ANGALIA LIVE NEWS

Monday, October 15, 2012

UBINAFSI ULIVYO HATARI KWENYE MAPENZI NA FAMILIA -4


TUENDELEE na mada yetu, leo ikiwa ni sehemu ya mwisho. Zingatia kwamba kama mpenzi wako ananuka kikwapa, usimuache akachekwa mitaani. Unayo nafasi ya kumlinda kwa kumfanya badala ya kunuka awe ananukia. Hii ni kwa sababu mnapokuwa wawili, ujenzi wa thamani yenu unategemeana. Unamjenga mwenzako naye anakujenga.
Siku zote tambua kwamba jinsi unavyojiweka kistaarabu ndivyo unavyoweza kutoa sura ya namna ambavyo mwenzi wako atachukuliwa na watu wengine. Mapenzi ni sanaa inayohitaji mtu aishi kwa masilahi ya mwenzi wake. Kwa faida yako, nakuomba uanze utekelezaji wa falsafa hii.
Kuna msemo kwamba ukitaka kumjua mtu muangalie rafiki yake. Hivi ndivyo inavyokuwa. Sasa basi, ikiwa mwenzi wako atakuwa na sura ya ovyo mbele ya jamii, itakutafsiri kwamba nawe ni ovyo. Hebu vaa upendeze halafu umfanye naye apendeze ili mpewe sifa mnayostahili.
Ubinafsi usiotakiwa, kuwa hodari wa kubadili mavazi wakati mwenzako amechakaa, ngozi inakosa matunzo, nywele hazitamaniki na nguo zake zimechanika, utakufanya ushushwe hadhi kwenye jamii, wakati mwenyewe utakuwa unajiona mwanamke au mwanaume bora, mtanashati au mrembo.

SHINDA UBINAFSI, ZUIA MATUMIZI MABAYA YA FEDHA
Unapoamua kuwa na mwenzi wa maisha, maana yake unakuwa umejiridhisha kwamba unajitosheleza kwa malezi. Yaani utamlea kama ambavyo wewe mwenyewe unavyojilea. Hiki siyo kipengele cha jinsia, watu wote wanawajibika kwenye eneo hili.
Umepata mtoto, ina maana kwamba umekubali kwa hiari yako, kubeba msalaba wa malezi. Huyo kiumbe amekuja duniani kwa kibali chako, ingawa muwezeshaji ni Mungu. Kama kibali kimetoka kwako ni kwa nini usiweke misingi bora, itakayosimamia ukuaji wake?
Ni kosa kubwa kujiingiza kwenye matumizi mabaya ya fedha, wakati unatambua fika kwamba unachokitumia si cha kwako peke yako. Ulipoamua kuwa na familia, maana yake memba wa familia yako ni wanahisa kwenye kipato chako.
Kitendo cha kutumia fedha unazopata kwa fujo, ukiweka kiburi kwamba ni zako ni ubinafsi. Wengi waliojiwekea na hata wale wanaoendelea kujiwekea msimamo huo, hatma yao ni mbaya mno. Kwa kawaida hufilisika na familia ikiwa haina chochote.
Mifano ya mitaani ambayo tunaendelea kujifunza, kwamba baba alikuwa meneja wa benki kwa miaka 10 lakini baada ya kustaafu, familia ni hohehahe. Hata chakula mlo mmoja kwa siku unashindikana, watoto wanashindwa kuendelea na shule kwa sababu ya ada, ikupe fundisho kuhusu ubaya wa ubinafsi.
Hata kama hujawa na familia, jiwekee nidhamu kwamba kila unachoingiza ni kwa ajili yako na familia yako ijayo, kwa hiyo wekeza. Siku zote hakikisha unahifadhi fedha. Ishirikishe familia yako katika kuamua kuongeza kipato cha ziada na uwekezaji wa vitega uchumi kwa ajili ya maisha ya baadaye.
Achana na hulka mbaya kwa kujiona wewe ndiyo wewe kwa sababu una nguvu zako. Hapa duniani, hakuna mwenye mkataba na Mungu kuhusu afya na urefu wa maisha yako. Mungu anapoamua kuyafupisha maisha yako, utamuachaje mtoto wako?
Ikitokea Mungu anaamua kuiteteresha afya yako kidogo, utajivunia kitu gani? Upo hai lakini huna uwezo wa kutafuta fedha kwa sababu una ulemavu au maradhi ndiyo yamekuandama. Nawe ulipokuwa na nguvu zako, hukujua kama kuna kesho, uliteketeza kwa mbwembwe kila unachopata.
Afya, riziki, furaha na kila aina ya starehe unazoweza kuzipata leo, kwa jumla yake visikufanye ukashindwa kwamba wapo watu waliokuwa imara lakini leo hii wako vitandani na wengine wameshatangulia mbele za haki. Jambo moja tu, kabla ya hatma yako, unaiacha vipi familia yako?
Mohamed Ali alikuwa matata sana ulingoni. Akasifiwa kwamba ana mkono wa chuma kutokana na uzito wa makonde aliyokuwa anayashusha kuwaadhibu mabondia wenzake. Leo hii, bondia huyo hana uwezo wa kusimama hata dakika 10 kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya kutetemeka.
Hii ina maana kuwa endapo Ali asingewekeza katika maisha yanayokuja, angekuwa ombaomba lakini sivyo. Mpaka leo, bondia huyo ana utajiri unaofikia Dola za Marekani milioni 80, yaani kwa fedha za Kitanzania ni tajiri kwa shilingi bilioni 128. Yaani mabavu yake ya zamani, yametafsiri maisha yake ya leo. Afya si nzuri ila ni tajiri.
Mike Tyson ambaye alikuwa anaingiza shilingi bilioni 60 mpaka 70 kwa dakika kutokana na uwezo wake wa kuwaadhibu mabondia katika sekunde za raundi ya kwanza ulingoni, leo hii amebaki na utajiri wa shilingi bilioni moja. Yaani matumizi yake mabaya ya fedha, yametafsiri hatma yake mbaya.
Matokeo yake sasa, leo hii Tyson anajitahidi kuwa mbunifu ili aweze kuishi katika kiwango anachokitaka kulingana na hadhi yake. Kwa maana hiyo basi, ubinafsi ni mbaya, siku zote fanya kwa kutambua kwamba haupo peke yako ila upo na familia yako. Mwenzi wako wa maisha ni mwanahisa wa mshahara wako au kipato katika biashara zako. Vivyo hivyo kwa mtoto wako. Anza leo kukomesha kila aina ya ubinafsi, Usaliti, uchafu na hata Matumizi Mabaya.

www.globalpublishers.info

No comments: