ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 9, 2012

Mwakyembe avunja Bodi ya Bandari



Miezi mitatu baada ya viongozi wandamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) wasimamishwe kazi kwa tuhuma za kutokana na vitendo vya ufisadi, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ameifuta uteuzi wa wajumbe wote wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka hiyo na kuteua wapya.
Agosti mwaka huu, Dk. Mwakyembe alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Ephraem Mgawe maofisa wengine waandamizi sita wa bandari kwa tuhuma hizo na kuunda kamati ya uchunguzi.

Hata hivyo, kabla hajaweka hadharani ripoti ya uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili viongozi waliosimamishwa baada ya kamati ya uchunguzi kumkabidhi, Dk. Mwakyembe ameifumua Bodi ya Wakurugenzi wa TPA kwa kuwaondoa wajumbe sita wa zamanai na kuteua wapya wanane.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana, uteuzi huo ulianza Novemba 6, mwaka huu na kwamba Waziri amechukua uamuzi huo kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa chini ya kifungu cha 6(2) cha sheria ya Bandari na kifungu cha 1(2)(i) cha jedwali la kwanza la sheria ya Bandari ya mwaka 2004.
Walioteuliwa kuingia katika bodi hiyo ni Dk. Jabiri Bakari, John Ulanga, Caroline Temu, Jeffer Machano, Dk. Hildebrand Shayo, Saidi Sauko, Mhandisi Julius Mamiro na Asha Nassoro.
Hata hivyo, kwa mujibu wa sheria, uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi hufanywa na Rais.
Kabla ya uteuzi huo, waliokuwa wajumbe wa bodi hiyo ambao sasa wameondolewa ni Dustan Mrutu, Mhandisi George Alliy, Mtutura A. Mtutura, Emmanuel Mallya, Mwantumu Malale na Maria Kejo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mabadiliko hayo ni sehemu ya hatua ambazo Wizara hiyo imechukua kurejesha ufanisi katika mamlaka hiyo ili iweze kuchangia zaidi kwenye pato la Taifa.
Kufuatia uteuzi huo mpya, Dk. Mwakyembe ameiagiza Menejimenti ya TPA kuwakabidhi nyaraka zote muhimu wajumbe wapya wa bodi ili wajiandae kabla hajakutana nao ndani ya siku 10 kuwapa maelekezo ya kazi za kufanya.
Hata hivyo taarifa hiyo haikueleza sababu za bodi hiyo kufutwa.
Vigogo wengine waliosimamishwa sambamba na Mgawe Agosti mwaka huu, ni Julius Mfuko (Maendeleo ya Miundombinu); Hamad Kashuma (Huduma); Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Cassian Ng'amilo na Mameneja wawili wa bohari ya mafuta Kurasini Oil Jetty (KOJ) na Mhandisi wa bohari hiyo.
Viongozi hao wa TPA walisimamishwa kwa muda ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zinazowakabili ikiwamo wizi wa makontena, wizi mkubwa wa mafuta, udokozi wa mizigo na rushwa katika utoaji wa huduma.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

FANTASTIC!
THIS IS WHAT HAS BEEN LACKING OVER MANY YEARS!!!
LEADERSHIP!!! REMOVE THESE STINKING AND CORRUPTION-MINDED PEOPLE AND LET WORK BE SEEN FOR THE BENEFIT OF THE COUNTRY!
VIVA TANZANIA !!!

MDAU WA NORTH CAROLINA, USA