ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 30, 2012

ZANZIBAR HEROES ILIVYOICHAPA RWANDA NA NIYONZIMA 'NDANI' JANA 2-1



Wachezaji wa Zanzibar Heroes wakisujudu wakati wakishangilia goli lao la kwanza lililofungwa wakati wa mechi yao ya Kundi C la Kombe la Chalenji kwenye Uwanja wa Mandela, Kampala leo.

Selemani Kassim 'Selembe' wa Zanzibar Heroes akiwatoka wachezaji wa timu ya taifa ya Rwanda (Amavubi) wakati wa mechi yao ya Kundi C la michuano CECAFA Challenge kwenye Uwanja wa Nelson Mandela uliopo Namboole nchini Uganda jana. Zanzibar Heroes walishinda 2-1. Habari na Picha kwa hisani ya Straika Blog
**********************LICHA ya mazingira magumu ya uwanja uliojaa tope kama shamba la mpunga, timu ya Zanzibar Heroes walipambana kishujaa na kushinda kwa magoli 2-1 mechi yao ya Kundi C la Kombe la Chalenji jijini Kampala dhidi ya Rwanda jana jioni. 
Nyota wa klabu ya Azam FC ya Dar es Salaam, Khamis Mcha 'Viali' alifunga mara mbili na kuifanya Zanzibar ifikishe pointi 4 baada ya mechi mbili na sasa ina uhakika wa kutinga hatua ya 8-Bora hata kwa nafasi ya ‘best looser’ kulingana na matokeo ya mechi za mwisho. 
Rwanda inayoshika nafasi ya pili ya msimamo wa Kundi C kwa kuwa pointi 3 na Malawi iliyo katika nafasi ya tatu kwa pointi 3 pia baada ya jana kushinda 3-2 dhidi ya Eritrea inayoburuza mkia, zinaweza kufikisha pointi 6 zikishinda mechi zao za mwisho Jumamosi. Hata hivyo, matokeo hayo hayataizuia Z’bar kutinga robo fainali kama ‘best looser’, endapo itapoteza mechi yake ya mwisho Jumamosi dhidi ya Malawi. 
Hali mbaya ya uwanja iliwagharimu pia Malawi na Eritrea, ambapo katika matukio mawili -- moja kwa kila timu -- mpira uliokuwa ikiserereka kuingia wavuni ulikwama kwenye dimbwi la maji kabla ya kuokolewa na mabeki wa timu hizo. 
Katika tukio la kwanza wakati Malawi wakiongoza kwa magoli 2-0 wangeweza kufunga goli la tatu baada ya mpira kumpita kipa na mchezaji mchezaji wa malawi kupiga shuti dogo katika lango tupu akidhani amefunga lakini mpira ulikwama kwenye dimbwi kabla ya beki kufika na kuokoa mpira.
Tukio jingine lilikuja wakati Eritrea wakiwa nyuma kwa magoli 2-1 na wangeweza kufanya matokeo yawe 2-2 lakini mpira uliokuwa ukienda wavuni ulinasa kwenye dimbwi na kuwapa nafasi Malawi kuokoa. 
Zanzibar ilipata goli la kuongoza katika dakika ya 9, shukrani kwa madimbwi ya maji yaliyouzuia mpira usimfikie kipa wa Rwanda, Jean Claude Ndoli, aliyekuwa katika nafasi nzuri ya kuuokoa jirani na ukingo wa boksi na kumpa mwanya Mcha kufunga katika nyavu tupu.
Mcha alifunga goli la pili katika dakika ya 62 kufuatia pasi ndefu kutoka kulia.
Rwanda walicharuka na kupata goli kupitia kwa Dady Birori aliyefunga kwa kichwa katika dakika ya 80 kufuatia krosi ‘matata’ ya nahodha Haruna Niyonzima.
Kocha wa Rwanda, Milutin Sredjovich ‘Micho’ alisema baada ya mechi hiyo kwamba hawezi kusingizia uwanja kwa kipigo chao kwa sababu hata wapinzani wao walicheza katika uwanja huo huo lakini alisema mazingira yalikuwa hayafai kuendelea kuchezewa mechi.
Michuano hiyo inaendelea kesho kwa mechi za Kundi A ambapo Kenya itacheza dhidi ya Ethiopia saa 10:00 jioni kabla ya wenyeji Uganda ambao tayari wametinga robo fainali watawakaribisha Sudani Kusini saa12:00 jioni.

No comments: