Siku mbili baada ya chama cha walimu (CWT) wilayani hapa kudai kuwa mishahara ya walimu ambao ni marehemu bado inakuja na huenda inaliwa na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, mweka hazina wa Halmashauri hiyo amekanusha tuhuma hizo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana mweka hazina wa halmashauri ya wilaya hiyo, Peter Msamba, alisema hakuna mishahara ya marehemu ambayo inakuja na kuliwa na watumishi wa halmashauri hiyo kama inavyodiwa.
Msamba alisema Halmashauri hiyo imekuwa ikizuia mishahara ya marehemu ambao walikuwa ni watumishi wa halmashauri hiyo inapokuja, ili isingie kwenye akaunti zao na kwamba imekuwa ikirejeshwa hazina makao makuu.
Alisema mtumishi anapofariki taratibu zimekuwa zikifanyika, kupitia kwa mkuu wa idara husika kwa ajili ya kuzuia mshahara wake, ambapo pia idara ya utumishi imekuwa ikipeleka majina ya watumishi ambao ni marehemu kwa menejimenti ya utumishi wa umma, ili waweze kufutika kwenye malipo ya mishahara (Payroll).
“Mimi ndiye mweka hazina wa halmashauri, nakuhakikishia kwamba hakuna mishahara ya marehemu ambayo inakuja na kuliwa kama inavyodaiwa, mishahara hiyo inapokuja uwa tunaizuia na kuirudisha hazina makao makuu,” alisema.
Kuhusu baadhi ya watumishi kufutika kwenye malipo ya mishahara, Msamba alikiri kwamba tatizo hilo lipo na kwamba liko juu ya uwezo wake lakini halmashauri hiyo inaendelea kulishughulikia na kuongeza kuwa tatizo hilo si la Bunda tu bali ni la nchi nzima na serikali inaendelea kulishughulikia.
Awali akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa CWT wilayani hapa, Francis Ruhumbika, alisema zaidi ya walimu 13 ambao ni marehemu bado mishahara yao inakuja na huenda inachukuliwa na baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo.
Ruhumbika aliwataja marehemu hao na cheki namba zao kwenye mabano kuwa ni Nchagwa Fransic (854300), Bahati Manyerero (5929742), Dominico Turo (5204571), Sospeter Msheri (7373017), Elizabeth Mtatiro (4442064) na Felex Mwaipopo (10569522).
Wengine ni Zabron Mafweko (5206494), Clavery Maiga (625788), Salvatory Tungaraza (8733436), Wambura J. Wambura (6260945), Milingo J. Kitanga (6792095) na Akelo O. Wilson (8856638).
Kufuatia hali hiyo CWT wilayani hapa imetangaza maandamano ya walimu wote yatakayofanyika Novemba 16 mwaka huu, ikiwa ni pamoja na kuishinikiza Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, kulipa madeni ya walimu yanayofikia zaidi ya Sh. bilioni 1.1, wakiwemo waliofutika kwenye malipo ya mishahara baada ya kuhakikiwa na serikali katika zioezi la kubaini watumishi hewa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment