ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 9, 2012

Busara kumlipa fedha zote Bi Kidude

Yussuf Mahmoud akizungumza na waandishi wa habari kujibu madai yaliotolewa na Mpwa wa Msanii Mkongwe wa Taarab Zanzibar, Fatma Binti Baraka (Bi Kidude) aitwae Baraka Abdallah kuhusiana na kuwa Busara imeshindwa kumlipa msanii huyo
UONGOZI wa Sauti za Busara Zanzibar umesema wapo tayari kurejesha fedha zote za Bi Fatma Bint Baraka (Bi Kidude) zilizobaki ambazo ni Dola za Kimarekani 2,000 zilizobaki katika akaunti ya Msanii huyo Mkongwe huku Mtoto wa Bi Kidude akitoa shutuma kali mbele ya Uongozi huo kuwa mama yake amekuwa akidhulumiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la Zamani Mjini Unguja Meneja wa Busara Promotion, Yussuf Mahmoud aliwaambia waandishi hao lengo la kuitisha kikao hicho na kukanusha taarifa zinazosambazwa na vyombo vyahabari mbali mbali ambazo zimekuwa zikiwashutumu kuwa wanamchukulia fedha zake Bi Kidude.

Meneja huyo alisema Busara wapo tayari kurejesha fedha hizo kwa Bi Kidude mbele ya mwanasheria na mtu ambaye atatoa atapewa idhini na Bi Kidude mwenyewe kwa kuwa kumekuwepo na malalamiko mengi ambayo yanatolewa na mwana familia Bakara Abdallah ambaye ni Mpwa wa Bi Kidude anayeishi naye tokea kuanza kuumwa kwake.
“Uongozi wa Busara upo tayari kukabidhi fedha zote za Bi Kidude hivi sasa lakini tutakapopata idhini yake nani tumkabidhi tutamkabidhi Dola 2,000 kwa familia ya Bi Kidude ambazo zipo katika account ya Bi Kidude na hivi fedha atakabidhiwa mbele ya mwanasheria” alisema Yussuf ambaye amekuwa akishutumiwa kunifaika na fedha za Bi Kidude.
Yussuf alisema “Uongozi wa sauti za Busara unatoa taarifa kuhusu madai ya Mpwa wa Bi Kidude anayejulikana kwa jina la Baraka kupitia vyombo vya habari. Sauti za Busara inapinga madai yaliotolewa na Baraka dhidi yake na inapenda kutumia fursa hii kuufahamisha umma habari za uhakika” alisema
Akizungumzia suala hilo hilo Meneja Mradi wa Busara, Jaurney Ramadhani alisema madai yanayotolewa sio sahihi kwa kuwa Bi Kidude wakati wa uzima wake huwa anakwenda kuchukua fedha “Miaka hiyo Bi Kidude alikuja na Bwana Baraka ofisini za Busaraakamtambulisha kwetu na akasema kuanzia sasa Baraka atakuwa anakuja kuchukua pesa yangu ya kila wiki 50,000. huu ndio ulikuwa mwanzo wa kumjua Baraka Abdallah” alisema Ramadhani.
Naye Mtoto wa Bi Kidude wa kulea, Suweid Eigli alisema yeye anafahamu kwamba Mama yake huyo (Bi Kidude) amekuwa akidhulumiwa kwa kuwa anafanyishwa kazi za sanaa bila ya kulipwa fedha zinazostahiki na alipojaribu kuulizia akauti ya Bi Kidude ina kiasi gani cha fedha hakuwahi kujibiwa.
“Bi Kidude alikuwa anawekewa fedha zake kweli hatukatai lakini kuna watu wanajinufaisha kwa maslahi yao na wengine siwataji lakini wanamchukua na kumfanyisha kazi wakiwemo wamiliki wa vituo vya televisheni na radio hapa nchini, lakini mimi mwanzo wa kutoelewana na Yussuf mimi nilimuuliza kwani kiasi gani cha fedha kimo katika account ya Bi Kidude? Jibu sijalipata mpaka leo hii” alisema Eigli.
Eigli alisema amesikitishwa sana kuona Mama yake huyo akiwa mgonjwa na hakuna anayeguswa na ugonjwa wake kwa kuwa ametumia maisha yake katika sanaa na kujituma lakini wenye kunufaika ni wengine, “Inaniuma sana ninapoona Bi Kidude anaishi maisha yake mimi lazima iniume kwa sababu ameninyonyesha mie amaenilea na kunionesha dunia lakini nisema tu kuwa nimefukuzwa kwa sababu nimeonekana nitarithi nyumba ya Bi Kidude kwa kweli inaniuma sana sana” alisema huku akionesha huzuni.
Alisema jamaa za Bi Kidude wamemfukuza ndani ya nyumba ya Bi Kidude wakiamini kwamba atafaidi endapo Bi kidude akifa na atapata kumuandikia nyumba ambayo anaishi naye.
Kikao hicho ambacho walialikwa waandishi wa habari kuja kusikiliza madai yaliotolewa na familia ya Bi Kidude kimeingia doa baada ya mtoto wa kaka yake Bi Kidude aitwae Baraka ambaye analalamikiwa na ndiye aliyemchukua Bi Kidude na kumhudumia wakati huu kudaiwa kuwa amekataa kufika katika kikao hicho.
“Sauti za Busara haina kinyongo na Baraka wala familia yake ila tunachoshangaa ni kwa nini hataki kuja ofisini ili aelezwe story nzima ya mahusiano kati ya Yussuf na Bi Kidude kwani inafahamika ni mtu ambaye amejitokeza kipindi hiki cha hivi karibuni na hajui story ya Bi Kidude na Yussuf” amesema Ramadhani.
Akizungumzia kuhusu Busara kushindwa kulipia fedha za matibabu za Bi Kidude Ramadhan alisema katika kikao hicho kwamba Busara imejaribu kumlipia gharama za matibabu aliyokuwa akidaiwa katika hospitali ya shilingi 270,000 baada ya familia kutaka fedha hizo zilipwe.

No comments: