POLISI mkoani hapa wamefanikiwa kuipata simu ya upepo ‘radio call’ iliyokuwa ikitumiwa na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, marehemu Liberatus Barlow ambayo ilichukuliwa baada ya kuuawa kwa kupigwa risasi usiku wa manane eneo la Minazi Mitatu Kitangiri.
Mbali na simu hiyo, jeshi hilo pia limefanikiwa kupata ufunguo wa gari la marehemu Barlow ambaye aliuawa wakati akimsindikiza mwanamke mmoja aliyeitwa Doroth Moses walipokuwa wakitoka kwenye kikao cha harusi ya ndugu yake.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Lili Matola, alisema jana kwamba vitu hivyo vilipatikana vikiwa vimefichwa katika shimo la majitaka katika nyumba moja iliyopo maeneo ya Nyashanya.
Pia jeshi hilo limefanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa wengine wawili wanaodaiwa kuhusika katika mauaji hayo na Kamanda Matola alisema wataunganishwa kizimbani na wengine watano Novemba 15, mwaka huu.
Alisema watuhumiwa hao wawili (majina tunayahifadhi kwa sasa), mmoja wao akiwa ni ndugu wa mtuhumiwa namba moja katika mauaji hayo, ndio waliotaja sehemu vilikokuwa vimefichwa vitu hivyo baada ya kuhojiwa.
“Baada ya kuonyesha vilipokuwa vimefichwa, ilibidi kumtaarifu mwenye nyumba ambaye alitoa idhini ya kubomolewa kwa shimo hilo la majitaka na mmoja wa watuhumiwa aliingia na kutoa ‘radio call’ pamoja na funguo za gari la marehemu,” alisema Kamanda Matola.
Alisema kuwa baada ya kutekeleza mauaji hayo, mtuhumiwa namba moja alitoa maelekezo ya wapi pa kuficha vifaa hivyo. Kabla ya kuficha simu hiyo, waliitenganisha na betri yake.
Kamanda Matola alisema katika msako waliofanya nyumbani kwa watuhumiwa hao, pia walikuta sare za moja ya kampuni ya ulinzi pamoja na magwanda ya mgambo.
Alisema kuwa vitu vingine vilivyokamatwa ni kofia mbili, moja ikiwa ya polisi na nyingine ya kampuni ya ulinzi pamoja na vifaa mbalimbali vinavyotumika kwa ajili ya kufanyia uhalifu.
Alisema mmoja wa watuhumiwa aliwahi kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, alichokitumikia kuanzia mwaka 2006 baada ya kukutwa na makosa ya unyang’anyi kwa kutumia silaha. Hata hivyo, alisema aliachiwa huru mwaka 2010 baada ya kukata rufani Mahakama Kuu na kuachiwa huru.
Alisema katika mahojiano na polisi, mtuhumiwa huyo alisema alishawishiwa na kaka yake kufanya kazi hiyo ya ujambazi.
Mbali na watu hao, Matola alisema polisi pia inamshikilia mtu mmoja (jina tunalihifadhi) mkazi wa Nyakabungo akituhumiwa kufadhili kundi hilo la majambazi.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment