwislam au ya Mkristo! Akaonya kuwa wote wanaopandikiza chuki na kunufaika na mgogoro huo waache kwani wataangamiza taifa.
Gazeti la Uhuru la Jumatatu, Juni 28, 1993 lililoandika wazi upendeleo uliofanywa hapa Dar es Salaam katika kuchagua watoto wa kuingia kidato cha kwanza, majina ya watoto 84 Wakristo yakiachwa na nafasi zao wakapatiwa wenzao wa Kiislam matokeo yake gazeti hilo la Jumatano, Juni 30, 1993 yalitangazwa majina ya walimu 58 waliohusika na kashfa hiyo ya upendeleo kwa watoto wa Waislam na kwa mujibu wa sheria walisimamishwa kazi hapa Dar es Salaam.
Nimetoa mifano hii kuonesha kuwa udini katika nchi yetu upo na umeanza kugawa taifa na sijaona viongozi wakikemea kwa nguvu zote. Nawasihi Watanzania kwamba tusiupe mwanya ufa huu wa udini na ukabila utumalize kwani tutajuta.
Naamini wale wote wanaoujua Ukristo au Uislam hawapayuki ovyo, ni wasikivu, hawana dharau kwa wasiokuwa wa dini yao badala yake wanashirikiana kutunza amani. Maalim Hassan Yahya Hussein aliwahi kuniambia kuwa sura ya IV Maidah aya ya 82 inasema, Uislamu hauchukii Ukristo, sasa vipi Waislam halisi wachome makanisa? Matukio kama yale ya Zanzibar na juzijuzi Mbagala ni ya kulaaniwa kwa wapenda amani wote.
Nawasihi Waanzania kwamba tuepuke vishawishi vya kutugawa kwa misingi ya udini na ukabila, tuendelee kuwa Watanzania wenye imani za kiroho tofauti kutokana na mapokeo tuliyonayo, bila kufanya hivyo, tutaiingiza nchi katika matatizo mazito.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
3 comments:
msipotoshe na kutudanganya yeye ndo aliye kuwa mdiji mkubwa alilikubatia kanisa lake hakuliwacha katu katika siasa zake,alikuwa na ukabila pia, waislamu hawakuwa na udini hata chembe walipo msaidia kutafuta uhuru walimuona mwenzao lakini alivyoupata mbona alijua udini wake na kuwaweka watu wake wa udini wake na kabila lake.
msitudanganye bwana mmetudanganya hapo zamani lakin si sasa tumeshaamka na tuna fanya research na kusoma vitabu vya kila aina hata kama mmeipotosha historia yetu.
binadamu kiumbe mzito mdanganye mmanya lakini si binadamu
nimeyasoma maneno yako muandishi lakini ninacho sema nyerere hajatufanyia chochote sisi, tumemsaidia na katuacha solemba na ni kweli kabisa utake usitake muandishi wa nakala hii kwamba waislamu waliachwa maksudi wasipae elimu na hadi hii leo utasikai si wao wanataka elimu ya akhera hawataki ya dunia wako madras shule hawataki, ni mtu juha sana anayesema hivi na kuamini hivi.
katika dini zote hakuna dini iliyosisitiza kusoma zaidi ya uislamu mkitaka msitake fanyeni research na ndo maana anaposoma muislamu huwa anasoma kweli kweii si mchezo anakuwa msomi kweli kweli si wakugushi wala wa kitapeli.
lakin yote sawa mungu mkubwa binadamu hakuna atakacho kufanyia zaidi ya muumba wako ambaye siyo athumani atakaye kuonea choyo ukipata.
waislamu sio wadini hata kidogo walimsaidia mwalimu kupata uhuru kwani walikuwa hawajui ni mkiristo alivyopata si kawasaliti na kuwataifishia majumba, mashule na mali zao kisa kujenga vijiji vya ujamaa ujama gani kama si choyo na husda zake.
walivyokuja wakoloni nani alikuwa makarani wao,wakiristo walikuwa hawakusoma hivyo na hawapo wengi hivyo, bwana msitupotoshe tuna ijua historia yetu.
ndo maana hivi sasa tunakuonneni mnakaza buti mnaguogopa mnataka tuwe chini yenu daima na nyinyi kujifanya mmewahi na kusoma wapi
mungu si athumani.
kwa nini basi msifufuwe TANGANYIKA, NNAOGOPA NINI SI MNAJUA KWAMBA MICHANGO MIKUBWA YA WAISLAMU ITAONEKANA KATIKA HISTORIA.
ETI VITA VYA MAJI MAJI WALIKUWA WAMEJIPAKA MAJI WATU WAZUNGU WAKIPIGA RISASI ISIWAUWE MNAWAZIMU
WALIKUWA UMMMA WA KIISLAMU WANAKWENDA KUSALI WALITAWADHA ILI KUMUOMBA MUNGU AWAOKOWE. MMEIPOTOSHA HISTORIA YA NCHI NA MCHANGO WA WAISLAMU LAKINI MTATUONA HIVI HIVI TUKINGARA NA MADRASA YETU DAIMA.
Huyu muandishi alianza kutaja mada za Udini na Ukabila lakini hakuizungumzia zaidi mada ya Ukabila badala ya kuitaja tu bali amejikita zaidi kwenye Udini, hivyo inanifanya niamini kwamba yeye mwenyewe inaonekana anajisikia vibaya dhidi ya uonevu wa siri na wa dhahiri uliokuwa unafanyika kwa Waislam na kuwanyima elimu bora. Mfumo wa namba ulikuja baada ya malalamiko mengi ya Waislam kuonewa kwenye kusahihisha mitihani na kufelishwa vibaya na huyo Nyerere mwenyewe ulimkera sana mfumo huo wa namba ulipoletwa lakini hakuwa na la kufanya ila kuukubali tu ili kupunguza malalamiko lakini kwa vile namba zilitolewa baada majina kuainishwa ikawa bado wanaendeleza uonevu kwa siri.
Sasa muandishi ulitegemea Waislam wakubali tu kila wanalofanyiwa kisa eti wasije wakahatarisha amani? Chanzo cha yote ni uonevu na kubaguliwa na watu wameshachoka, Waislam wakipewa haki sawa hawana matatizo. Muandishi napenda kukwambia kuwa kuna watu wengi sana walifikia hatua ya kubadilishwa majina kutoka ya Kiislam kwenda ya Kikristo ili wapate nafasi za elimu ya juu, sasa jifanye hulijui hilo na kama kweli hulijui basi ungefanya uchambuzi juu ya hili suala kabla hujaandika hii makala yako. Uislam ni dini ya Amani na Usawa, haibagui mtu.
Kwa mfano, Mw. Nyerere hakuweza kupigania Uhuru na kufanikiwa bila ya msaada wa Waislam. Kuna Sheikh mmoja mkubwa na maarufu sana aliewahi kuwa Mufti wa Afrika Mashariki nzima akiitwa Sheikh Hassan Bin Ameir (Mungu amraham), huyu Sheikh alimsaidia sana Nyerere wakati wa kupigania Uhuru na kumsaidia kupata kura nyingi za Waislam. Huyu Sheikh akitoa kadi za TANU kwenye mihadhara yake ya dini. Lakini baada tu ya Tanganyika kupata Uhuru na Nyerere kuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri, alimfurusha mbio na kumrejesha Zanzibar alipotokea kisa akimkosoa juu ya masuala ya kuendesha nchi na usawa kwa Waislam. Mwisho wa yote Nyerere akaishia kulalama, eti tumechoka na Wazanzibar na Uislam. Kiasi hayo matatizo mnayoyaona sasa yatokee ni kwa alichokipanda huyo huyo Nyerere na chuki zake dhidi ya Uislam. Kama Nyerere hakuwa mdini, asingekuwa akijinasibu kwenye viriri, kwa mfano kwenye hiyo hiyo hutuba aliyotowa alipokutana na waandishi wa habari mwaka 1995 alijinasibu kwamba anaona fahari kuwa ni Mkatoliki anaetembea kila mahali na Biblia yake na Azimio la Arusha na kila anapokwenda basi akijinasibu na Uzanaki wake.
Sasa ndio muyaone mapungufu ya huyo Mw. Nyerere kwamba hutowadhulumu watu haki zao na kuhubiri Usawa kiujanja ujanja, na kudhibiti waumini wa dini moja (Uislam) ukategemea utajenga Taifa lenye kuishi kwa amani milele, hapana, iko siku yatakurudi tu. Ndio matatizo yaliokuwepo sasa hivi Tanzania.
Mdau wa California, Haji Jingo.
Post a Comment