ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, November 3, 2012

Siri nzito uhaba wa mafuta

 Waziri atangaza kufuta leseni za mafuta
         Mbunge CCM ataka `kuishughulikia` Serikali
Hatma ya ukosefu wa mafuta nchini hususani ya dizeli na petroli imegubikwa na utata, kutokana na serikali kutoa taarifa zinazopingana.
Mazingira Wakati Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, akiliambia Bunge, mafuta yameanza kusambazwa, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) imesema utekelezaji wake bado haujaanza.
wakati hali ikiwa hivyo, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ametangaza kufutwa leseni za biashara ya mafuta kwa kampuni zilizokiuka taratibu.

Pia ameivunja bodi ya kampuni ya uingizaji mafuta nchini (PIC) kwa madai kuwa inaundwa na wajumbe walio wafanyabiashara ya mafuta wasiokuwa na uwezo katika sekta hiyo.
Lakini hali ilivyo sasa, mikoa kadhaa kadhaa imejikuta katika kadhia hiyo, hali iliyomsababisha Mbunge wa Mwibara (CCM), Alphaxard Lugora kulitaka Bunge lisitishe shughuli zake jana na kulijadili tatizo hilo.
Hatua ya Lugora imeilazimisha serikali kutoa tamko la awali bungeni, kupitia kwa Simbachawene, ikisema limeshaanza kushughulikiwa na hali imeanza kurejea kuwa ya kawaida.
Wakati Bunge likielezwa hivyo jana, Meneja Mawasiliano wa Ewura, Titus Kaguo, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa, hali ya upatikanaji mafuta bado ni ngumu.
Katika tukio la bungeni, baada ya Spika Anne Makinda kumaliza matangazo jana asubuhi, Lugora alitumia kanuni ya 47 kutaka shughuli za Bunge zisitishwe, badala yake kujadiliwa hali ya dharura ya uhaba wa mafuta nchini.
Hoja hiyo iliungwa na wabunge wengi kupitia mfumo wa kusimama, ambapo walikuwemo wa CCM na wanaotokana na vyama tofauti vya siasa kikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Akiwasilisha hoja hiyo, Lugora alisema upatikanaji wa nishati hiyo hususani dizeli na petroli ni mbaya kuliko maelezo.
Alisema sasa hivi imefikia hatua ambapo mteja akienda kununua bidhaa hiyo kwenye vituo vya mafuta, anapimiwa kwa `vibaba’. “Mimi mwenyewe niliambiwa nipewe lita 10 ili wengine waweze kupata,” alisema.
Alisema hali kama hiyo inaweza kuwatokea watu tofauti wakiwemo wajawazito na wagonjwa wanaohitaji huduma ya gari maalum la kusafirishia wenye matatizo ya afya.
Lugora alisema kutokana na `unyeti’ wa jambo hilo, kuna wasiwasi wa kukwepo kwa hujuma kutoka kwa kampuni kubwa, ionekane Sheria ya Ununuzi wa Jumla (bulk procurement) imeshindikana hivyo kurejesha ununuzi wa rejareja.
Lugora aliomba wabunge wamuunge mkono hoja yake hiyo, ili kupata ufumbuzi wa tatizo hilo, ambapo idadi kubwa ya wabunge ilifanya hivyo.
Hata hivyo, serikali kupitia kwa Simbachawene, ilisema hali ya mafuta itarejea kama kawaida, baada ya tatizo lililosababisha kuwepo kwa uhaba wa nishati hiyo kushughulikiwa.
Naye Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, alitumia kanuni za 55 (F) na 59 (B) ya kuruhusu haki za Bunge, alihoji kuhusu uundwaji wa Kamati ya Nishati na Madini iliyovunjwa na Spika Makinda kutokana na kashfa za rushwa.
Kabla ya kutoa hoja hiyo ambayo hata hivyo ilikosolewa na Makinda, Mnyika alisema kwenye Bunge la bajeti iliyopita, serikali ilitoa taarifa ya utatuzi wa tatizo hilo na Novemba mwaka jana, lilipitisha maazimio ya kushughulikia gesi na petroli.
Alisema hatua hiyo ilifanyika kwa kuiruhusu Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ifuatilie suala hilo lakini kwa bahati mbaya ilivunjwa.
“Nchi haina mafuta, kamati imevunjwa, matatizo yanashindwa kushughulikiwa kwa sababu ya kukosa kamati,” alisema.
Akiikosoa hoja ya Mnyika, Makinda alisema suala hilo liliwasilishwa na Mbunge huyo kwa njia ya barua na linafanyiwa kazi.
Lakini kutokana na hoja ya Lugora, Makinda alimuita Naibu Waziri kuijibu, ambapo (Simbachawene) alisema Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, yupo jijini Dar es Salaam kufanikisha suluhu ya kudumu.
Alisema chanzo cha tatizo kilitokana na makosa ya kuruhusu meli za mafuta zinazopitia bandari ya Dar es Salaam kwenda nje ya nchi, bila kutambua kiwango cha mafuta kilichopo nchini.
Simbachawene alisema suala hilo limeshughulikiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (Ewura), Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) na Mamlaka ya Bandari (TPA).
“Kwa hali ya sasa tatizo hili limeshughulikiwa tumeamua kuchukua mafuta ya on transit (yanayopitia nchini kwenda nje ya nchi),” alisema.
Alisema kwa upande wa Dar es Salaam tatizo hilo limekwisha kwa kuwa mafuta yameshajaa na magari makubwa yameanza kuchukua mafuta kwenda mikoani.
“Tunaamini kuwa tatizo hili halitarejea tena,” alisema Simbachawene na kuongeza kuwa waziri atatoa taarifa rasmi kwa kuzungumza na waandishi wa habari.
Akifunga hoja hiyo, Spika aliagiza serikali itoea taarifa rasmi siku ya Jumatatu bungeni.
EWURA YATOA TAARIFA TOFAUTI
Kwa upande wake Ewura imesema katika kukabiliana na uhaba wa mafuta, serikali imezuia lita milioni 40 za mafuta zilizokuwa zinasafirishwa kwenda nje ya nchi. Mafuta hayo sasa yanatarajiwa kuuzwa nchini ili kuziba pengo linalotokana na uhaba uliopo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Meneja Mawasiliano wa Ewura, Titus Kaguo, alisema akiba ya lita milioni 80 zilizokusudiwa kusafirishwa kwenda nje, zilipunguzwa kwa kiwango cha asilimia 50.
Alisema serikali imeshatoa vibali kwa baadhi ya kampuni za mafuta, ili ziyauza hapa nchini ambapo mpaka sasa, kampuni tisa zimeridhia maombi hayo. Hatua hiyo itawezesha `kusambaza’ lita milioni 26.6 za petroli na diseli pamoja na mafuta ya taa yenye ujazo wa lita milioni 1.48.
Hata hivyo, wakati Simbachawene akisema mafuta hayo yameshasambazwa sokoni, Kaguo alisema utekelezaji wake haujaanza, kwa vile kampuni hizo hazijatimiza masharti ya Mamlaka ya Mapato (TRA) ikiwemo kulipa kodi ya asilimia 100.
Alizitaja kampuni hizo kuwa ni Mogas, Gapco, GBP, Lake Oil, Hass Petroleum, Puma, Oryxy, Engen na Camel. Hata hivyo, alisema tatizo la mafuta linatarajiwa kumalizika kwa kipindi kifupi (hakutaja) ambapo meli zilizoshindwa kupakua mafuta kutokana na kukosa nafasi ya kutia nanga, zitakakapofanya hivyo.
Alisema kutokana na ucheleweshaji, meli hizo zilisubiri kwa siku 19 bila kupakuliwa, hivyo kutumika kwa akiba ya Agosti mwaka huu, iliyokuwa kwa wafanyabiashara. Kwa mujibu wa Kaguo, kipindi hicho hapakuwa na meli iliyoleta mafuta, hivyo kusababisha uhaba wa mafuta bidhaa hiyo.
Hata hivyo, Kaguo alisema kuanzia Novemba 6 hadi 9 mwaka huu, meli zitaanza kupakuliwa mafuta na kuanza kuingia sokoni.
Akizungumzia akiba ya mafuta yaliyopo kwa sasa alisema kuwa kuna diseli lita milioni 35.8 ambayo ni matumizi ya siku 10, petrol lita milioni 16.2 ambayo ni matumizi ya siku tisa. Pia alisema yapo mafuta ya ndege yapo lita milioni 11.7 matumizi ya siku 25 na mafuta ya taa yapo lita 558,180.
WAZIRI AJITOKEZA , ATANGAZA KUFUTA LESENI ZA MAFUTA
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema uamuzi alioufikiwa ulitokana na kampuni za mafuta kufanya kazi kinyume cha taratibu huku wajumbe wa PIC wakihusika kulinda maslahi yao kibiashara.
Uamuzi huo, aliutangaza jijini Dar es Salaam jana jioni, baada ya kukutana na wafanyabiashara ya mafuta na waandishi wa habari.
Alisema sababu ya uhaba wa mafuta ni kile alichokiita kuwa ni ‘mvutano wa kizembe’ kati ya Ewura, bodi ya PIC na wafanyabiashara.
Profesa Muhongo alisema kutokana na mvutano huo, baadhi ya wafanyabiashara waliamua kupeleka mafuta nje ya nchi, wengine wakayaficha kwenye maghala kwa kisingizio kuwa bei elekezi haiwalipi faida.
Alisema kuna baadhi ya kampuni zilipewa leseni ya kuagiza mafuta, lakini biashara zao zilikuwa za mfukoni na kuisababishia serikali hasara na usumbufu.
Kutokana na hali hiyo, aliiagiza Ewura kuzifutia leseni kampuni zilizoshindwa kuingiza mafuta kwa kipindi cha miezi sita na taarifa hiyo kumfikia Jumatatu ijayo.
Profesa Muhogo alisema bodi ya PIC imevunjwa kutokana na kuwa na wafanyabiashara ambao kazi kubwa walioifanya ni kulinda biashara zao.
“Sasa bodi mpya itakayoundwa itakuwa ya kisasa na itakuwa na mjumbe mmoja mmoja kutoka idara husika na mwenyekiti atatoka wizarani,” alisema.
Alisema wajumbe wa bodi hiyo wataoka Mamlaka ya Mapato (TRA), Mamlaka ya Bandari (TPA), Kampuni ya kupakua na kupakia makontena bandarini (TICTS), PIC na Ewura.
Alisema bodi mpya inatarajiwa kuanza kazi ifikapo Jumanne ya wiki ijayo.
MNYIKA: POKEENI TAARIFA ZA SERIKALI KWA TAHADHARI
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, amesema umma unapaswa kupokea kwa tahadhari taarifa zinazotolewa na Wizara ya Nishati na Madini na taasisi zake nje ya Bunge.
Alisema taarifa hizo ni zile zinazohusu masuala ya sekta ya nishati ikiwemo uhaba wa mafuta uliopo sasa, hivyo kusisitiza umuhimu kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospter Muhongo, atoe taarifa bungeni kuhusu masuala tajwa.
Aidha, Mnyika alisema Spika Makinda anapaswa kutoa maelezo bungeni ya kuelekeza Kamati ya Kudumu ya Bunge, itakayochambua ukweli wa taarifa hizo.
“Kujirudia mara kwa mara matatizo katika sekta za nishati hususan katika biashara ya mafuta, kumechangiwa na sababu za udhaifu wa kisera, kimaamuzi, kiusimamizi na kiutendaji wa baadhi ya viongozi na watendaji wengine…” alisema Mnyika.
Mnyika alidai kuwepo taarifa kuwa uhaba huo ni matokeo ya baadhi ya wamiliki wa vituo vya mafuta, kuficha petroli na dizeli wakisubiri kutangazwa kwa bei mpya ya bidhaa hizo.
Kwa mujibu wa Mnyika, matatizo katika biashara ya mafuta hayahusu uhaba wa dizeli na petrol tu, bali pia kasoro katika ununuzi wa mafuta ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme.
Habari hii imeandikwa na Beatrice Bandawe, Dodoma, Mashaka Mgeta na Beatrice Shayo, Dar es Salaam.
CHANZO: NIPASHE

No comments: