Ukishindwa kudhibiti hisia zako, inaweza kukusababishia kushindwa kutimiza majukumu yako ya kila siku vyema. Usaliti ni tatizo kubwa sana rafiki zangu. Lakini vipi, umeshawahi kufikiri juu ya kugundua kabisa kwamba unasalitiwa?
Umewahi kufikiria...unampigia simu mpenzi wako, halafu anapokea mtu wa jinsia nyingine tena usiku wa saa sita nini kinatokea? Mathalani umekwenda kwa mpenzi wako usiku kwa kumshtukiza, halafu unamkuta yupo na mtu ndani, utaumia kiasi gani?
Hata hivyo, maumivu siyo mwisho, machozi yako siyo suluhisho, lazima uende hatua moja zaidi ya hapo. Haya ni mambo ambayo yanaweza kutokea katika uhusiano, umejiandaaje? Umegundua wazi kuwa mwenzako anakusaliti, unajua unapaswa kufanya nini? Au wewe unadhani ungefanyaje?
Je, ungejiua? Ungeachana naye? Yote hayo siyo suluhisho la kudumu. Kote huko kuna matatizo yake, lazima upate suluhisho moja la kumaliza kabisa tatizo hili.
Nimekuwa nikitoa ushauri kwa watu wengi sana kuhusu masuala ya mapenzi, ndoa na elimu rika. Siku moja nilipokea simu ambayo ndiyo iliyonisukuma hasa kuandaa mada hii. Ilikuwa ni simu kutoka kwa mama mmoja ambaye alilalamikia kuhusu kusalitiwa na mumewe.
Katika mazungumzo yetu, alisema: “Mimi ni mama mwenye watoto wanne, naishi na mume wangu kwa miaka 15 sasa, mume wangu si mwaminifu na nimegundua kwamba anatoka nje ya ndoa yetu tangu mwaka 2004.
“Lakini kila nikimuuliza anakuwa mkali, wakati mwingine hunipiga au kunipeleka nyumbani kwa ndugu zake. Baadaye alikwenda kusoma kozi fupi ya miezi sita, aliporudi akaanza tena tabia yake ya kurudi nyumbani usiku, wakati mwingine hadi saa sita!
“Ninapompigia simu usiku akiwa amechelewa, anasema yupo ofisini. Lakini kuna siku nilimuomba simu yake, nikaanza kupekua meseji, nikakutana na sms chafu, nilipomuuliza juu ya sms zile, akasema kama anataka aniambie ukweli, basi nimuahidi kumsamehe.
“Kwakuwa nilikuwa nataka kujua ukweli, nikamwambia nitamsamehe, ndipo aliponiambia kwamba zile meseji zilikuwa za dada mmoja hivi (nahifadhi jina lake) jirani yetu na alikiri kuwa na uhusiano naye wa kimapenzi.
“Sikufanya fujo yoyote, hadi leo sijamwuliza chochote, lakini nataka kuachana naye ili niangalie maisha yangu maana tabia yake ya kurudi nyumbani usiku bado hajaacha. Tangu tuoane sijawahi kumsaliti hata siku moja na wala sitarajii kufanya hivyo.
“Sitaki mwanaume yeyote kwa sasa, natamani kuishi mwenyewe. Naomba ushauri wako kaka Shaluwa. Kichwa hakifanyi kazi sawasawa, pia sina raha katika ndoa zaidi ya kero tu! Nisaidie tafadhali kaka yangu.”
Hayo ndiyo maneno ya dada yetu huyo ambaye kwake, maisha ya ndoa ni machungu kuliko kawaida. Ni imani yangu kwamba, wapo wengine wenye matatizo kama ya huyu dada.
Wiki moja baadaye niliandika mada iliyotoka katika gazeti damu moja na hili la Risasi Mchanganyiko ambapo nilimshauri yule dada moja kwa moja. Yawezekana na wewe upo katika tatizo kama la dada yetu huyo, huna haja ya kulia na kuhangaika. Ipo dawa.
Kwa faida ya wote, wenye tatizo kama hilo na hata wale ambao hawana, lakini kwa sababu wote tupo kwenye sayari ya mapenzi, inawezekana kabisa yakakukuta. Sasa hapa tutapata darasa.
Ushuhuda huu uwe utangulizi kwako katika kusoma kwa upana na kujifunza zaidi juu ya usaliti. Natamani sana kuendelea na mada yetu leo, lakini kutokana na ufinyu wa nafasi, kwa leo naomba kuweka kituo kikubwa hapa, wiki ijayo tutaendelea, USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.
No comments:
Post a Comment