ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, November 13, 2012

JINSI VYAKULA TULAVYO VINAVYOTUMALIZA - 6

VYAKULA vinavyotumaliza na tutazungumzia vitafunwa; endelea.
Hali hii haiko kwenye mkate peke yake, bali iko karibĂș kwenye vitafunwa vyote ambavyo ndivyo vyakula vikuu vya familia nyingi nchini. Vitafunwa hivyo ni pamoja na chapati, ‘skonzi’ ambazo nazo hutengenezwa kutokana na ngano iliyoondolewa virutubisho vyake baada ya kukobolewa. Utaona ni jinsi gani tuko hatarini kwa kupenda kula kila siku vyakula vinavyotuangamiza.

Katika hili, tunashauriwa kula mkate unaojulikana kama ‘mkate mweusi’ au ‘Brown Bread’, wenyewe kidogo una nafuu kutokana na kutengenezwa na ngano isiyokobolewa na huwa haiongezwi sukari au makorombezwo mengine. Ingawa kwa ladha mkate huu siyo mzuri mdomoni, lakini kiafya ni bora na mzuri uingiapo tumboni kwa sababu una kamba lishe za kutosha.
Halikadhalika, wanaopenda kula chapati, maandazi na sikonzi, wanashauriwa kutumia unga wa ngano isiyokobolewa ili kujiepusha na madhara yatokanayo na ulaji wa nafaka zilizokobolewa. Tupende kuthamini sana vyakula vyenye faida mwilini hata kama havina ladha nzuri mdomoni, kuliko kupenda kula vyakula vyenye ladha nzuri mdomoni lakini vyenye madhara tumboni.

STAILI HII YA MAISHA NDIYO SABABU ZA WEWE KUUGUA MARA KWA MARA
Baada ya kuelezea aina ya vyakula tunavyopenda kula na kuona namna vilivyo hatari kwenye miili yetu, hebu tuangalie staili ya ulaji ya baadhi ya watu kuanzia asubuhi hadi mlo wa usiku, kila siku na kwa maisha yao yote.
Usemi usemao kuwa ‘jinsi ulivyo, kunatokana na unavyokula’, una maana kubwa. Baada ya kuangalia ratiba hii utaweza kujijua uko kundi gani na pia utajua kwa nini hali yako ya kiafya ni dhaifu.

Wako baadhi ya watu na ndiyo familia nyingi, huanza asubuhi kwa kutia tumboni vyakula ambavyo siyo tu havina viini lishe au virutubisho vyovyote, bali vyenye hatari kwa ustawi wa afya zao.
Mfano, unaamka asubuhi huku kitu cha kwanza kuingia tumboni mwako kinakuwa chai ya rangi iliyoungwa kwa vijiko vitatu mpaka vinne vya sukari, kitafunwa ni mkate, chapati au maandazi. Baada ya kunywa chai, pengine unashushia na soda au juisi za rangi.
Mchana unawadia, unakula ugali wako uliopikwa kwa unga wa sembe nyeupe na nyama. Wengine mchana watakula wali wa pilau ya nyama ya ng’ombe na baada ya mlo watasindikizia na soda. Au wengine watakula chips kuku au mayai. Vyote ni vya kuku wa kizungu.
Awamu ya mwisho inakuwa ni mlo wa usiku, ambao nao kwa aliyekula ugali mchana, labda usiku atakula wali na aliyekula wali pengine ataamua kubadili kwa kunywa chai na mkate mweupe au chai na chapati, au kurudia tena chips mayai.
Kwa zile baadhi ya familia zenye kipato, asubuhi huweza kuanza kunywa chai ya maziwa yenye sukari mpaka ya ‘kujilamba’ ikisindikizwa na mayai ya kukaanga kwenye mafuta kibao, na kisha kushusia na juisi ya boksi. Mchana ukapita kwa kula pilau ya kuku wa kizungu na kushushia na bia na usiku labda ukala chapati na mchuzi wenye mafuta kibao na mapochopocho mengine ya kukaanga kisha kushushia na ka mvinyo kidogo.
Kwa mtizamo wa kawaida, utaona ulaji wa vyakula vyenye mafuta, sukari nyingi na vilivyonona ndiyo maisha bora, lakini kwa upande mwingine ulaji wa vyakula vya aina hiyo huwa ndiyo chanzo kikuu cha maradhi hatari ya moyo, saratani, kisukari na unene wa kupindukia.
Itaendelea wiki ijayo.

No comments: