ANGALIA LIVE NEWS

Monday, October 29, 2012

Uchaguzi wa madiwani vurugu tupu



UCHAGUZI mdogo wa Madiwani uliofanyika katika Kata 29 jana uliingia dosari baada ya vurugu kubwa kutawala katika sehemu mbalimbali na kusababisha watu kujeruhiwa.
Katika vurugu hizo, gari la Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Rachel Mashishanga liliharibiwa vibaya huko Shinyanga.
Mkoani Ruvuma, wafuasi wa Chadema na CCM walipigana mapanga na kusababisha saba kati yao kujeruhiwa vibaya na kukimbizwa katika Hospitali ya Mkoa, Songea.
Vurugu hizo zilizuka muda mfupi baada ya wafuasi wa vyama hivyo kupiga kura katika Kata ya Mletele kujaza nafasi ya aliyekuwa diwani wa kata hiyo, Legere Panya aliyefariki.
Mchuano mkali ulikuwa kati ya Maurus Lungu wa CCM na Leokardo Mapunda wa Chadema. Katika uchaguzi huo Lungu aliibuka mshindi kwa kura 955 na kumshinda Mapunda aliyepata kura 297.
Akizungumzia majeruhi, Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa, Dk Benedicto Ngaiza alisema: “Wanne kati yao walitibiwa na kuruhusiwa na watatu wanaendelea na matibabu huku mmoja wao akiwa (ICU), Chumba cha Wagonjwa wanaohitaji Uangalizi Maalumu.
Alimtaja majeruhi aliyelazwa ICU kuwa ni Mashaka Mbawala anayedaiwa kuwa mfuasi wa CCM ambaye aliumizwa vibaya mguu wake wa kulia na mkono wa kulia.
Majeruhi wengine wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Chadema ni Athuman Moyo na Nyenje Ally ambao waliumizwa kifuani na usoni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Deusdedit Nsimike hakupatikana kuzungumzia tukio hilo.
Huko Shinyanga gari la Mashishanga lilivamiwa na kundi la watu na kupigwa mawe.
Tukio hilo lilitokea jana asubuhi katika Kata ya Mwawaza, Shinyanga wakati gari hilo likitokea katika vituo vya kupigia kura.
Katibu wa Chadema mkoani Shinyanga, Nyangaki Shilungushela alisema gari hilo lilivamiwa na watu waliokuwa na mawe na kushambuliwa kabla dereva, Joshua Mashishanga kulikimbiza kutoka katika eneo hilo.

Alisema mmoja wa watu waliohusika katika tukio hilo amekamatwa na wengine wanatafutwa ili wafikishwe kituo cha polisi.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangala alisema hana taarifa kuhusu tukio hilo na kuhoji gari la Mbunge huyo lilifuata nini katika eneo la uchaguzi.

Katika uchaguzi uliofanyika katika Kata ya Darajambili mkoani Arusha, risasi zilirindima mfulululizo na kuzua taharuki kwa wakazi waliokuwa wamejitokeza katika vituo vya kupigia kura.
Risasi hizo zinadaiwa kupigwa na Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari na Mwenyekiti wa UVCCM, Wilaya ya Arusha, Godfrey Mwalusamba baada ya kuibuka ghasia baina ya wafuasi wa vyama vyao katika eneo la Shule ya Sekondari Felix Mrema.
Katika vurugu hizo wafuasi zaidi ya 15 wa Chadema walikamatwa na Polisi huku Nasari na aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini kwa tiketi ya Chadema, Godbless Lema wakitokomea kusikojulikana.
Hata hivyo, viongozi hao baadaye walionekana katika viunga vya kupigia kura.
Alipoulizwa juu ya tukio hilo, Nasari alikanusha kurusha risasi lakini Mwalusamba kwa upande wake, alikiri akisema alifanya hivyo kwa lengo la kujihami.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema ni mapema kuzungumzia tukio hilo ingawa alisema baadhi ya wafuasi wa CCM na Chadema wanashikiliwa kutokana na vurugu hizo.
Hadi tunakwenda mitamboni, Chadema kilikuwa kinaongoza katika kata nyingi za Jimbo la Arusha Mjini na wilayani Arumeru, katika Kata ya Bang’ata CCM kiliibuka na ushindi.
Wilayani Liwale, Lindi, watu watatu wakazi wa Kijiji cha Mpengele wamenusurika kufa baada kujeruhiwa vibaya, mmoja kuvunjwa mkono katika vurugu zilizoibuka wakati wakipiga kura. Waliojeruhiwa katika vurugu hizo ni Rajabu Mohamed (21), Said Mpengule (22) na Juma Lihambilo ambao wanaaminika kuwa ni wafuasi wa CUF.
Akizungumza akiwa Hospitali ya Liwale, Mohamed alisema kuwa alijeruhiwa na wafuasi wa CCM.
Mwananchi

No comments: