
Katika utangulizi wa mada hii wiki iliyopita tuliona mambo waliyokutana nayo wasomaji wenzenu ambao walipata kuwasiliana nami wakiomba ushauri. Wenzi wao wanawang’ang’aniza kufanya ngono, wakidai kufanya hivyo ndipo watakapoamini kuwa kweli wanapendwa!
Jambo hili halina ukweli hata kidogo. Yaani utakuta msichana ameutunza usichana wake kwa miaka mingi, halafu eti auharibu kwa mtu mwenye tamaa zake kisha aachwe? Usikubali kabisa....ni afadhali uendelee kusubiri mpaka kwenye ndoa.
Heshima ya usichana wako ni zawadi nzuri sana kwa mwanaume ambaye ameitambua thamani yako na kuamua kufunga ndoa na wewe. Huyo ndiye anayestahili. Ikiwa utaamua kwa hiyari yako kutoa penzi, ni wewe tu, lakini isiwe kwa sababu ya kuonesha mapenzi.
Kimsingi hakuna ulazima wa kukutana kimwili ili kudhihirisha penzi la dhati. Ngono ni kitu kingine na mapenzi ni kitu kingine. Hivi ni vitu viwili ambavyo havina uhusiano wowote.
Asitokee mtu akakudanganya kwamba kwa kutoa penzi ndipo utaonesha unavyompenda. Si kweli. Kimsingi ngono huja baada ya tamaa kuingia kati ya wawili wanaopendana.
Hata hivyo, kuna uwezekano mkubwa, ukawa na tamaa ya kufanya ngono na mtu hata kama huna mapenzi katika moyo wako. Suala la kufanya ngono siyo kithibitisho cha kuonesha mapenzi ya dhati.
Baadhi ya walio katika uhusiano, hudanyanywa na kipengele hiki. Utakuta msichana anaambiwa na mpenzi wake kwamba ili aoneshe kuwa anampenda basi lazima akubali kufanya naye ngono. Wangapi wanadanganywa na kuachwa? Ukiwa mmoja wao, utalala na wangapi?
WAKATI NI UPI?
Kimsingi suala la kufanya mapenzi halina kanuni, hakuna muda maalum wa kuanza kufanya mapenzi na mpenzi wako mpya. Ngono ni hisia tu, tena basi huwa bora zaidi kama hisia hizo zikaja kwa wakati mmoja kati yako na huyo unayempenda.
Wataalamu wa saikolojia ya mapenzi, wanashauri wapenzi wasishiriki tendo hilo mpaka pale watapokuwa wamefahamiana kiasi cha kutosha juu ya tabia zao na historia walizopitia. Pamoja na hayo, suala la ngono halikwepeki ikiwa mtaruhusu kukutana sehemu tulivu mkiwa wawili.
Jambo la msingi ni kutulia na kujipanga, msifanye ngono kama sehemu ya mapenzi. Tambua kuwa ngono ni kitukingine na mapenzi ni kitu kingine. Hata kama mtakuwa mmeamua kushiriki kitendo hicho, mfahamu kuwa mnastarehesha nafsi zenu tu na siyo kuoneshana mapenzi ya dhati.
UKWELI NI HUU
Tafiti mbalimbali za wataalamu wa mambo ya uhusiano, zinaonesha kuwa wengi walio katika uhusiano huwa hawawezi kuvumilia kuendelea kuwepo katika uhusiano bila ya kufanya mapenzi.
Hata hivyo, tafiti hizo za uhakika zinaeleza kuwa baada ya wapenzi kufanya ngono, ile hamu ya kuendelea kuwa pamoja hupungua! Hiyo husababishwa na dharau za kimaumbile na kujihakikishia kuwa hakuna kitu asichokijua kwa patna wake.
Wengi hulia baada ya kujikuta wakiingia katika mkumbo huu. Hebu jiulize, kama anakupenda, kwa nini ang’ang’anie kufanya mapenzi haraka? Wewe ni wake na huenda mna ndoto za kuishi pamoja siku moja, kwa nini asivumilie mpaka wakati huo? Akitaka anaweza kuvumilia na kufaidi mambo hayo mkiwa katika ndoa.
DHIHIRISHA PENZI LAKO...
Yapo mambo mengi sana ya kufanya badala ya ngono, huna sababu ya kutoa kipaumbele kwenye ngono wakati kuna vitu vingine vingi unavyoweza kuvifanya na kuyafanya mapenzi yenu yakaendelea kudumu mkiwa na matarajio mazuri yajayo.
Mnaweza kukaa sehemu nzuri yenye utulivu kwa ajili kupanga maisha yenu ya baadaye. Epukeni sehemu zenye vificho, ambazo zinaweza kuwapa vishawishi vya kufanya mapenzi. Lakini pia, kutoka pamoja hususan wikiendi hunogesha zaidi mapenzi.
Kutumiana zawadi ni njia nyingine ambayo inaweza kunogesha penzi lenu na kuweka mambo ya ngono pembeni. Amini usiamini rafiki yangu, suala la faragha si muhimu sana katika uhusiano hasa unapokuwa mchanga.
Mkifikia uamuzi huu ni lazima wote wawili mjadiliane na kufikia muafaka kabla ya kukimbilia, mwishowe ukaingia kwenye majuto. Nasisitiza kusema kwamba, uamuzi wa kila kitu uko mikononi mwako.
Mada imeisha, wiki ijayo nitakuja na somo lingine, USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.
No comments:
Post a Comment