Na Alex Kassuwi
Ndugu zangu ni vizuri kuambiana mambo ya msingi haswa linapokuja swala la hatma ya Taifa letu.
Tanzania ni nchi ya kipekee duniani na watu wake ni wa kipee pia, utu wetu , utanzania wetu huwezi pata sehemu nyingine. Watanzania ni watu wenye upendo, amani na mshikamano huwezi linagnisha na nchi yoyote ile. Tumekuwa tukiishi siku zote kwa amani, kupendana na kushirikiana kabla na hata baada ya kuasisiwa taifa letu. Lakini baada ya kuingia siasa za upinzani nchini mwetu , kumekuwa na fikra zenye kuhatarisha amani yetu. Hatukatai upinzani, ndio maana kumekuwa na vyama vingi vya siasa nchini Tanzania. lakini kamwe hatutaruhusu amani yetu kupotea na siasa za kutubagua. Hadi hapa, Amani na maendeleo yaliyopoTanzania yametokana na uongozi wa chama cha mapinduzi. Kuanzia kwa wazee wetu waasisi, na viongozi wetu wakiongozwa na Mwenyekiti wetu, Rais wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete. Kwa siasa safi na uongozi makini, Sina budi kuzitaja sababu 5 kwa nini chama cha mapinduzi kitashinda uchaguzi wa 2015.
Moja; CCM imeweza kulinda na kudumisha Uhuru wa Nchi yetu na raia wake.
Muhimu kwa watanzania wote kukumbuka kwamba chama cha mapinndizi hakina udini wala ukabila kwa misingi hiyo kimeweza kudumisha amani na umoja wa nchi yetu.
Mbili; CCM imekuwa ya kwanza katika ushirikishwaji wa watanzania wote walio nje ya nchi katika kutoa mchango wao ili kuleta tija na maendeleo ya taifa letu.
Tatu; CCM imehakikisha kwamba Nchi yetu inatawaliwa kwa misingi ya kidemokrasia. Nchini Tanzania kuna demokrasia ya kutosha na hata kupitiliza. Mwananchi yoyote anao uhuru wa kuishi, kuabudu na kufanya maamuzi apendayo ili mradi sheria za nchi zinazingatiwa.
Nne; CCM haina ubaguzi, kila mtu anayo nafasi. Chama cha mapinduzi siku zote kimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba Serikali na vyombo vyote vya umma vinatoa nafasi zilizo sawa kwa raia wote, wanawake na wanaume bila kujali rangi, kabila, Dini, au hali ya mtu.
Tano; CCM iko mstari wa mbele katika kuimarisha uhusiano mwema na Vyama vyote vya Siasa vya Nchi nyingine vyenye itikadi kama ya CCM ambavyo kweli vinapinga Ukoloni, Ukoloni Mamboleo, Ubeberu na Ubaguzi wa aina yoyote.

3 comments:
Ndugu Kassuwi,mtazamo wako wa mawazo ni mzuri kwa kiasi fulani. nafikiri ni vizuri ukatumia vyombo vya habari kuelimisha jamii badala ya propaganda. kwanza kabisa ingekuwa busara kujua katiba ya nchi yako,nchi inaendeshwa na katiba na ndio nguzo ya nje.hakuna chama chochote cha siasa tanzania kina udini sababu katiba ya nchi imeweka bayana hilo. sijui wewe amani inayoizungumzia ni ipi,tanzania ya waasisi wetu sio hii ya leo. unakumbuka waasisi wetu moja ya nguzo kuu ilikuwa rushwa ni adui wa haki. maana yake ni nini!! haki hainunuliwi ni wajibu wa kila mtanzania kupata haki bila kununua. maendeleo ni nini!! kila mtanzania aweze kuishi katika pato la kati(middle class),lakini sasa hatuna middle class. tuna matajiri na maskini. kusema ccm imekuwa msstari kushikirikisha wananchi walio nje hiyo sio sahihi,kwa misingi hii,moja ccm inaogoza kuwa na wabunge wengi(majority)wameshindwa kupitisha /kuleta mjadala wa kujadili dual citizenship. acha kutania watanzania walio nje!!! unasema ccm inaleta mshikamano umepata kusikiliza hotuba za viongozi wenu zanzibar wanavyotukana matusi ya nguoni hata siwezi kuyarudia. nenda kaangalie au sikiliza hotuba za viongozi wenu zanzibar za november 4,2012. acha kutumia vyombo vya habari kwa propaganda.kumbuka ni utanzania kwanza,pili ndio chama(ccm)kama kweli wewe unaipenda nchi yako na unataka iendelee.niko tayari kwa mjadala kama utakwa sio propaganda. ni vizuri kudebate kwa maendeleo(issues)sio propaganda. nchi inaongozwa kwa misingi ya katiba sio katiba ya ccm.
ndugu kassuwi,kumbuka maneno ya busara ya mmoja wa waasisi wa ccm(baba wa taifa-Mwl Julius K.Nyerere)."MIMI NANG'ATUKA LAKINI NAENDELEA KUAMINI BILA CCM MADHUBUTI NCHI YETU ITAYUMBA" tafakari maneno hayo,nchi inayumba au la,natumaini Mwalimu angekuwepo angewambia acheni propaganda tumikieni wananchi sio wewe.
Mambo ya maendeleo ya nchi sio sawa na ushabiki wa Simba na Yanga. Ukiona chama cha siasa lengo lake ni "kushinda uchaguzi" ujue kuna tatizo. Kushinda uchaguzi ni matokeo. Tukiangalia pointi zako tano moja baada ya nyingine tunaona zinaacha maswali mengi tu:
Moja; Hakuna chama nchini ambacho kina ukabila au udini. Kama kingejaribu kujisajili Tendwa angekisambaratisha kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo hakuna chama kinachoweza kujitofautisha kwa kutokuwa na ukabila au udini. Hii ndio sababu pamoja na mke wa rais na mtoto wake kujitosa katika vinyang'anyiro vya kugombea uongozi wa kisiasa ndani ya CCM, hakuna mtu anayesema kwamba CCM ni chama chenye nepotism (upendeleo kwa ndugu). Sana sana watu wana mashaka tu na kiwango cha busara kwa baadhi ya watu (bila kutajana majina).
Mbili; CCM imekuwa ya kwanza katika ushirikishwaji wa watanzania wote walio nje ya nchi katika kutoa mchango wao ili kuleta tija na maendeleo ya taifa letu. Ni hoja yenye ukweli hii???? CCM imefanya nini kuhakikisha haki ya Watanzania walioko nje kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu inalindwa mpaka sasa? Hakuna hata mtu mmoja wa CCM anayeongelea suala hili.
Tatu; CCM imehakikisha kwamba Nchi yetu inatawaliwa kwa misingi ya kidemokrasia. Nchini Tanzania kuna demokrasia ya kutosha na hata kupitiliza. Mwananchi yoyote anao uhuru wa kuishi, kuabudu na kufanya maamuzi apendayo ili mradi sheria za nchi zinazingatiwa. Ni kweli kwamba nchi yetu inatawaliwa kwa misingi ya kidemokrasia lakini ni vigumu kusema kwamba ni kwa sababu ya CCM. Katiba ya nchi inampa kila Mtanzania HAKI ya kuishi na kufurahia maisha. Ukiangalia matatizo ya hivi karibuni kuna mashaka juu ya serikali kulinda haki ya kuishi ya Watanzania. Marehemu Mwangosi aliuawa na vyombo vya dola vyenye jukumu la kulinda usalama wa raia kwa sababu tu alikuwa anaandika habari za vyama vya upinzani. Dk Ulimboka alinusurika kuuawa na mtu ambaye kwa mujibu wa Dk Ulimboka mwenyewe ni mfanyakazi wa Ikulu. Mpaka sasa hakuna anayetaka tujue ukweli wa matukio haya mawili. Kuna viinimacho vya 'kesi mahakamani' vinaendelea.
Nne; CCM haina ubaguzi, kila mtu anayo nafasi. Chama cha mapinduzi siku zote kimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba Serikali na vyombo vyote vya umma vinatoa nafasi zilizo sawa kwa raia wote, wanawake na wanaume bila kujali rangi, kabila, Dini, au hali ya mtu.
Hiki ni kichekesho. Sasa hivi kuna chaguzi za CCM zinaendelea. Kila uchaguzi umegubikwa na rushwa. Bila hela huwi kiongozi. CCM ina ubaguzi bubu. Hata mwenyekiti wenu kazungumza hayo mambo ya rushwa na makundi na mitandao ambayo inawasumbua.
Tano; CCM iko mstari wa mbele katika kuimarisha uhusiano mwema na Vyama vyote vya Siasa vya Nchi nyingine vyenye itikadi kama ya CCM ambavyo kweli vinapinga Ukoloni, Ukoloni Mamboleo, Ubeberu na Ubaguzi wa aina yoyote.
Bila mifano hii ni propaganda. Kuna nchi ngapi duniani zinatawaliwa na wakoloni? CCM inashirikiana vipi na vyama vyao kwa sasa?
Utanzania kwanza, vyama baadaye. Kama serikali ya CCM ikifanya kazi nzuri itashinda uchaguzi. Lakini kama mnalala na kuamka kuwaza kushinda uchaguzi mtaishia kuchakachua tu kura, kitu ambacho hakimsaidii yeyote zaidi ya walafi wa madaraka.
Post a Comment