ANGALIA LIVE NEWS

Monday, October 29, 2012

UNAPOPEWA, JIULIZE UNATOA NINI? USIENDEKEZE MAPENZI YA KIZAMANI -2

WIKI iliyopita nilieleza kuwa sijawahi kuona mwanaume anamuacha mke kwa madai kwamba hachangii chochote kwenye pato la familia. Hii inatokana na ukweli kwamba imeshajengeka hivyo na ni ngumu kutengua kuwa mwanaume ndiye mtoa huduma, hata kama mke atakuwa anashinda nyumbani na kubadili saluni kwa kujipamba.
Wapo ambao hawataki wapenzi wao watoke kwenda kutafuta. Anataka akatafute peke yake halafu arudishe nyumbani akatumie na mama watoto wake. Ukweli ni kuwa aina hii ya watu, ni wale wanaosumbuliwa na wivu wa kupindukia. Anaogopa mpenzi wake akifanya kazi, ataibiwa.
Hata wanawake, wengine hawataki kuwa mbali sana na wenzi wao. Anachotaka ni muda mzuri wa kupumzika na mpenzi wake japo kipato kitakuwa kidogo. Anamaanisha wakiingiza kidogo tu kinatosha. Mwenzi wake akiwa mbali ni mgogoro. Atauliza: “Kazi sawa lakini na mimi nikae na nani muda huu?”
Siku zote nasimamia mapenzi na maisha. Inatakiwa wanaopendana wawe mstari wa mbele kupigania maendeleo yao. Hivyo basi, sikubaliani na mtindo wa kujifungia muda mwingi, badala ya kushirikiana katika kuongeza kipato. Inawezekana leo kinawatosha kwa sababu mpo wawili, mtoto akija je?
Ni lazima watu wafanye kazi kwa bidii. Kila mmoja aone anao wajibu wa kupambana kuongeza kipato kwa mwenzake. Hata kama huna kazi, je, unafanya nini kuhakikisha mpenzi wako hatetereki wakati anakuhudumia? Pengine mawazo yako yanajenga sana.
Usiwe mtu wa kukaa, kusubiri ufanyiwe kila kitu. Mtoto wa kike kazi yake kupiga mizinga. Anatendewa hili kesho anaomba lingine bila kujiuliza yeye anatoa nini kumwezesha mpenzi wake. Mtindo wa kungoja kupewa, hatari yake ni kubwa. Wapenzi wengi wameachana baada ya mmoja kuhisi anaelemewa na mzigo.
Kwa wanandoa ni afadhali lakini wapenzi ambao hawajaoana athari yake huwa ni kubwa sana. Inawezekana akajitahidi kutoa lakini utoaji unaendana na uwezo. Akihisi ni mzigo ataona afadhali na mapenzi yafe. Zingatia, kutaka kupewa bila kujiuliza wewe unachangia nini ni mapenzi ya kizamani. Tafadhali sana, usiwe wa kizamani.
Wakati unajiongeza kwamba unashindwa kubadilika kutokana na wakati, tambua kuwa mtindo wako wa kimaisha unakufanya uonekane mzigo mzito kwa mwenzio. Tambua kuwa mzigo huwa haukumbatiwi, kwa kawaida aliyeubeba hutamani kuutua. Akifanikiwa kuutua, hupumua.
Kwa mantiki hiyo, tabia zako zinaweza kumfanya mpenzi wako ajisikie amani siku akiachana na wewe. Na kwa kukuongezea ni kwamba hakuna kitu kibaya kama mwenzi wako aone nafuu ya kuwa bila wewe, hapo ni lazima ujue kuna matatizo ambayo yapo ndani yako.

NI ASILI MBAYA
Mtu ambaye anataka apewe zaidi, mara nyingi anakuwa na kasoro za kimaumbile. Huyo anakuwa ni mbinafsi kwa sababu chake kinakuwa ni cha kwake peke yake lakini cha mwenzake anataka kukiwekea sauti. Mara nyingi wanakuwa hatari kwa sababu husumbuliwa na nongwa.
Atataka apewe hata kikiwa hakipo. Anapokosa huhisi kanyimwa. Mtu wa aina hiyo siyo tu kwamba hafai kwenye mapenzi bali hata kwenye maisha ya kawaida kijamii. Hachangii wenzake wanapokuwa wanahitaji michango lakini yeye asipochangiwa ni nongwa.
Mapenzi ni jinsi ambavyo moyo unaridhika, inapotokea mtu anaanza kujiuliza maswali mengi kuhusu mpenzi wake, maana yake anakuwa anamtilia wasiwasi. Pale wasiwasi unapoendelea ndivyo na kiwango cha mapenzi hupungua. Hali hiyo inapozidi, mapenzi hufa kabisa.
Hujawahi kuona watu wanaishi, kila mtu anajua ni wapenzi lakini ndani yao ni kama hakuna kupendana. Yaani wanaishi kwa mazoea tu! Moja ya sababu za wapenzi kufikia hatua hiyo ni mmoja kumuona mwenzake ni mzigo mzito kuubeba. Yaani anakuwa amemkinai.
Tabia hiyo ni sumu hatari kwa maana wapo walioshindwa kupata wenzi wa maisha yao, kwani kila mmoja alimkimbia. Maisha magumu lakini wewe hutaki kutambua hilo, badala yake unataka mahitaji lukuki. Unapaswa kujiuliza wewe umefanya nini?
Angalau basi, kama wewe ni wa kupewa, ufanye juu chini kuhakikisha unapunguza matumizi. Ila wewe ndiye mkali wa kuongeza mahitaji. Ni rahisi kuachwa kwa sababu mtoaji atakapoanza kujiuliza, mwisho wa maswali yake atapata jibu kuwa wewe ni mnyonyaji.

CHUKUA MUONGOZO HUU
Hebu ishi kwa mtindo wa kula na kipofu. Yeye anakupa, sasa kazi kwako kuhakikisha unampa faraja na amani. Ana fedha, wewe huna, kwa hiyo mahitaji yako yanamtegemea yeye, jitahidi kujikomboa ili nawe uwe unaingiza kipato cha kukutosheleza na wakati unapigania hilo, hakikisha unakuwa faraja yake.
Itaendelea wiki ijayo.

www.globalpublishers.info

No comments: